Friday, June 12, 2020

Unaifahamu Historia ya ukatili wa Polisi nchini Marekani dhidi ya Wamarekani weusi

Vitendo vya Maafisa wa Polisi nchini Marekani kuwatesa raia wake ni vitendo ambavyo vimetafsiriwa kuwa ni matukio ya mateso ambayo yanakiuka sheria dhidi ya raia. Mateso hayo yamekuwa yakihusisha utumiaji wa nguvu, vipigo vinavyosababisha mateso na wakati mwingine mauaji ya raia hao. Pia tafsiri nyingine imesema vitendo hivyo vimekuwa vikihusisha maneno yenye ukali na dharau na njia nyingine zisizo za kiuungwana.

Nchini Marekani polisi hawa wamekuwa wakiwatesa raia wa rangi zote, makabila yote, watu wa umri wote (watoto, vijana na watu wenye umri mkubwa), jinsi zote na madaraja yote ya kimaisha.

Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, Wamarekani weupe maskini na wale wafanyakazi  walionyesha hasira zao dhidi ya sera za kibaguzi kwa miji ya kaskazini mwa taifa hilo.

Wakati huo huo, Wayahudi na wahamiaji wengine kutoka kusini na Mashariki mwa Ulaya walipaza sauti zao kuhusu unyanyasaji uliokuwa ukifanywa na polisi katika jamii zao. Mnamo mwaka 1920 hususani idara za polisi wa maeneo ya mijini kama vile New York na Chicago walitumia mbinu zaidi za kisheria dhidi ya wahamiaji wa Kiitaliano ili kudhibiti kabisa wizi, udanganyifu, ukabaji na utekaji.

Mnamo mwaka 1943  Maafisa wa Idara ya Polisi huko Los Angeles walikuwa wamejiingiza katika mashambulio ya Wamarekani wenye asili ya Mexico wakati wa Fujo za Zoot Suit. Kuanzia hapo ndipo chanzo kikubwa cha uadui dhidi ya WaLatino hao. Mateso dhidi ya mashoga na wasagaji yaliyokuwa yakifanywa na polisi jijini New York mnamo mwaka 1969 yaliamsha maandamano na harakati za Haki za Mashoga.

Mnamo mwaka 2001 katika shambulio la Septemba 11, waislamu wazaliwa wa Marekani walijikuta katika wakati mgumu kutoka kwa polisi, hali iliyoamsha tena sauti za kulalamikia unyanyasaji ukiambatana na ubaguzi wa rangi.

Ilianzishwa operesheni  ya kuwasaka magaidi wa tukio hilo hadi misikitini kwa zaidi ya muongo mmoja. Licha ya unyanyasaji huo Wamarekani weusi walilengwa zaidi. Makadirio ya wataalamu walio wengi wanasema uwepo wa Wamarekani weusi katika idara za Polisi kungefanya Polisi Weupe wakose nafasi.

Licha ya unyanyasaji huo kufanywa na polisi wa taifa hilo kwa raia wake lakini Wamarekani weusi limekuwa ni kundi ambalo linatolewa macho na udenda na polisi hao. Wataalamu mbalimbali wanakadiria kuwa katika idara za Polisi weupe kumekuwa na unyanyasaji mkubwa dhidi ya weusi.

Ubaguzi wa rangi imekuwa ndio sababu kubwa ya polisi kutenda vitendo hivyo na kwa makundi mengi katika jamii ya Wamarekani. Lakini kusema kwamba ubaguzi wa rangi pekee ndio sababu haitoshi zipo sababu nyingine ambazo zimekuwa chanzo cha unyanyasaji unaofanywa na Polisi.

Inaelezwa kuwa kwa polisi walioko maeneo ya mijini hususani wale ambao ni chipukizi, kukubalika kwao na kupanda katika vyeo kunategemea namna watakavyochukua mitazamo, maadili na matendo ya kundi lenyewe ambalo kihistoria limekuwa likipambana kuondoa ubaguzi huo wa rangi. Hivyo basi katika makala haya yatajielekeza katika uzoefu, historian a hali ilivyo kwa sasa.

VUGUVUGU LA KUHAMIA MIJINI

Mahusiano baina ya Wamarekani weusi na Idara za Polisi wa Mijini lilianza wakati wa kile kinachofahamika kama Great Migration au vuguvugu la kuhamia mijini ambalo nchini Marekani lilifanyika kati ya mwaka 1916 hadi 1970.

Kipindi hiki Wamarekani weusi walitoka maeneo ya vijijini upande wa Kusini mwa taifa hilo na kwenda katika maeneo ya Kaskazini na Magharibi ambako kulikuwa ni mijini.

Hali hiyo ilichangiwa zaidi hasa kutokana na Vita vya Pili vya Dunia (1939-1945). Jamii nyingi za Wamarekani weupe ikiwamo idara za Polisi walijikuta wakigutuka kuona uwepo wa Wamarekani weupe  hali ambalo ilizidisha hofu na uhasama, mitazamo ilijengeka katika muundo wa ubaguzi wa rangi.

