Mnamo Mei 8, 2020 ilitangazwa kuwa Freddie Blom raia wa Afrika Kusini alikuwa akiifikisha umri wa miaka 118.
Rais wa taifa hilo Cyril Ramaphosa alimtakia Happy Birthday Njema mwanaume huyo mwenye umri mkubwa anayeishi barani Afrika. Baada ya Bloom kupokea salamu kutoka kwa Ramaphosa alimwambia kuwa ingefaa zaidi apunguze bei ya sigara maana ni ghali sana. Blom alisema, "Nimeishi miaka mingi kwasababu ya neema ya Mungu."
Bloom alitangazwa na vyombo vya habari ulimwenguni kuwa ni mwanaume ambaye aliona namna maradhi ya Spanish Flu yalivyoutesa ulimwengu kama alivyoona maradhi ya Corona.
Guiness Book of World Records ilimtangaza Bloom kuwa ameipita rekodi ya Mwingereza aliyeweka rekodi ya kuishi muda mrefu akifikisha miaka 112.
Wakati hayo yakijiri nchini Tanzania hakukuwa na taarifa zozote zinazomhusu mwanamke mwenye umri mkubwa kuliko wote ulimwenguni aliyekuwa hai hadi alipofariki Mei 27, 2020 akiwa na umri wa miaka 126 aliyefahamika kwa jina la SUZANA BENJAMIN MMARI "Mateti".
Makala kumhusu mwanamke huyu yalichapishwa katika Gazeti la kila siku nchini Tanzania Daima Juni 13, 2020 uk. 9, 12-13 na mwandishi JABIR JOHNSON maarufu JOHNSON JABIR
Mwaka 1887 kazi ya Injili kwa Kanisa la Kilutheri ilianzishwa nchini Tanganyika (baadaye Tanzania) na Chama cha “Misioni cha Berlin III” au “Evangelical Missionary Society for East Africa” (EMS) kutoka Ujerumani. Kituo cha kwanza cha misheni kilikuwa ni Kigamboni, Dar es Salaam.
Chama cha pili, yaani “Chama cha Misioni Berlin I”, nacho kutoka Ujerumani, kiliingia Tanganyika kikitokea Afrika ya Kusini na kuanza kazi Nyanda za Juu Kusini mwaka 1891 kilipoanzisha kituo cha misheni sehemu iitwayo Ipagika au Pipagika (Wangemannshöhe) katika Dayosisi ya Konde.
Mwaka 1890 “Chama cha Berlin III” kilibadilika na kuchukua sura mpya baada ya kubadili sera yake na kujulikana kwa jina la “Bethel” au “Misioni ya Bethel”. Misioni hii ikafika Tanga na kuanza kazi eneo la Mbuyukenda. Baadaye Misioni ya Bethel iliamua kufikisha Injili ya Kristo nje ya mipaka ya Tanganyika. Wamisionari waliohusika walipanga kwenda Rwanda kupitia Bukoba. Walipofika Bukoba mwaka 1910 wakashawishika kufungua kituo Bukoba na ile nia ya kuanzisha kazi ya misioni Rwanda ikawa imesitishwa.
Chama cha tatu kufika Tanganyika ni “Chama cha Misioni cha Leipzig” (nacho kilitokea Ujerumani). Kiliingia nchini mwaka 1893 na kuanza kazi ya misioni Kaskazini ya nchi kwa kuweka kituo cha misheni Kidia, Old Moshi.
Wakati chama hicho cha Kimisheni cha Leipzig kilipokanyaga ardhi ya Kidia kilikutana na familia nyingi wakati huo utawala wa Kijerumani ulikuwa ukizozana sana na Mangi Meli ambaye hakukubalika kuchukuliwa mamlaka yake.
Miongoni mwa familia hizo ilikuwa familia ya Mzee Kornelio Letima Masamu ambayo ilikuwa miongoni mwa familia zilikuja baadaye kujiunga na kuwa sehemu ya kanisa hilo. Mwaka mmoja baadaye alizaliwa mtoto wa kike aliyepewa jina la Suzana Kornelio Masamu. Suzana akawa miongoni mwa waamini wa kanisa la Kilutheri wa Usharika wa Kidia ambako kazi ya Injili ya Umisheni kutoka Leipzig ilianzia hapo.
