Tuesday, June 9, 2020

Waandishi Kilimanjaro wapokea vifaa kujikinga na Covid-19

Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Kilimanjaro  (MECKI) imepokea vifaa vya kujikinga na maambukizi ya corona kwa ajili ya waandishi wa habari mkoani humo kutoka Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kuwakabidhi walengwa wa vifaa hivyo.

Akizungumza na Tanzania Daima baada ya kukabidhi msaada wa vifaa hivyo Mwenyekiti wa MECKI Bahati Nyakiraria alisema vifaa hivyo ni mojawapo ya juhudi za UTPC katika kuwalinda wanahabari wakiwa katika majukumu yao kwani nao ni binadamu kama wengine.

Nyakiraria alisema vifaa vilivyoletwa ni pamoja na barakoa 350, vitakasa mikono 200 na glavu zaidi ya 200 na wamevikabidhi kwa waandishi wa habari mkoani humo waliohudhuria hafla hiyo ya hivi karibuni katika ofisi ya wanahabari hao mjini Moshi.

“Sisi waandishi wa habari ni binadamu ambao tuna haki ya kulindwa na kuchukua tahadhari inapobidi, sasa UTPC waliliona hilo kwa kutoa msaada huu utakuwa unatimiza azma na malengo ya umoja huo wa kuwaangalia wanachama wake ikiwa na maana ya vilabu vya waandishi wa habari nchini,”

Aidha mwenyikiti huyo aliwataka waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini kuvitumia wakati wanapokuwa katika majukumu yao ya habari kwani wanakutana na watu wengi ambao hawajui afya zao.

Kwa upande wake mwandishi wa habari Lucy Ulomi alishukuru kupokea vifaa hivyo na kusema kupewa vifaa hivyo kunaonyesha wazi kuwa changamoto hii ambayo imeikumba dunia kwa sasa bado ipo na sio jambo la kupuuzia hata kidogo.

Mkoa wa Kilimanjaro una wanahabari wapatao 80 huku walio hai katika klabu ya waandishi wa habari mkoani humo ni 26.






0 Comments:

Post a Comment