Neno ‘Firauni’ ni jina ambalo lilitumiwa kuonyesha wafalme wa
Misri wa zamani; kama ulivyo msimbo wa Kaisari kwa wafalme wa Roma, Kisra kwa
wafalme wa Fursi (Iran ya sasa) na Najashi kwa wafalme wa Uhabeshi (Ethiopia ya
sasa).
Kwa mujibu wa Muhammad Jawad Mughniyya katika uchambuzi wake
aliangazia neno Musa na kulipatia ufafanuzi ambapo ‘Mu’ lina maana ya maji na
‘Sa’ lina maana ya mti. Sababu kuu aliyoitaja alisema mama yake Musa alimweka
katika sanduku, akalifunga kufuli na akalitupa katika mto Nile kwa kumhofia Firauni.
Waswahili tukaja na msemo wetu “Ukistaajabu ya Musa, Utaona
ya Firauni.” Tukimaanisha kuna baadhi ya mambo yanaweza kukufanya ukashangaa na
kushangaa pindi unapostaajabu lile unakutana na hili.
Ni kawaida kwa makabila mengi nchini kuzika miili ya wapendwa
wao katika mikoa au maeneo ya asili ya ukoo au familia husika. Ndio maana
baadhi ya watu wanapofariki dunia husafirishwa na kupelekwa kuzikwa katika
mikoa yao ya asili. Moja ya makabila yenye utamaduni huo ni Wachaga kutoka
katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Katika jamii ya Wachaga mkoani Kilimanjaro, Mchagga akifariki
taratibu za kumzika zinaandaliwa ambapo huoshwa vizuri na kuvishwa sanda ambayo
mila za zamani ilikuwa ni ngozi ya mnyama, kaburi lilichimbwa la urefu kama wa
mita sita kisha kutandazwa majani ya mgomba ndani ya kaburi na miti aina ya
“sale” pembezoni mwa kaburi kisha marehemu anawekwa ndani yake akiwa ameketi
akiutazama mlima Kilimanjaro kisha kufukia kwa kufuata utaratibu maalum.
Mila na desturi hizo zimedumu kwa muda mrefu lakini
zimeathiriwa na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali. Ujio wa dini na ustaraabu
wa magharibi na mashariki umeathiri muundo huo wa kuzikana kwa wachaga ambapo
Mchaga anapokufa anawekwa kwenye sanduku na taratibu nyingine za tamaduni hizo.
Katika makala haya tutamwangazia mwanaume mmoja wa Kijiji cha
Kifuni, Kibosho mkoani Kilimanjaro ambaye ana umri wa miaka 64 aliyepania kwa
udi na uvumba kwamba siku ya kufa kwake, siku hiyo hiyo akizikwa basi apandiwe
mti wa matunda na baada ya mwaka mmoja watu waende wakavune mazao ya mti huo
yaani matunda.
Kijiji cha Kifuni kipo umbali wa kilometa 20 kutoka mjini
Moshi kwa njia ya Kibosho na unapokwenda kijijini hapo barabarani kumepambwa na
mimea ya migomba na kahawa huko nyumba zikionekana na unachukua dakika
kuangazia nyumba hizo cha Wachaga huwezi kukosa kuliona kaburi.
Hali ya ubaridi, na ukungu jua likiwa limefichwa na mawingu
anaonekana mzee mmoja mwenye kimo cha futi 5 na inchi 7 akiwa amevaa koti kubwa
la kujikinga na baridi na kofia ya asili ya waingereza ambazo hupendelea
kuvaliwa na wazee (Kofia hiyo ambayo hufahamika kwa jina la Gatsby anaipendelea
sana mzee huyo). Mzee huyo mweusi kwa rangi ya ngozi yake, uso wake mrefu na
mashavu yenye dimples anakutana na mwandishi wa makala hii na kujitambulisha
kwa jina la Leonard Massawe.
Mzee Massawe amekuwa akifahamika kwa jina la Lepaje kutokana
na harakati zake katika utunzaji wa mazingira hususani kijijini kwao na
Kilimanjaro kwa ujumla kupitia taasisi yake isiyo ya kiserikali ya Lepaje.
