Matatizo ya akili yanahangaisha maelfu ya mamilioni ya watu
katika kila sehemu ya dunia na yana matokeo mabaya juu ya maisha ya watu. Hofu
moyoni ni miongoni mwa vichocheo vikubwa vinayoleta matatizo hayo duniani pote.
Tumesikia kuhusu tukio la Mmarekani mweusi George Floyd
alivyotendewa na Polisi ya Minneapolis, Marekani. Floyd (46) ambaye alikuwa
mfanyakazi wa mgahawa mmoja nchini humo aliuawa na Afisa wa Polisi baada ya
kukamatwa na kukandamizwa ardhini na askari katika eneo la shingo hali
iliyomfanya apoteze fahamu hatimaye kufariki dunia baada ya kufikishwa
hospitali.
Kifo cha askari huyo kinazidisha mkururu wa matukio ya
Wamarekani Weusi katika taifa hilo kuuawa na Maafisa wa Polisi.
Umoja wa Mataifa (UN) kupitia kwa Mkurugenzi wa Masuala ya
Haki Michelle Bachelet umezitaka mamlaka nchini humo kuchukua hatua stahiki na
kuzuia mauaji ya Wamarekani Weusi wasio na silaha.
Taarifa kutoka nchini humo zinasema maofisa waliofanya
unyama huo Jumatatu ya Mei 25, 2020 wamefukuzwa kazi.
Shirika la Ujasusi la Marekani FBI limeanzisha uchunguzi
kuhusu tukio hilo. Mwanasheria mkuu wa Minnesota Erica MacDonald katika taarifa
yake ya pamoja na ile ya FBI iliyotolewa na Rainer Drolshagen imesema uchunguzi
wa tukio hilo umepewa kipaumbele.
Mkuu wa Jeshi la Polisi la Minneapolis Medaria Arradondo
aliomba radhi kwa ndugu, jamaa na marafiki baada ya kifo cha Floyd.
Hakika juma la mwisho la mwezi Mei 2020 lilikuwa juma la
machungu na giza kwa watu wenye ngozi nyeusi na wanaharakati bila kujali rangi
zao duniani kote kwani tukio hilo limezusha hasira.
Binafsi nimeona ni vema tukazama kwa kina kuliangalia suala
hili la Askari Polisi Weupe wa Marekani sababu zipi zimekuwa zikiwafanya kutenda
unyama huo kwa watu wenye ngozi nyeusi? Je ni matatizo ya akili ya askari hao
au ni makosa ya weusi wenyewe?
Jarida la Lancet la nchini Marekani Julai 28, 2018
lilichapisha utafiti wake kuwa Polisi nchini Marekani huwaua Wamarekani Weusi
zaidi ya 300 kila mwaka nchini humo. Hatua hiyo imekuwa ikizidisha hali ya
wasiwasi kwa Wamarekani Weusi hivyo mdodoro wa afya ya akili huwapata
waathirika wa visa hivyo hata kama sio moja kwa moja.
Katika chapisho hilo Jarida la Lancet lilitaka hatua za
haraka zichukuliwe kunusuru afya ya akili ya Wamarekani Weusi nchini humo.
Mnamo mwaka 2014 aliuawa Mmarekani mweusi Michael Brown
katika kitongoji cha St. Louis huko Ferguson, Missouri na kuanza kwa kile
kinachofahamika sasa kama BLM yaani ‘Black Lives Matter’. Maandamano hayo
yamekuwa maarufu.
Gazeti la Washington Post tangu Januari 1, 2015 hadi sasa
limefuatilia na kuchapisha visa vya mauaji zaidi ya 5,000 yanayofanywa na
Maafisa wa Polisi wakiwa kazini.
Aidha gazeti hilo linasema kuwa vifo hivyo vimekuwa kitisho
kikubwa kutokana na asilimia 13 ya watu nchini Marekani ni Wamarekani Weusi
wanaofikia milioni 42. Pia Washington Post linasema Watu wenye asili ya
Kihispaniola (Latinos) wanaofikia milioni 39 nao pia wamekuwa wakiuawa na
Maafisa wa Polisi. Idadi ya mauaji hayo imepindukia na kuzidi Wamarekani weupe wanaofikia milioni
149 nchini humo.
Washington Post linasema Wamarekani weusi 30 katika kila
milioni moja wamekuwa wakiuawa, Latinos 22 kila milioni moja, Wamarekani weupe
12 katika kila milioni moja na watu wengi wanne kila milioni moja wamekuwa
wakiuawa na maafisa wa polisi.
Mwaka 2015 waliuawa watu 994, mwaka 2016 waliuawa 962, mwaka 2017 waliuawa 986, mwaka 2018 waliuawa
992, mwaka 2019 waliuawa 1,110 na mwaka huu hadi sasa wameuawa watu 400. Kwa
takwimu hizo hali hiyo imekuwa ikizidisha uhasama baina ya polisi wa kizungu na
Wamarekani weusi pindi wanapokutana uso kwa uso.
Maeneo yanayoongoza kwa mauaji hayo nchini Marekani ni New
Mexico, Alaska na Oklahoma. Taifa hilo tangu miaka ya 1900 limekuwa likionyesha
unyama mkubwa kwa Wamarekani weusi hata kama hawana silaha kuliko kwa
Wamarekani weupe.
Chanzo kimoja cha masuala ya sheria nchini Marekani kinasema
Mmarekani mweusi mmoja kati ya 1,000 anatarajia kupoteza maisha akiwa mikononi
mwa polisi, wastani ambao ni mara 2.5 kuliko Mmarekani mweupe atakaposhikwa na
Maafisa wa Polisi.