Imani ya weupe hususani Idara za Polisi za upande wa Kaskazini kuhusu Wamarekani weusi ni kwamba ni watu ambao wamerithi chembechembe za vurugu na tabia ya kutenda maovu hivyo kuzuia hali hiyo ilikuwa ni lazima waanze kuwaundia sheria na kanuni ambazo ziliwabana kwa usalama wa Wamarekani weupe.

Katikati ya miaka ya 1950 idara za polisi za mijini ziliandaa mpango ambao uliwaingiza Wamarekani weusi katika idara hizo kwa madhumuni ya kuwalinda weupe dhidi ya weusi. Unyanayasaji mkubwa ulijitokeza kipindi hicho vipigo na matumizi makubwa ya nguvu havikuweza kuzuilika kwa ajili ya kudhibiti kundi kubwa la Wamarekani weusi. Polisi  hao waliendelea kuwakamata weusi hao bila hata kuwa na kosa, kauli za dharau na vitisho, unyanyasaji wa kijinsia wa wanawake wenye asili ya Afrika, mauaji ya raia yaliyofanywa na polisi hao.

Polisi hao waliendelea kujipenyeza kwa Wamarekani weusi wakiwahusisha na ufanyaji wa biashara haramu ya dawa za kulevya, silaha, ukahaba, uzururaji. Japokuwa  unyanyasaji wa Wamarekani weusi uliokuwa ukifanywa na Polisi ulikuwa ni changamoto kubwa katika maeneo ya mijini hadi katikati ya karne ya 20 lakini Wamarekani weupe wengi hawakujua hali hiyo hadi miaka ile ya 1960.

Hiyo ilitokana na kwamba magazeti, majarida na vyombo vya habari vingi nchini humo vilivyokuwa vikimilikiwa na wazungu hao havikuona kama ni habari muhimu.

Isipokuwa mapema katika karne ya 20 vyombo vya habari vya weusi ndio vilivyokuwa mstari wa mbele kukusanya na kuchapisha kuhusu unyanyasaji huo wa polisi dhidi ya Wamrekani weusi. Inaelezwa kuwa mara kadhaa ilikuwa ndio habari kuu kama ni magazeti au majarida basi itakaa ukurasa wa mbele. Pia ushahidi wa ndani na mashirika mbalimbali ya haki za raia nchini humo yalikusanya maelfu ya nyaraka na baraua kutoka kwa Wamarekani weusi ambao walieleza uzoefu wa moja kwa moja kutokana na unyanyasaji huo wa Polisi.

UKATILI WA POLISI BAADA WWII

Kutokana na sababu mbalimbali matukio ya unyanyasaji Polisi dhidi ya Wamarekani weusi yalionekana dhahiri na kuzidi katika taifa hilo katika miongo baada kumalizika kwa vita vya Pili vya Dunia mnamo mwaka 1945.

Mosi, ushindi uliopatikana kutokana na demoktrasia katika vita hivyo uliwafanya Wamarekani weusi walitarajia kwamba watakuwa na uhuru na demokrasia watakaporudi nyumbani ambapo wengi wao walikuwa katika vikosi vya jeshi la Marekani. Kama Wamarekani weusi wakaanza kutengeneza namna nzuri ya haki na uhuru wakitaka serikali na vyombo vyake vikiwamo vya kisheria kuwaangalia namna polisi weupe wanavyofanya.

Pili, vuguvugu la Wamarekani weupe waliokuwa wakiishi katika maeneo ya vijijini kwenda kwenye miji ya karibu kwa ajili ya kujitafutia nafasi nzuri zaidi za kiuchumi ziliwahamasisha polisi kuwakinga weupe hao dhidi ya weusi kwa kuongeza unyanyasaji. Polisi walianza kuwaua weusi kwa kuwanyonga bila hatua zozote za kisheria ikiwa ni sehemu ya kuwakandamiza. Wakati polisi wakifanya haya ndipo kundi Ku Klux Klan (KKK) lilipoibuka na kuanza kufanya kazi likilenga zaidi Wamarekani weusi. Lilikuwa likifanaya kazi azke upande wa miji ya Kusini mwa taifa hili ambako unyanyasaji wa polis dhidi ya weusi ilikuwa sio kitu cha kushangaza kwani serikali na viongozi wa siasa, wanasheria wa wilaya na majaji walihamasisha polisi kufanya ukatili huo.

Tatu hususani katika miji mingine ya kaskazini, ongezeko la watu weusi liliwatisha mno Maofisa wa Polisi  hali iliyowafanya waweze kutunga sheria na kanuni za kuonekana katika maeno ya wazi. Vitongoji vilianza kujaa Wamarekani weusi ambao walionekana kama wao ndio wenye ardhi ile. Nne, kujiunga kwa Wamarekani weusi  katika Jeshi la Polisi mwanzoni mwa miaka 1970 kuliongeza vitendo vya unynyasaji kwa Wamarekani weusi kwani kundi lililoingia lilitaka kujionyesha kuwa ni maaskari wazuri mbele ya weupe ili liweze kukubalika ndani ya idara za polisi nchini humo.