SIMULIZI YA KUSTAAJABISHA YA BI. SUZANA
Jina lake halisi ni Suzana Kornelio Masamu. Alizaliwa Aprili 23, 1894 huko Masamuni. Safari ya kuanza kuitwa Suzana Benjamin Mmari inaanzia hapa. Mara ya kwanza kabisa aliolewa na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Samwel Ndemanyisho Mmari.
Baada ya maisha ya ndoa ambayo hayakudumu sana mumewe Samwel alifariki na kumwacha akiwa mjamzito. Huzuni kuu ilimshika Suzana na kumlemea kiasi cha kusababisha kujifungua kabla ya wakati na mtoto alifariki dunia akiwa tumboni mwa mamaye; kwa maana Samweli hakufanikiwa kumzalia hata mtoto.
Kama ujuavyo mila na desturi za kichaga zilikuwa bado hazijashikamana na dini hivyo kuna baadhi ya mambo yalikwenda kimila zaidi. Baadaye wazazi wa pande zote mbili za Mmari na Masamu waliketi kitako na kuamua Suzana aolewe na mdogo wake Samweli Ndemanyisho ambaye ni Benjamin.
Ndoa ya pili ilifungwa mnamo Desemba 15, 1921 kwa kumbukumbu zilizopatikana katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kidia. Kwa lugha nyepesi ni kwamba Benjamin alipata bahati ya mtende kama ilivyokuwa kwa Onani katika Biblia. Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuitwa Suzana Benjamin Mmari.
Mumewe huyo alifariki miaka ya mwanzoni ya 1940 na kuzikwa hapo hapo Kidia. Na ndio sababu hata Bi. Suzana alizikwa pembeni ya kaburi la mumewe huyo. Wakati mumewe anafariki Bi. Suzana alikuwa na umri wa miaka 47. Alifariki dunia saa 4:15 asubuhi ya Mei 27 mwaka huu akiwa nyumbani kwake na kuzikwa siku tatu baadaye.
Bi Suzana maarufu kama Mateti au Kiwalii alifanikiwa kuzaa watoto sita, wanne wa kiume na wawili wa kiume. Bi Suzana ameacha wajukuu 92, vitukuu 305, vilembwe 173 na vilembwekeza sita.
SIKU YA MAZIKO
Mchungaji Sayuni Shao wa KKKT Usharika wa Kidia alisimama kwa ujasiri na kuzungumza haya, “ Siku ya leo tumekusanyika hapa, pamoja na kuwa tuna majonzi katika mwili lakini kwa kweli kurudisha shukrani nyingi kwa zawadi kubwa ya maisha na umri wa bibi yetu. Leo ni siku ya kumwimbia Bwana nyimbo za sifa. Ni siku ya kucheza mbele za Bwana. Ni siku ya kupiga vigelegele, vifijo nderemo. Ni siku ya kualika mataifa yote na kusema : Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele kama ambavyo Zaburi ya 136 inavyotulekeza na watu wote wasema Amen kubwa,” alisikika Mchungaji Shao.
Mchungaji Shao alimtaja Bi. Suzana, “aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya ushauri ya usharika wa Kidia. Mungu alimtumia sana katika eneo la mashauri ya ndoa. Pia aliwahi kuwa mzee wa kanisa, aliwahi kufanya kazi na wamisionari wa kwanza eneo hili. Miaka michache iliyopita alitembelewa na ugeni wa mjukuu wa Dkt. Bruno Gutmann, Janice walioijua historia yake tangu zamani hizo.”
WATU WANAVYOMZUNGUMZIA BI. SUZANA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima walisema kifo cha mwanamke huyo ambaye ameacha uzao wa watu 582 katika vizazi vitano sio cha kawaida na hakipaswi kuachwa kama kilivyo bila kumbukumbu hiyo kuhifadhiwa kwa vizazi vijavyo.
Mjukuu wa Bi. Suzana anayefahamika kwa jina la Noel anamtaja bibi yake kuwa alikuwa mcha Mungu, alipenda kuwahi kanisani kila mara, alikuwa mwombaji na kila jioni kabla ya kualalaliwaombea watoto na wajukuu zake mara nyingi kwa kuwataja majina.
Noel anasema Bibi yake alikuwa mwimbaji wa kwaya kanisa na nyumbani, alikuwa mkarimu kutoka moyoni uliojaa tabasamu na utajiri.
