Tuesday, June 2, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Santiago Bernabéu de Yeste ni nani?


Juni 2, 1978 alifariki dunia mwanasoka wa Kimataifa wa Hispania na mbeba maono ya ujenzi wa Uwanja mpya wa klabu ya Real Madrid Santiago Bernabeu. 

Nyota huyo alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu wa timu ya taifa ya Hispania na klabu ya Real Madrid aliyekuwa anacheza katika nafasi ya mshambuliaji. 

Bernabeu ndiye mchezaji muhimu kuliko wote katika historia ya klabu ya Real Madrid kwani alisaidia Madrid kuingia miongoni mwa klabu zenye mafanikio Hispania na Ulaya. Mpaka sasa uwanja unaotumiwa na Real Madrid wanauita kwa jina lake. Alikuwa rais wa klabu ya Real Madrid kwa miaka 35 kuanzia mwaka 1943 mpaka 1978. 

Mwaka 1978 Bernabeu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82. Jina lake halisi ni Santiago Bernabeu de Yeste. Alizaliwa huko Almansa, Albacete nchini Hispania Juni 8, 1895. 

Familia yake iliondoka huko Almansa na kwenda Madrid akiwa na umri mdogo. Mnamo mwaka 1909 akiwa na umri wa miaka 14 Bernabeu alijiunga na timu ya vijana ya klabu ya Real Madrid baada ya kuwa mtazamaji kwa miaka mingi. Timu ya wakubwa alianza kuhudumu nayo mnamo mwaka 1911. 

Bernabeu alipotua katika miamba hiyoalipewa unahodha kwa miaka na alikuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji. Alistaafu soka mnamo mwaka 1927 na miaka miwili baadaye Ligi Kuu ya Hispania ilianza kuchezwa rasmi nchini humo.  

Alipostaafu aliendelea kujishikiza katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu hiyo hadi mwaka 1935, alishika wadhifa wa kuwa mkurugenzi, kocha msaidizi na baaaye alikuwa kocha mkuu wa miamba hiyo. Mnamo mwaka 1943 alishika wadhifa wa Rais wa klabu hiyo hadi kufariki kwake mwaka 1978. Alishika wadhifa huo kwa muda wa miaka 35. 

Mnamo mwaka 1936 kuliibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania ambavyo vilidumu kwa takribani miaka mitatu hadi mwaka 1939. 

Hivyo basi kwa kutokea tafrani hilo kandanda lilisimama kwa muda na Bernabeu alipata fursa ya kulitumikia jeshi akiwa upande wa Wazalendo wa taifa hilo chini ya Jenerali Agustin Muñoz Grandes. Baada ya kumalizika kwa vita hivyo alirudi katika klabu ya Real Madrid ambako hali ilikuwa mbaya kupitiliza hata maono ya miamba hiyoo yalipotea. 

Bernabeu alibeba maono kwani viongozi walioongoza awali walio wengi walipoteza maisha wakati wa vita hivyo na baadhi ya mataji yaliibiwa. Wakati anarudi kilichokuwa kikionekana ni uanzishwaji wa klabu mpya Atletico Madrid (ambayo ilikuwa ikiitwa Atlético Aviación, Timu ya Kikosi cha Anga). 

Los Blancos hawakupata msaada wowote ule kutoka serikali kwa ajili ya ujenzi wa klabu hiyo. Bernabeu aliendelea kwa miezi kadhaa mbeleni kuwatafuta wachezaji wa zamani, wakurugenzi na wanachama wa klabu kwa ajili ya jambo moja tu la kuifufua klabu hiyo. 

Mnamo mwaka 1943 kulitokea vurugu baada ya Real Madrid kuitandika FC Barcelona ambapo kuliifanya serikali itumie hekima kutafuta suluhisho la ambapo serikali iliwataka marais wa timu zote mbili kujiuzulu na ndipo Bernabeu alichaguliwa kuwa Rais wa Real Madrid. 

0 Comments:

Post a Comment