Juni 19, 2010 alifariki dunia mwanamichezo wa Kimataifa raia wa Sudan Kusini Manute Bol.
Alifariki dunia kwa matatizo ya figo na maradhi ya
Steve-Johnson huko Virginia nchini Marekani akiwa na umri wa miaka 48. Mwili
wake uliwekwa katika sanduku lenye urefu wa futi nane na alizikwa Sudan Kusini.
Bol alizaliwa Oktoba 16, 1962 na alikuwa akifahamika sana
kutokana na kimo chake pia harakati zake kisiasa na mchezaji wa kikapu katika
Ligi Kuu nchini Marekani (NBA).
Katika historia ya mchezo wa kikapu nchini Marekani Manute ni
miongoni mwa walioko kwenye orodha ya wachezaji warefu zaidi akifikisha futi 7
na inchi 7 sawa na mita mbili 2 na sentimeta 31.
Hadi sasa Manute Bol anashika nafasi ya tano ya kuwa mchezaji
wa kikapu duniani kwa kuwa mrefu akizidiwa na raia wa Libya Suleiman Ali
Nashnush (1943-1991) huyu alikuwa na mita 2.45, raia wa China Sun Mingming ana
mita 2.36; raia wa Uingereza Neil Fingleton (1980-2017) aliyekuwa na mita 2.33
na Paul Sturgess ambaye ana kimo cha mita 2.32
Manute alizaliwa kwa wazazi Madute na Okwok Bol huko Turalei
o Grogrial ambayo sasa ni Sudan Kusini na kukulia huko. Baba yake alikuwa wa
kabila la Wadinka na kiongozi wa jamii hiyo.
Baba yake alimpa jina hilo la Manute likiwa na maana ya
‘Baraka ya Pekee’. Hata hivyo kama ilivyo katika baadhi ya jamii za kiafrika
tarehe rasmi ya kuzaliwa kwake haikuwahi kuwa wazi lakini ilikadiriwa tu.
Manute Bol alitokea katika familia ya watu warefu kwani mama
yake alikuwa futi 6 na inchi 10 sawa na mita 2.08 huku baba yake akiwa na futi
6 na inchi 8 sawa na mita 2.03, dada yake alikuwa na futi 6 na inchi 8 sawa na
mita 2.03.
Manute Bol aliwahi kusema kuwa babu yake alikuwa na kimo cha
futi 7 na inchi 10 sawa na mita 2.39 Kwa asili Wadinka kutoka jamii ya
Wanilotes ni watu warefu sana hapa ulimwenguni.
Alianza kucheza mchezo wa soka mwaka 1972 lakini aliachana
nao kwasababu ya kuwa mrefu sana . Ndipo katika ukuaji wake akakimbilia katika
mchezo wa kikapu akiwa na timu mbalimbali ikiwamo Wau na Khartoum zote za
Sudan.
Akiwa katika masomo yake ya Chuo Kikuu nchini Marekani huko
Bridgeport alichaguliwa na Washington Bullets katika NBA Draft ya mwaka 1985.
Katika medani ya kikapu alicheza miaka 10 hadi mwaka 1995 huko nchini Marekani.
Manute Bol ndiye mchezaji pekee aliyeweka rekodi ya kuzuia
kupiga matawi kuliko pointi alizofunga akiwa na wastani wa kupiga matawi 15
katika mchezo mmoja. Pia amewahi kuzitumikia Golden State Warriors,
Philadelphia 76ers, Miami Heat na Florida Beach Dogs.
0 Comments:
Post a Comment