“Bibi laikuwa mchapakazi, aliweza kufuga na kutunza mifugo, kutunza mashamba Old Moshi na kulima shaba kubwa kwa mkono eneo la Lombeta, Msaranga, shamba ambalo kwa sasa tumepewa sisi wajukuu haitoshi bibi alikuwa kiunganishi cha ukoo katika mambo mbalimbali. Mungu alimpa hekima ya kuunganisha nyumba yake na ukoo kwa ujumla alikuwa mshauri,” anasema Noel.
Shangazi wa Bi. Suzana aliyejitambulisha kwa jina la Ailameni Massawe (87) anasema alimfahamu shangazi yake akiwa na umri wa miaka 20 wakati huo alikuwa anafanya kazi ya kutunza bohari katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi.
“Nimefanya kazi Hospitali ya Mawenzi miaka 30 tangu mwaka 1950 hadi nilipostaafu, shangazi yangu alikuwa mpole, mwalimu, msuluhishi, kiongozi mfano wa kuigwa hakika nitammiss sana,” anasema Massawe.
Mkazi wa Kiboriloni mjini Moshi aliyejitambulisha kwa jina la Gabby Mzei alisema kuna haja ya kuanzisha kitabu cha kumbukumbu za mambo ya Tanzania na Afrika kama ambavyo Guiness Book of World Records kinavyofanya huku kumbukumbu za Afrika zikiachwa nyuma.
“Kumbukumbu kama hizi hazipewi kipaumbele, nafikiri bibi yetu amekwishamaliza kazi yake hapa duniani lakini kuna ulazima wa kuwa na kitabu chetu ambacho kitafuatilia kwa karibu masuala haya na kuyaweka kwenye kumbukumbu ili vizazi vijavyo vione na vijifunze,” alisema Mzei.
Mwanadada aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Malisa wa Old Moshi alisema kuondokewa na kikongwe huyo ni suala ambalo limempa mafunzo makubwa ikiwamo kumwamini Mungu na kujitunza licha ya changamoto mbalimbali za kimaisha.
“Historia yake ni ya kuvutia hakika imenivutia na mimi imenipa changamoto ya kuendelea kumtumaini Mungu na kuishi kwa nidhamu kubwa kwani bibi nilikuwa nikimuona na kuzungumza naye alikuwa kiongozi na mwalimu, alimpenda Mungu kwa kweli na alikuwa anawahi kanisani,” alisema Mariam.
Mkazi wa Soweto mjini Moshi aliyejitambulisha kwa jina la Hilaria alisema kuondokewa na kikongwe huyo kunaonyesha dhahiri namna gani Tanzania ilivyojisahau kufuatilia mambo yake kwa ajili ya vizazi vijavyo kwani akiwa hai hakuna aliyekuwa akimfahamu sana mwanamke huyo.
“Tunakwama wapi sisi watanzania, alipokuwa hai mwanamke huyu hakufahamika na wengi mpaka alipofariki, ni simanzi kwa vizazi vijavyo. Kuna ulazima wa kuanza kuchukua hatua stahiki kutunza kumbukumbu na kufuatilia mambo yetu,” alisema Hilaria.
Kwa upande wake Malisa GJ aliandika katika ukurasa wa Facebook kuhusu kifo hicho ambapo alisema Afrika imeachwa mbali katika kumbukumbu mbalimbali ikiwamo ya Suzana Benjamin Mmari.
“Ni bahati mbaya kwamba taasisi zinazotunza rekodi za dunia haziangalii sana Afrika, lakini kabla hajafariki alipaswa kuwa ndiye mwanadamu mwenye umri mkubwa zaidi (the oldest living person),” aliandika Malisa GJ.
UTATA WA TAREHE YA KUZALIWA
Profesa Haroub Othman mnamo Julai 3, 2006 alikaririwa akisema kumbukumbu za mambo mbalimbali na muhimu kwa taifa imekuwa changamoto katika utunzaji wake kutokana na utamaduni wa Mwafrika wa kutumia kinywa (simulizi) kutunza kumbukumbu hizo.
"Tatizo letu kama nchi ni kuwa vichwa vya wazee na viongozi wetu ndio maktaba za kumbukumbu za mambo muhimu ya Taifa. Sasa wanapofariki, hufariki na kumbukumbu hizo. Hii si sahihi hata kidogo. Ni muhimu kama Taifa tuchukue hatua madhubuti ili kumbukumbu hizi zihifadhiwe vitabuni, Maktaba na Makumbusho ya Taifa" alisema Profesa Haroub.
