Binafsi huwa nina
swali moja ambalo huwa napendelea sana kuwauliza watu. Nalo ni zaidi ya jibu
kwani ni mchakato wa mawazo ambao unanifanya niwe na furaha. Swali hili huwa
linanipa upekee wa kumtazama mtu ninayemuuliza, lakini pia huwa linanipa fursa
ya kuwa na mtu huyo katika vilindi vya ndani. Baada ya kujifunza majibu yao
huwa naona ni bora kujijibu mwenyewe. Jibu lenyewe ni Mwanamke.
Umewahi kujiuliza
swali hili? Dunia ingekuwaje bila ya mwanamke? Umewahi kujiuliza kuhusu kauli
ya mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Nietzsche (1844 –1900) aliyosema,
“Mwanamke lilikuwa kosa la pili la Mungu”.
Mwanamke wa shoka
nchini Marekani Oprah Winfrey ana nukuu yake mahiri inayosema, “Fikiri kama
Malkia. Malkia haogopi kushindwa. Kushindwa ni hatua ya kukufikisha katika
Ukuu.”
Pia mwanamke wa
shoka nchini Marekani, mwandishi wa habari na mwanaharakati wa kijamii na
kisiasa Gloria Marie Steinem aliyepambana kwa kiasi kikubwa na kupata umaarufu
mkubwa miaka ile ya 1960 hadi 1970 kumtetea mwanamke kwa njia mbalimbali
ikiwamo kuanzisha jarida la Ms. alisema, “Hadithi ya mapambano ya kutaka usawa
kwa wanawake sio ya mwanamke mmoja au shirika moja lakini ni juhudi za pamoja
za wote wanaojali haki za binadamu.” Nukuu hii inafaa kupigilia msumari Dunia
ni mahali salama pa mwanamke na anaweza kushika hatamu za uongozi na mambo
yakaenda.
Kwa miaka elfu sasa
mwanamke amekuwa hapewi nafasi ya kufanya maamuzi mbele ya jamii hata kama
uwezo wa kufanya hivyo. Harakati zinaendelea kutupia jicho jinsi hii, wachache
waliobuka na kuongoza jamii kufanya maamuzi wameonekana kuwa wanaweza.
Katika makala haya
tutamwangazia mwanamke wa shoka nchini Tanzania miongoni mwa wengi waliopo,
aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikali. Huyu ni Bi.
Bernadetha Kinabo, ambaye kwa sasa amestaafu utumishi wa umma baada ya zaidi ya
miaka 22.
Bi. Kinabo anaanza
kwa kuweka bayana nafasi ya mwanamke katika kuongoza jamii kwa mifano. “Nchi za
Scandinavia wapo wanawake ambao ni Marais na Mawaziri wakuu wanatawala hadi
leo. Hapa Tanzania Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere aliweka misingi mizuri
kwa akina Mama alishirikiana nao bega kwa bega katika utawala wake,” anafafanua
mama Kinabo na kuwataja baadhi ya wanawake waliofanya vizuri wakati wa utawala
wa Baba wa taifa mwalimu Nyerere kuwa ni Lucy Lameck na Bibi Titi Mohammed.
Anatoa mfano wa
wanawake waliotawala na wanaotawala katika maeneo mengine duniani kama vile
Angela Merkel wa Ujerumani, alikuwapo Margaret Thatcher wa Uingereza, Indira
Gandhi wa India, na Golda Meir wa Israel ambao anawataja kama wanawake wa shoka
waliosoma na kuongoza, na kuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji ambao uliwazidi
hata viongozi wa jinsi ya kiume.
“Hata sasa uongozi
wa awamu ya Tano tunaye Makamu wa Rais mwanamke Mhe; Samia Suluhu Hassan ambaye
anafanya kazi nzuri sana na katika mkoa wetu wa Kilimanjaro tunaye Dkt. Anna
Mghwira ambaye ni mama mahiri wenye kujiamini,” anafafanua Bi. Kinabo.
