Nchini Tanzania masuala ya ndoa yanaendeshwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Sheria zinazosimamia masuala ya ndoa ni Sheria ya Ndoa, Sura ya 29 ya Sheria za Tanzania.
Kifungu cha 9(1) kinabainisha kuwa muungano huo ni lazima uwe wa kudumu. Pia kifungu cha 12 kinazungumzia kuwa ndoa ni ya kudumu labda tu kama kuna kifo au talaka. Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria hii, ndoa za mkataba wa muda fulani hazikubaliki.
Muungano huo ni lazima uwe kati ya watu wa jinsi tofauti, yaani kati ya mwanamke na mwanaume kama kifungu cha 9(1) kinavyosema. Pia maharimu hawaruhusiwi kuoana yaani wenye undugu wa karibu.
Kifungu cha 15 kinaeleza kwamba kama mmoja wa wafunga ndoa ana ndoa ya mke mmoja basi hawezi kufunga ndoa nyingine. Hali kadhalika mtu aliye na ndoa ya wake wengi hawezi kufunga ndoa ya mke mmoja. Pia kama mwanamke ana ndoa inayoendelea hawezi kuolewa tena na mwanaume mwingine. Kwa mujibu wa kifungu cha 9(2) na (3) kuna aina mbili tu za ndoa zinazotambulika, nazo ni ndoa ya mke mmoja na ndoa ya wake wengi.
Kuna aina tatu za ufungishaji ndoa ambazo ni kidini, kiserikali na kimila kama ambavyo kifungu cha 25 (1) kinavyoeleza. Ufungishaji wa Ndoa za Kidini, Ufungishaji Ndoa Kiserikali na Ufungishaji Ndoa Kimila. Sheria ya ndoa katika kifungu cha 160 inaeleza juu ya mahusiano haya kwamba endapo mwanamke akiishi na mwanaume kwa miaka miwili au zaidi mfululizo na jamii inayowazunguka ikawatambua na kuwapa hadhi ya mume na mke, basi mahusiano hayo yaweza kupata dhana ya kuchukuliwa kama wanandoa.
Ili kuwe na dhana ya ndoa pia ni lazima sifa za watu wanaotaka kufunga ndoa kama zilivyoelezwa hapo juu ziwe zimefuatwa. Kwa mfano, hakuna dhana ya ndoa endapo mmojawapo hajafikia umri wa kufunga ndoa.
NDOA BATILIFU: Kwa mujibu wa kifungu
cha 39 ndoa batilifu ni ndoa halali kisheria lakini kwa sababu fulani fulani
mara tu baada ya kufunga ndoa inaonekana wafunga ndoa hao hawawezi kuendelea
kwenye ndoa hiyo. Mambo yafuatayo yanaweza kuifanya ndoa kuwa batilifu:
● Kutoweza kufanya tendo la ndoa.
● Mmoja wa wanandoa kudhihirika kuwa na kichaa au kifafa.
● Mmoja wa wanandoa kudhihirika kuwa alikuwa ana magonjwa ya
zinaa.
● Mke kudhihirika kuwa alikuwa na mimba ya mwanaume mwingine.
● Mwanandoa mmoja kukataa kwa makusudi kufanya tendo la ndoa
tangu ndoa kufungwa.
Ndoa batilifu ni ndoa halali na itaendelea kuwa hivyo hadi
hapo mahakama itakapoitengua.
MATUNZO: Matunzo Kifungu cha 63 kinatamka kwamba mume ana
wajibu wa kumtunza mkewe kwa kumpa mahitaji yote muhimu katika maisha kama
mavazi, chakula na malazi kulingana na uwezo wake. Mke pia atakuwa na wajibu huo
ikiwa tu mume kwa sababu ya ugonjwa hawezi tena kufanya kazi yoyote. Na kama
mume hatekelezi wajibu huo kwa makusudi mahakama chini ya kifungu cha 115
yaweza kumwamuru kutekeleza wajibu huo.
KUTENGANA: Kutengana na talaka ni haki alizonazo kila
mwanandoa endapo ndoa yao itakuwa na matatizo kiasi kwamba itaonekana wazi kuwa
wawili hawa hawawezi tena kuendelea kuishi pamoja. Kutengana ni ile hali ya
wanandoa kuacha kuishi pamoja, yaani kuacha kuishi chini ya dari moja.
Kutengana kupo kwa aina mbili, kwa hiari ya wanandoa wenyewe na kwa amri ya
mahakama. Amri ya kutengana kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 111 inawafanya
wanandoa wasikae tu pamoja lakini haiondoi wajibu na majukumu aliyo nayo
mwanandoa kuhusiana na matunzo.
TALAKA: Talaka ni amri ya mahakama ya kuvunja ndoa. Chombo
pekee chenye uwezo wa kuvunja ndoa ni mahakama tu. Mazoea ya wanandoa kupeana
talaka mitaani aidha kwa maandishi au kwa mdomo, hizo si talaka kwa mujibu wa
sheria ya ndoa. Ni lazima talaka itolewe na mahakama ili haki ya kila mwanandoa
itamkwe bayana. Kwa mujibu wa kifungu cha 100 mahakama haiwezi kusikiliza shauri
la talaka kama ndoa haijadumu kwa miaka miwili. Ili shauri la talaka lipokelewe
kabla ya miaka miwili ya ndoa kupita ni lazima mahakama itoe idhini. Idhini
hiyo hutolewa pale tu ambapo mwanandoa mmoja anapata mateso yasiyokuwa ya
kawaida.
SABABU ZA KUTOA TALAKA: Vifungu vya 99 na 107(1) vya sheria
ya ndoa vinatamka kwamba sababu inayoweza kuifanya mahakama kutoa talaka ni
pale tu itakaporidhika kuwa ndoa imevunjika kiasi ambacho haiwezi kurekebishika
tena. Sababu zinazofanya ndoa ionekane kuwa haiwezi kurekebishika tena ni:
● Ugoni na hasa kama tabia hiyo imeendelea hata baada ya
mwanandoa mwingine kupinga tabia hiyo.
Ukatili wa kiakili au wa kimwili ambao anatendewa mwanandoa
mmoja au hata kama watoto ndio
wanaofanyiwa ukatili huo.
● Ulawiti
● Kuzembea wajibu kwa makusudi
● Utoro au kutelekeza kwa makusudi kwa muda wa miaka
isiyopungua mitatu.
● Kifungo cha maisha au kisichopungua miaka mitano.
● Kutengana kwa hiari au kwa amri ya mahakama kulikodumu kwa
miaka mitatu au zaidi.
● Kubadili dini.
● Kichaa kisichopona ambapo madaktari bingwa wasiopungua wawili
wamethibitisha kwamba hakuna matumaini ya huyo mtu kupona.
Alama ya muhimu katika makala haya ni kwamba Mahakama pekee ndiyo yenye wajibu wa kutoa talaka na sio vinginevyo.
0 Comments:
Post a Comment