Katika kitabu cha “Historia ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Afrika Mashariki 1902-1912 (Kilimanjaro, Arusha, Meru na Pare)” kilichoandikwa kwa lugha ya Kidachi na Mchungaji K. Adolph na Mchungaji Johannes Shantz wa Leipzig na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na Anthony Payne wa London, Uingereza kisha kwa Kiswahili na Mshumbue Marealle II, OBE na Rusk Shirima Kishimba katika Uk. 36 kinaeleza namna Wachungaji Fussmann, Sagebrock na Von Lany waliingia katika ardhi ya uchagani na hali waliyoikuta kabala ya mwaka 1900.
Waliukuta utawala wa Kijerumani tayari umeshaota mizizi hivyo wachungaji hao walijumuika kuanzisha kituo cha tatu katika ardhi ya Uchagani hapo Moshi. Lakini hali haikuwa nyepesi kwani wamisionari wa kwanza wa Kiingereza walishindwa kabisa kuanzisha kazi yao hapo Old Moshi kabla ya mwaka 1892 kutokana na upinzani wa Mangi Meli.
Kamanda wa Kijerumani aliyefahamika kwa jina la Kapteni Johannes alifanikiwa kuwaokoa wageni hao na kuwakabidhi kipande cha ardhi kilichokuwa kiasi cha robo tatu umbali kidogo kutoka katika boma la serikali hapo Old Moshi. Ardhi hiyo ilikuwa usawa wa mita 1450 kutoka usawa wa bahari.
Hapo mahema yalijengwa na hapo hapo nyimbo za dini zikaimbwa, sala zilifanywa na zaburi zikasomwa. Hadi Machi 24, 1896 nyumba ya makao ya muda, ya kuta za udongo na paa la makuti. Lilikuwa tayari kuhamiwa. Milango ya nyumba hiyo ilitengenezwa kutokana na mbao zilikuwa zimetumiwa kama masanduku ya mizigo na kushikizwa na misumari.
Hapo ndipo wakaja mafundi wajenzi wa Kitamil kutoka Machame na wakaanza kujenga majengo imara ya Misheni. Kazi rasmi ya kufundisha dini na masomo zilianza kwa pamoja Machi 15, 1896 Ibada ya kwanza ya lugha ya Kichaga na Kiswahili ilifanyika na Aprili 22, 1896 mafundisho ya dini yalianzishwa na mahali hapo walipopewa paliitwa Kidia.
Ubatizo ni miongoni mwa mafundisho ya dini ambapo wengi walibatizwa kabla ya mwaka 1900 lakini ilipofika mwaka 1905 Suzana akiwa na umri wa miaka 11 alibatizwa na kipaimara alipata akiwa na umri wa miaka 25 yaani miaka 14 baadaye ambayo ilikuwa Machi 20, 1919.
Bi Suzana anakumbuka vizuri katika rekodi zake miongoni mwa wajukuu zake walisema kuwa aliwaambia alibatizwa ukiwa ni mwaka mmoja baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kumalizika na wakati huo akiwa na umri wa miaka 25.
Hii ina maana kuwa Bi. Suzana alizaliwa mnamo mwaka 1894 na sio 1889 kama ambavyo iliandikwa kwenye msalaba wakati wa maziko yake. Hoja ni kwamba kama Bi. Suzana alipata kipaimara akiwa na umri wa miaka 25 kama alizaliwa 1889 basi ingekuwa mwaka 1914, hoja ambayo inapingwa na maneno yake kwa wajukuu zake kuwa alipata kipaimara baada ya vita kumalizika kwani mwaka 1914 ulikuwa ndio mwanzo wa Vita vya Kwanza vya Dunia na vilimalizika 1918.
Bi. Suzana Benjamin Mmari ni mwanamke aliyepata neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuziona karne tatu, yaani karne ya 19, 20 na 21.Kikongwe huyu alipenda nyimbo kadhaa za Kikristo lakini huu aliupenda zaidi: “Njewuka Ko Yesu Fo, Amekenjikumbia Moo…..” yaani Sitatoka kwa Yesu kamwe, Kwani amekufa kwa ajili yangu.
BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE AMEN.
0 Comments:
Post a Comment