Mzee huyo na mwanaharakati huyo wa mazingira mkoani
Kilimanjaro anasema kila akilala na akiamka akili yake ipo kwenye mazingira
kuyageuza kuwa fursa wakati huo huo yakiendelea kuwa sehemu ya mapambano dhidi
ya mabadiliko ya tabia nchini.
SABABU ZA KUTAKA KUPANDA MTI WA MATUNDA KWENYE KABURI LAKE
Watalaamu wa masuala ya uso wanasema uwepo wa ‘dimples’
katika uso wa mtu huwa unaashiria baadhi ya mambo kama; ubunifu, kazi, bahati,
umakini, kwenda na wakati ukisasa, watu wenye furaha, na wenye uwezo.
Wasomi hao wanasema ubunifu kwa watu wenye dimples ni
asilimia 77 na kuyatendea kazi wanayoyabuni hufikia asilimia 77.
Ubunifu ndio chanzo kikubwa cha mzee huyo kuona fursa ya
makaburi katika ardhi ya Uchagani ambayo imekuwa ikishikiliwa na mila zaidi
kuliko kwenda na wakati uliopo.
“Mimi nimewaambia
familia yangu pindi nitakapokufa, mwanangu nitakapokufa naomba nipandiwe mti wa
parachichi kikonyo, ili matunda yakishakomaa watu wachume wawe na uchumi mzuri
kwani hatuwezi kwenda kama uchumi wetu upo chini wakati huo huo tunashindwa
kuzitumia fursa, ” anasema Massawe.
Aidha Massawe anawahimiza Wachaga wenzake kuachana na tabia
ya kuishi kwa mazoea, huku akisisitiza kuwa kuna mazoea mengine hayawezi kuitoa
jamii katika lindi la umaskini.
“Ninaishauri jamii kuanza kubadilisha mitazamo yao kuwa
mpendwa wao anapofariki wanaanza maandalizi ya kumjengea kaburi, wanachotakiwa
kwa sasa ni kujenga mazoea ya kuotesha
miti ya maparachichi, machungwa na mipapai,”anasema Massawe.
MTAZAMO WA MTI WA MATUNDA KABURI KAMA FURSA UMEPOKELEWAJE?
Watu mbalimbali kuanzia kijijini kwake Kifuni na Kilimanjaro
yote wanatofautiana katika suala hilo huku walio wengi wakimuona mzee huyo kama
anazeeka vibaya kwani inaonyesha namna anavyoshindwa kuheshimu mila na desturi
za mababu zake wa Kichaga.
“Unajua kuna wazee wengine wanazeeka vibaya ndugu mwandishi,
sasa unaanza kupanda mti wa matunda kaburini halafu baadaye uje uuvune na ule
tena, yaani mimi nikijua haya mapapai, maparachichi yametoka hapo sijui
itakuwaje,” anasema Deodatus wa Kifuni.
Kwa upande wake mwanadada aliyejitambulisha kwa jina la Glory
mkazi wa Moshi anasema ulimwengu uliopo ni wa kuziangalia fursa zinazopatikana
kwa ajili maendeleo badala ya kukalia mila na desturi ambazo hazina mashiko.
“Unajua unaweza ukawa umesoma lakini huna uwezo wa
kukabiliana na mazingira lakini ukiwa mbunifu haijalishi utakabiliana na
mazingira kama ambavyo Mzee Massawe ameiona fursa hiyo, mazoea kitu kibaya
sana,” anasema Glory.
Mzee Leonard Massawe alizaliwa Mei 5, 1956 katika kijiji cha
Kifuni, tarafa ya Kibosho Magharibi, Wilayani Moshi. Alifunga ndoa katika
Kanisa la Utukufu wa Msalaba huko Umbwe akiwa na umri wa miaka 44 na
amefanikiwa kuzaa watoto watano na ana wajukuu watano.
0 Comments:
Post a Comment