SIRI YA MAFANIKIO KATIKA UONGOZI
Bi. Kinabo anasema
mafanikio makubwa katika utumishi wake wa zaidi ya miaka 20 katika vitengo
mbalimbali nchini yametokana na umakini na ushirikiano na watu ambao alikuwa
akifanya nao kazi.
“Mimi nimefanya kazi
kwa miaka 22 nikiwa Mkurugenzi mtendaji katika halmashauri mbalimbali hapa
nchini, nilipokuwa kiongozi sikuamini katika kukwamishwa katika nafasi yangu,
kwenye sehemu yangu ya kazi nilikuwa na nyenzo, watu, fedha, vifaa niliweza
kuvitumia vizuri na nikiwa na tatizo nilikuwa ninakaa na watumishi wenzangu.
Ushirikishwaji katika kazi ni jambo la muhimu sana,” anasema.
Aidha Mkurugenzi
huyo wa zamani wa Manispaa ya Moshi Mjini anasema umakini wa mwanamke unakuwa
mkubwa kuliko wa mwanaume kutokana kuwa mwoga.
“Mwanamke ni muoga,
mwanamke ni mtunzaji mzuri wa fedha sio mwizi tofauti na wanaume wanaangalia
mbele zaidi hata anapokuwa kazini anaweza kujiibia yeye mwenyewe tofauti na
mwanamke,” anafafanua Bi. Kinabo.
Hata hivyo Bi.
Kinabo anawataka wanawake wapende zaidi kujiendeleza kielimu ili kujinasua
katika mfumo dume na hatimaye kuwepo na usawa katika nafasi ambao utatokana na
uwezo wa kiutendaji na sio kama jinsi.
NAFASI YA MWANAMKE
KATIKA MAENDELEO
Bi. Kinabo anasema
uongozi unaojali, uongozi unaoonyesha njia, unatokana na wanawake kwani
wamekuwa viongozi kuanzia ngazi ya malezi ya familia na kuwataka wanawake
kuinuka sasa kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali kutoka ngazi ya chini hadi
taifa.
“Ukiangalia katika
Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asilimia 36 ni akina mama, Bunge
la Rwanda asilimia 48 akina mama, hivyo natoa wito kwa akinamama wenzangu kujitokeza kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi, katika manispaa ya Moshi takwimu zinaonyesha, idadi ya
watu zaidi ya asilimia 51 ni wanawake huwezi kuwadharau katika kuleta
maendeleo,” anasema Bi. Kinabo.
Bi kinabo anaweka
bayana kuwa bado kuna wanawake hawajabaki nyuma na kuongeza kuwa wapo baadhi
hadi sasa wanaamini lazima watawaliwe tu, na wapo wanaume wanaamini wao ndio
watawala tu jambo ambalo sio sahihi.
Mwanamke huyo wa
shoka miongoni mwa wanawake nchini anavutiwa sana na Mkuu wa Mkoa mwanamke Dkt.
Mghwira na kuongeza kuwa alimtambua alipojitosa kugombea nafasi ya Urais mwaka
2015 kwamba aliweza kuzunguka maeneo mengi hapa nchini, akiuza sera zake, na
kumtaja kama mfano mzuri wa kuigwa na wanawake nchini Tanzania, Afrika na dunia
kwa ujumla.
Gavana wa kwanza wa
Utah nchini Marekani na kiongozi wa kidini Brigham Young (1801-1877) aliwahi
kusema, “Unamwelemisha mwanaume, unakuwa umemwelimisha mwanaume.
Unapomwelimisha mwanamke, unaelimisha kizazi.” Hakika aliyewafungua macho
wazazi wa Bi. Kinabo kumpa elimu hawakukosea, kizazi cha watanzania kinajivunia
kuwa na mwanamke huyu ambaye ni miongoni mwa wengi waliowahi kufanya vizuri
katika ngazi za uongozi.
Bi. Kinabo alizaliwa Novemba 29, 1951 na kwa sasa yupo kwenye makazi yake mkoani Kilimanjaro. Amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini ikiwemo Mkurugenzi wa wilaya za Kinondoni Jijini Dar-es-salaam, Manispaa za Mbeya, Singida, Arusha na Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
0 Comments:
Post a Comment