Wednesday, June 17, 2020

Ifahamu wilaya ya Rombo na vivutio vya utalii

Kwa mujibu wa TUKI (2004:445) utalii ni hali ya kusafiri mbali au kuvinjari huku na huko ili kufurahia mandhari. 

Upo utalii wa aina mbalimbali kama vile wa asili, kiutamaduni na mambo ya kale.  Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu sana katika maendeleo ya nchi na ni sekta ambayo huliingizia taifa pato la kiuchumi. Sekta hii huhusisha watu wa jamii mbalimbali duniani, watu wenye tofauti za kiutamaduni, kiuchumi, kiitikadi, kijamii na wanaozungumza lugha tofauti.

Kulingana na Benavides (2001) utalii una nafasi kubwa katika uchumi wa Tanzania. Ni moja kati ya vyanzo vikuu vya fedha za kigeni na unatoa nafasi za ajira kwa jamii. 

Hivyo basi, inaonekana kuwa utalii ni tasnia muhimu sana katika kuongeza upatikanaji wa kazi, kuondoa umaskini na upatikanaji wa fedha za kigeni. 

Kufikia mwaka 2015 pato la utalii kwenye uchumi wa taifa la Tanzania linategemewa kufikia dola za Kimarekani milioni 3,699.4.

Kutokana na umuhimu wa sekta ya utalii nchini, ipo haja ya kuwa na na vyanzo vya taarifa ambavyo vinafikisha mawasiliano sahihi kwa wageni ili kutangaza vivutio vya utalii na utamaduni wa jamii kwa ujumla

Pamoja na hayo, utalii ni eneo ambalo bado halijafanyiwa kazi vya kutosha katika ukuzaji wa sekta ya utalii katika wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Wilaya ya Rombo ni miongoni mwa wilaya saba za mkoa wa Kilimanjaro upande wa Mashariki ya mlima, makao makuu ya wilaya hiyo yanapatikana katika mji mdogo wa mkuu uliopo kata ya Kelamfua Mokala, Wenyeji wa wilaya hiyo ni Warombo walio sehemu ya Wachagga.

Wilaya ya Rombo imepakana na Kenya upande wa Kaskazini na Mashariki, wilaya ya Hai upande wa Magharibi na wilaya ya Moshi vijijini upande wa Kusini, katika sensa ya mwaka 2012 idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ni 260,963.

Katika Wilaya ya Rombo kuna maeneo mbalimbali ambayo ni vivutio vya utalii, maeneo hayo ni pamoja na Ziwa Chala, Vilele vya Mlima Kilimanjaro (Mawenzi na Kibo), Kaburi la Mangi Horombo na Mahandaki yaliyotumika kama maeneo ya maficho wakati wa Vita.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo Godwin Chacha anasema baadhi ya vivutio vilivyopo katika wilaya hiyo  ni pamoja na kaburi la Mangi Horombo, Handaki lenye urefu wa mita 68 lililotumiwa katika vita kati ya Warombo na Wamasai wakati wa vitana watu kujificha.

Anasema yapo pia maeneo ya utalii wa kupanda milima, utalii wa picha, utalii wa ndege na wanyama wadogowado Kima, Tumbili na Nyani, utalii wa utafiti, utalii wa utamaduni (ngoma, vyakula vya asili, michezo na matambiko. Vingine ni maeneo ya kijiografia kama  vile Ziwa Chala na maparomoko ya maji.

Anasema Utamaduni mwingine ni kufundisha watu kupika vyakula vya asili ya kichaga, kuwatembeza watalii kwenye mapango ya asili, kuwatembeza kwenye kijiji na kuona jinsi wanavyoishi na kupika vyakula vya asili wanavyokula.

Anasema mtalii anapotembelea kijiji pia atanufaika na ushuhuda wa kuona nyumba za asili walizokuwa wakiishi wachaga zamani, vyakula vya asili wanaoviita kwa majina yao asili.

Aidha anasema pia kuna utalii wa ngoma za asili za wachaga, vifaa vilivyokuwa vikitumika kubebea vyakula vikavu na matunda na kupepea mazao ya nafaka.

Chacha anasema wilaya ya  Rombo ipo katika mkakati wa kuyatunza maeneo yenye  vivutio vya asili na kubakia katika hali ya uasilia wake ikiwemo Ikulu ya Mangi Selengia aliyokuwa akiitumia wakati wa utawala wake lengo likiwa ni kuendelea kuvidumisha vivutio hivyo.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni  wa wilaya ya Rombo Florentine Henrico Langu, anasema Utalii wa Utamaduni katika wilaya hiyo unaweza kukuza utalii wa ndani kutokana na wilaya hiyo kuwa na vivutio vingi vya asili.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuzitaka Wilaya zote hapa nchini kuhakikisha kwamba utalii wa asili uliopo kwa kila halmashauri unafufuliwa ili kuongeza pato la wilaya, jambo hilo litachochea watu wengi kuvitembelea vivutio hivyo,”alisema Mwl Langu.

Anasema wilaya ya Rombo imeanza mkakati wa kufungua utalii uliosahaulika kama kaburi la Mangi Horombo, hali itakayosaidia kuendeleza utalii utakaokumbukwa na kujulikana kwa vizazi vijavyo.

SUALA LA VILELE VYA MLIMA KILIMANJARO
Vilele vya mlima huu vinapatikana Wilaya ya Rombo, njia inayotumika kupandia mlima Kilimanjaro ambayo ipo Rombo inajulikana kwa jina la Nalemuru route, ili kufika njia hii ni km. 95 toka Moshi Mjini.

Njia ya Nalemuru inapitika kwa urahisi na ina vivutio vya wanyama mfano Mbega, Tembo, Nyani, Kima, Tumbili, Ng’edere, Ngiri, Simba wachache, Mbwa mwitu, Mbweha na Wanyama wengine.

KABURI LA MANGI HOROMBO
Kaburi la Mangi Horombo lipo Tarafa ya Mengwe kata ya Mengeni takribani umbali wa mita sabini toka barabara kuu ya lami itokayo Moshi kwenda Tarakea.

Kaburi la Mango Horombo lina mvuto wa kipekee kutokana na urefu wa Mangi Horombo ambaye alikuwa na urefu wa futi nane na inchi mbili (Futi 8.2”) kimsingi linakumbusha historia ya Warombo kwa ujumla wake tangu alipofariki mwaka 1802. 

MAHANDAKI YALIYOTUMIWA NA MANGI
Katika kumbukumbu ya vita kati ya Warombo na Wamasai, kuna mahandaki katika eneo la kijiji cha Mamsera Tarafa ya Mengwe lenye urefu wa mita 68 chini ya mlima Uwa.

Katika handaki hilo lililotumiwa na watu kujificha lina vyumba ambayo vilitengwa kwa matumizi mbalimbali yakiwemo jiko, malazi sehemu ya kuwaficha watoto na vyumba kwa ajili ya walinzi.

Handaki hilo liligundulika mwaka 2007 na mwananchi mmoja wa eneo hilo, hivyo anatoa wito kwa wananchi toka ndani na nje ya nchi kuja kuliona na kupata historia ya kabila la Warombo.

Kwa ujumla serikali ina mipango mingi katika utalii lakini inapaswa inatakiwa pia kulinda na kuhifadhi rasilimali za asili na za kiutamaduni badala ya kuangalia upande mmoja tu wa kipato na ajira. 

0 Comments:

Post a Comment