Pia utafiti nchini humo uliofanywa na Mwanasayansi ya Jamii
Frank Edwards wa Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani umebaini kuwa
Wamarekani weusi, Walatino wake kwa waume na watoto wamekuwa wakiuawa na
maafisa wa Polisi kwa kiwango kikubwa kuliko wanavyofanyiwa weupe. Utafiti huo
umetaja visa kadhaa vya polisi kati ya mwaka 2013-2018 miongoni ni Eric Garner,
Tamir Rice and Freddie Gray.
Wanasayansi wanaendelea kuliangazia suala hilo kuwa sasa
limekuwa tatizo la Kiafya zaidi katika jamii kuliko inavyodhaniwa. Pia sababu
za mauaji hayo zinatajwa kuwa zinatokana na Wamarekani weusi kujihusisha kwa
kiasi kikubwa na dawa za kulevya na matumizi ya silaha hivyo askari hao huona
ni vema wakachukua jukumu moja tu la kuwamaliza.
Mnamo mwaka 2004 Taasisi ya Vera nchini Marekani ambayo
imekuwa ikishughulisha na masuala ya Sheria ilibaini kuwa mtazamo wa Wamarekani
weusi dhidi ya Polisi umetokana na
uzoefu walionao na pia uzoefu wa marafiki na familia zilizotendewa unyama huo
hivyo hofu ndio huzidisha vitendo hivyo.
Aidha taasisi ya Cato/YouGov Survey mnamo mwaka 2016
ilibaini kuwa Wamarekani weusi wamekamatwa zaidi na kupewa kichapo na Maafisa
wa Polisi kuliko Wamarekani weupe. Mara tano zaidi Mmarekani mweusi anatarajia
kupewa mateso na Maafisa wa Polisi kutokana na ngozi yao.
Utafiti huo ulibaini pia Mmarekani mweusi amekuwa na
wasiwasi zaidi wa vurugu dhidi ya Polisi kuliko kufanya kosa la vurugu.
Historia ya maeneo husika kama Baltimore, Ferguson, Cleveland, Chicago,
Milwaukee na sasa Minneapolis yamekuwa na vurugu kupitiliza zinazotokana na
Maafisa wa Polisi hali ambayo imekuwa ikitia hofu zaidi kutokana na kuwatazama
Freddie Gray au Laquan McDonald au Tamir Rice waliotendewa unyama na polisi.
Utafiti uliofanywa na NPR/Robert Wood Johnson Foundation
mnamo mwaka 2017 ulibaini kuwa nusu ya Wamarekani weusi wanaposimamishwa na
Polisi wamekuwa wakisimamishwa kwa ukali wa hali ya juu. Watu sita kati ya kumi
wameonyesha hilo na hivyo kuona kuwa hawatendewi inavyopaswa. Utafiti huo
umekielezea kisa kimoja cha Philando Castile aliuawa na Afisa wa Polisi licha
ya kutii wito wa polisi hao.
Historia ya miaka mingi ya nyuma inaonyesha namna ambavyo
Wamarekani hao weupe wanavyoshindwa kujiamini
kwani katika karne ya 19 na 20 Wamarekani weupe waliendelea kuwanyanyasa
hata wahamiaji wa Kiyahudi na Kiitaliano katika maeneo mbalimbali ikiwamo New
York na Chicago na polisi walitumika kufanya hivyo.
Pia kundi kubwa la Wamarekani weusi miaka ile ya 1916 -1970
lililokuwa likitokea maeneo ya kusini ambayo yalikuwa ya vijijini kwenda
Kaskazini na Magharibi ambako kulikuwa mjini kuliongeza hofu ya Wamarekani
weupe ikiwamo vitengo vya polisi hivyo uadui ukaanza.
Kuanzia miaka 1970 hadi 1980 kulijitokeza makosa ya jinai
mengi maeneo ya mijini ambayo yalisababishwa na Wamarekani weusi hali
iliyowafanya Polisi kuamini kwamba watenda makosa siku zote nchini humo ni
Wamarekani weusi hivyo akipatikana mahali popote pale ni kuchapa risasi tu…..
Sababu kubwa kuliko zote ilikuwa ni ile ya ongezeko la
Wamarekani weusi hususan upande wa kaskazini, idadi yao iliongezeka kwa kasi na
wakawa wameanza kukaa hata maeneo waliyokuwa wakikaa Wamarekani weupe na
ongezeko hilo liliwatishia hata Maafisa wa Polisi hivyo sheria zikaanza
kutungwa kwa ajili ya kuwadhibiti Wamarekani weusi ikiwamo kutotumia baadhi ya
maeneo ya hadhira.
Binafsi nafikiri matatizo ya akili ndani ya askari wa polisi
weupe nchini Marekani ambayo yamedumu kwa muda mrefu ndio sababu ya mauaji hayo
kwani idadi kubwa ya Wamarekani weusi waliouawa na polisi hao bila kukimbia ni
kubwa kuliko ya waliokuwa wakiwakimbia, Gazeti la Washington Post limechapisha
visa vya mauaji 3,356 watu hao walitii amri ya polisi na watu 684 waliuawa
wakati wakikimbia kwa mguu; sasa unafikiri lipi bora wakimuona askari huyo.
Kupitia matunzo mazuri ya akili kwa askari hao, mauaji ya
watu weusi na wengine yanaweza kuisha na watu wakaishi maisha yenye faida na
yenye furaha.
0 Comments:
Post a Comment