Juni 23, 79 alifariki dunia mtawala wa Kirumi
aliyefahamika kwa jina la Vespasian. Mtawala huyu alikalia kiti cha kuwa
Kaisari wa Rumi kutoka mwaka 69 hadi kifo chake.
Alifariki dunia kwa ugonjwa wa kuharisha
(kipindupindu). Katika mwaka wake wa tisa alipata homa akiwa Campania hivyo
ikambidi arudi Rome.
Hakukaa sana, alianza safari ya kwenda Aquae Cutiliae
karibu na Rieti ambako alikuwa akizuru wakati wa majira ya joto kila mwaka. Akiwa
huko ndiko hali yake kiafya ikazorota zaidi ambayo iliambatana na maradhi ya
kuharisha.
Waliokuwa karibu naye walikaririwa na mwanahistoria Gaius
Suetonius Tranquillus maarufu Suetonius kuwa wakati akiwa kitandani alihisi
kuwa mauti inamkabili ikabidi asema maneno haya, “Vae, puto deus fio.” Akiwa na
maana kwamba anakaribia kuwa mungu.
Siku ya kifo chake alikuwa akishusha mguu wake kutoka
kitandani lakini alishindwa na waliokuwa karibu naye kwa ajili ya kumpa msaada
wakajitahidi kumshusha kitandani lakini akafia mikononi mwao.
Suetonius ambaye alikuwa mwandishi wa historia nyakati
za mwanzo kabisa kuhusu masuala ya ufalme wa Rumi katika kitabu chake cha ‘The
Twelve Caesars’ aliandika kwamba Vespasian alifariki dunia akiwa na umri wa
miaka 69 miezi 7 na siku 7.
Vespasian anakumbukwa kutokana na tabia yake ya
kupendeza iliyoendana na uwezo wake wa kufanya maamuzi na nguvu za kijeshi.
Pia Vespasian ni mwanzilishi wa ujenzi wa Flavian
Amphitheatre maarufu kama Colosseum ambao ulikuja kumaliziwa na mtoto wake
Titus.
Titus aliingia madarakani mnamo mwaka 79 na kufariki
dunia mwaka 81. Awali alikuwa kiongozi wa kijeshi katika eneo la Yuda wakati wa
vita baina ya Wayahudi na Warumi.
Kati ya mwaka 71 na 79 wanahistoria mbalimbali
wanasema mtawala huyu aliamuru ujenzi wa majengo mengi katika dola la Rumi
ikiwamo Colosseum.
Vespasian alipambana kutanua dola la Rumi hadi
Uingereza ambapo mwaka 78 alimtuma Agricola katika ardhi hiyo kufanya utafiti
ambapo alirudi na ushahidi wa Kiakiolojia kuhusu Uingereza.
Vespasian aliingia kushika dola la Rumi baada ya
machafuko ndani ya ufalme. Ndani ya kipindi kifupi walitawala Makaisari wanne.
Makaisari hao wanne walitawala baada ya kifo cha
Kaisari Nero aliyeshika madaraka kutoka mwaka 54 hadi kifo chake. Vita vya
wenyewe kwa wenyewe vilimleta kwenye kiti hicho Lucius Livius Galba Ocella maarufu
Galba. Hata hivyo alikalia kiti hicho kwa miezi saba kutoka Juni 8 hadi Januari
15, mwaka 69.
Galba aliuawa na wafuasi wa Marcus Otho Caesar
Augustus maarufu Otho, ambaye alikalia kiti hicho kwa miezi mitatu hadi Aprili
16, mwaka 69.
Otho alizidiwa nguvu na Aulus Vitellius Germanicus maarufu
Vitellius ambaye alikalia kiti hicho kwa miezi minane hadi Desemba 22, mwaka
69.
0 Comments:
Post a Comment