Juni 13, 1980 alifariki dunia mwanazuoni na mwanamapinduzi
aliyejipambanua kwa itikadi kali za kijamaa (Marxist) raia wa Guyana Walter Anthony
Rodney. Mwanazuoni huyo alijikita katika kuonyesha namna Ubeberu, Ukoloni
mamboleo na Uliberali mamboleo, ulivyoididimiza Afrika.
Rodney alikuwa mwanahistoria maarufu sana duniani na
mwanaharakati wa kisiasa na msomu ambaye aliuawa mwaka 1980 huko Georgetown,
Guyana akiwa na umri wa miaka 38. Alisoma katika chuo kikuu cha West Indies
huko Jamaica na mnamo mwaka 1963 alihitimu shahada yake katika Historia na
alishinda tuzo ya Sanaa katika kitengo chuoni hapo.
Aliuawa kwa bomu la kutegwa katika gari lake, ukiwa ni mwezi
mmoja baada ya kutoka kusheherekea uhuru wa Zimbabwe. Wakati huo ulikuwa ni
mgumu katika harakati za Kisiasa nchini humo. Aliacha mke aliyefahamika kwa
jina la Patricia na watoto watatu. Kaka yake Donald Rodney alijeruhiwa katika
mlipuko huo. Sajenti wa Jeshi la Ulinzi nchini Guyana aliyefahamika kwa jina la
Gregory Smith alikaririwa akisema kuwa yeye ndiye aliyempa bomu Rodney
lililomuua siku hiyo.
Baada ya kutekeleza mauaji hayo Smith alikimbiana kwenda
uhamishoni French Guiana ambako alifariki dunia 2002. Ilikuwa ikiamini hivyo
lakini haikuthibitishwa kwamba kuuawa kwake kulipangwa na Rais wa Guyana wakati
huo Linden Forbes Burnham. Alirudi Guyana mnamo mwaka 1974 akitokea Tanzania.
Wakati Rodney akiwa nchini Tanzania kama Mhadhiri wa Chuo
kikuu cha Dar es salaam alitumia muda wake mwingi katika shuguli za kimapambano
kupinga ubeberu na Ukoloni uliokuwa ukiendelea kusini mwa jangwa la Sahara,
bega kwa bega na baadhi ya wanafunzi wa mrengo wa kimapinduzi akiwemo Karimu
Hirji mwenyewe.
Uhalisia wa fikra za Walter Rodney upo katika kitabu chake
cha ‘Jinsi Ulaya iliyodumaza maendeleo ya Africa’ (How Europe Underdeveloped
Africa) kitabu alichokiandika mwaka 1972,
Ni dhahiri kwamba hakuna njia mbadala yenye kufaa, unapohitaji
kuielewa historia ya jamii fulani bila ya kuangalia historia ya mahusiano ya
kijamii katika uzalishaji mali na umilikaji njia kuu za Uchumi, kwakuwa mfumo
mzima wa Uzalishaji mali na umilikaji njia kuu za Uchumi ndio kiini cha
migogoro katika historia ya mwanadamu toka kuwepo kwake.
Historia hiyo ndio msingi upelekeao uchambuzi yakinifu wa
jamii sasa na badae. Hivyo basi hatuwezi jadili Afrika ya sasa pasipo kuitazama
histroia yake katika vipindi vikuu vine; Kabla ya maingilio ya wageni kutoka
ulaya(1500 A.D), Wakati wa mahusiano na wageni wa ulaya (1500-1884 A.D), Wakati
wa Ukoloni mkongwe na Baada ya Uhuru. Katika vipindi hivyo vyote vinne ni
kipindi kimoja tu cha kabla ya mwaka 1500 A.D bara letu la Afrika lilikuwa na
ahuweni ya kupumua, kujiamlia huku likifuata njia yake ya kiustarabu katika
maendeleo halisi ya binadamu.
Lakini baada ya miaka 1500 kile kilichoitwa ustarabu wa wazungu/
Ulaya yaani biashara ya utumwa, Ukoloni na ubeberu havijawahi kuicha Afrika na
watu wake wakipumua. Biashara ya Utumwa ambayo kimsingi haikuwa biasahara bali
ni Vurugu za kijamii ‘Social Violence’ (Rodney 1972) ilidumu kwa karne nne
iliambatana na vifo vya mamiliioni ya Waafrika huku ikivuruga mpangilio wa
kistarabu wa watu wa Afrika katika kujiletea maendeleo yao kama jamii huru.
0 Comments:
Post a Comment