Hatimaye sababu ya mwisho katika hili ilikuwa ni kuongezeka kwa makosa ya jinai maeno ya mijini miaka 1970 na 1980 kwa Wamarekani weusi na majirani wengine kuliwaimarisha maofisa wa polisi wa kizungu kwa ajili ya udhibiti wa weusi na mtazamo kwamba weusi ni kizazi cha vurugu na jinai ulizidi kupata nguvu miongoni mwa weupe hali ilibadili pia hata mwenendo wa sera, kanuni na sheria.

UKATILI WA POLISI NA GHASIA

Kutoka mwaka 1960, unyanyasaji wa polisi ulikuwa ndio kichocheo kikubwa cha migomo na maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Migomo na maandamano hayo yalitokea maeneo ya mijini ikiwamo yale ya Watts mwaka 1965 na Detroit ya mwaka 1967.

Mnamo mwaka 1980 kitengo cha Haki na Uhuru cha jiji la Miami kiliwageukia polisi kwa mauaji waliyoyafanya ya Mmarekani mweusi ambaye hakuwa na silaha. Kwa siku tatu, watu 18 waliuawa na wengine 1,000 walikamatwa huku mali zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 200 ziliharibiwa vibaya.

Miaka 12 baadaye maofisa wa Polisi walimtandika vibaya sana Rodney King huko Los Angeles hali ambayo ilizusha maandamano na ghasia za Los Angeles mwaka huo. Ghasia hizi za Los Angeles zinachukuliwa kuwa ndizo mbaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Marekani dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Ndani siku sita zaidi ya watu 50 waliuawa na zaidi ya 2,300 walijeruhiwa huku mali zenye thamani ya dola za Marekani bilioni moja ziliharibiwa. Mnamo mwaka 2014 kijana Mmarekani mweusi Michael Brown huko St. Louis, Ferguson alitandika risasi na kupoteza maisha na polisi weupe wa Missouri lakini ghasia zilianza pale ambapo vyombo vya sheria vikishindwa kumchukulia hatua Afisa wa Polisi aliyefanya tukio hilo.  Mwaka uliofuata ghasia ziliibuka lakini hizi zikiwa za maandamano ya amani baada ya kuuawa kwa Freddie Gray huko Baltimore, Maryland na mwaka 2020 ghasia na maandamano yalitokea baada ya kuuawa kwa George Floyd huko Minneapolisi, Minnesota.

KAMPENI ZA KUPINGA UKATILI WA POLISI

Waathirika wa vitendo hivi sio pekee Wamarekani weusi bali wapo na weupe ambao wamejikuta wakikutana na unyanyasaji huu wa Maafisa wa Polisi wa Marekani. Weupe wanaonyanyasawa na polisi hao ni wale ambao wanatoka katika madaraja ya chini yaani kiuchumi wapo chini. 

Kampeni za kupinga unyanyasaji huo zimepata uungwaji mkono na Wamarekani weusi. Mojawapo ya kampeni zinazofanywa ni kuishinikiza serikali iwaajiri Wamarekani weusi katika idara za polisi katika maeneo ya usimamizi, pia katika patrol za Maafisa weusi katika viunga wanamoishi weusi hao, kuwa na Bodi ya kiraia itakayosimamia na kupitia mambo mbalimbali ili kuweka usawa. Pia kampeni hizo zimekuwa zikitaka kuwepo na idara ya haki ambayo itajikita katika uchunguzi wa kina kuhusu visa mbalimbali ambavyo maafisa polisi.

Kampeni hizo zimekuwa zikifanywa kwa kufanya migomo, kukaa eneo bila kuondoka hadi jawabu litakapotolewa (sit-ins), migomo ya wafanyakazi ya ndani ya ofisi wanazofanyia kazi (picketing). Mnamo mwaka 2014 baada ya mauaji ya Michael Brown na Eric Garner ndio yaliyosababisha vuguvugu la Black Lives Matter (BLM).

Vuguvugu hilo limekuwa muhimu kwa Wamarekani weusi dhidi ya unyanyasaji maafisa wa Polisi. Mnamo mwaka 2016 Wamarekani weupe watano wa Dallas, Texas na Maafisa watatu wa Polisi huko Baton Rouge , Louisiana walipigwa risasi na kuuawa. Hapo awali kampeni za kuzuia ukatili zilionekana kuongozwa na wanaharakati katika ngazi ya chini ya vijiji na na washiriki wengine wa jamii zilizoathiriwa moja kwa moja badala ya mashirika ya haki za raia.

Feature Story by: Jabir Johnson

 


0 Comments:

Post a Comment