Watu waliojiunga katika vikundi mbalimbali vya
kuweka na kukopeshana fedha (VICOBA) wametakiwa kuchukua tahadhari na kuwa
makini zaidi katika masuala yanayohusu usimamizi wa fedha ili kuondokana na
tatizo la wizi ama upotevu wa fedha zao.
Akizungumza na uongozi mpya wa kikundi cha Prosperity
Vicoba Group (PVG) mjini hapa, kwa niaba ya Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika
Mkoani Kilimanjaro John Henjewele, Afisa Ushirika Wilaya ya Moshi Vijijini
Eliona Omari alifafanua kuwa viongozi walioingia madarakani lazima wafuatilie
utekelezaji wa shughuli walizozipanga na wanachama hao na kufanya tathmini za
mwaka mzima.
Aliwataka viongozi na wanachama wa kikundi hicho
kuhakikisha kuwa, fedha zinazotolewa na halmashauri zinawekewa mikakati na miradi ya pamoja ili
kufanikisha malengo yaliyokusudiwa ya uchukuaji wa mikopo hiyo.
“Kinachoua hii miradi ni kutokuweka mikakati ya pamoja
ya kuhakikisha miongozo na taratibu zilizopo zinafuatwa kama sehemu ya
usimamizi makini wa fedha, hivyo uongozi uhakikishe unazingatia miongozo hiyo
na taratibu zilizopo za udhibiti wa fedha,” alifafanua Omari.
Aliendelea kufafanua kuwa, ili mwanachama aweze
kuchukua mkopo wake ni vyema akawa na malengo madhubuti ya fedha hizo na ikiwa
ataona lengo hilo halitafanikiwa ni bora kuacha kuchukua mkopo huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Prosperity
Vicoba Group (PVG), Bahati Nyakiraria aliwataka wanachama wake kuisoma katiba
na kuielewa vizuri kwani wengi wamekuwa hawasomi, ili kutambua haki na wajibu
wao.
“Msiwe watu wa kuja na kuweka Hisa zenu tu, pia kuna
haki zako lakini pia kuna haki za kulinda wenzako, kuna utaratibu wa kufahamu
kikundi kinaendeshwaje, wajibu wako na wajibu wa kikundi,” alifafanua
Nyakiraria.
Naye Mwezeshaji wa kikundi hicho, Bi. Devotha Membe
aliwataka wanakikundi kukopa kwa malengo waliyoyakusidia kwani wana Vicoba
wengi wameingia kwenye madeni makubwa kutokana na wengi wao kuwa na vikundi
vingi na wamekuwa wakikopa fedha kundi kimoja na kwenda kulipa deni kwenye
kikundi kingine jambo ambalo limesababisha baadhi yao kukamatiwa mali zao.
Viongozi waliochaguliwa ni Bahati Nyakiraria
Mwenyekiti, Katibu Samuel Shao, Mweka hazina Kennedy Massawe, wengine ni Ester
Kimario, Irine Mushi, Victoria, Salome Minja, Winfrida Nyella na Emma Mushi.
0 Comments:
Post a Comment