Chanzo cha Afrika Kusini kama nchi ni Rasi iliyoundwa
na Waholanzi katika eneo la Cape Town. Huko kabila jipya la Makaburu
lilijitokeza kati ya walowezi Wazungu kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani.
Lugha yao ilikuwa Kiholanzi iliyoanza kuchukua maneno ya Kifaransa, Kiafrika na
Kiingereza na kuendelea kuwa lugha ya pekee Kiafrikaans.
Karne za kwanza za koloni la Kiholanzi ziliona pia
kufika kwa watumwa kutoka Indonesia walioletwa kama wafanyakazi wa Waholanzi na
Makaburu. Hao Waindonesia walikuwa chanzo cha jumuiya ya Uislamu kwenye rasi
hiyo.
Pia machotara walitokea kutokana na kuzaliana kati ya
Makaburu na wanawake Waafrika na Waindonesia. Sehemu ya machotara hao wameingia
katika jumuiya ya Makaburu na wengi wao wanapimwa kuwa na mababu Waafrika.
Katika miaka iliyofuatia ubaguzi wa rangi uliongezeka
na watoto machotara wa Wazungu na Waafrika mara nyingi hawakukubalika; walianza
kuishi kama kundi la pekee kati ya Waafrika na Wazungu, nao ni chanzo cha hao
walioitwa baadaye "Cape Coloreds".
Mwaka 1814 Rasi ya Tumaini Jema (Good Hope) ilitwaliwa
na Waingereza na kuwa sehemu ya Milki ya Uingereza. Utawala wa Waingereza
ulisababisha uhamisho wa nje wa sehemu ya Makaburu waliotokana na Wazungu
kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani; Makaburu hao walihama kwenda kaskazini
wakaanzisha jamhuri ndogo kati ya maeneo ya Waafrika ama kwa njia ya mapatano
au kwa njia ya vita.
Kati ya miaka 1840 na 1850 Waingereza waliwafuata
Makaburu kwa kuenea kutoka maeneo yao hadi mto Oranje; waliteka Jamhuri ya
Kikaburu ya Natalia na kuanzisha koloni jipya la Natal.
Jamhuri mbili za Makaburu ziliweza kustawi kwa miaka
kadhaa ambazo zilikuwa jamhuri ya Dola Huru la Oranje upande wa kaskazini wa
mto Oranje na Jamhuri ya Transvaal (ilijiita pia Jamhuri ya Kiafrika ya Kusini)
upande wa kaskazini wa mto Vaal.
Milki za Kiafrika zilitafuta njia zao kati ya himaya
hizi za Wazungu ambao walikuwa na nguvu kutokana na silaha za kisasa. Wengine
walitafuta uhusiano mzuri na Makaburu na kushikamana nao; wengine waliona
Makaburu kama hatari wakatafuta uhusiano wa ulinzi na Waingereza.
Mikataba kati ya Waingereza na milki za Kiafrika
iliunda nchi lindwa zinazoendelea hadi leo kama nchi huru kama vile Botswana
(Bechuanaland), Lesotho (Basutoland) na Uswazi (Swaziland).
Katika miaka ya 1880 almasi na dhahabu zilipatikana
kwa wingi katika Jamhuri hizi na kusababisha kufika kwa wachimbamadini wengi,
hasa Waingereza, waliotaka kutajirika; Makaburu walisita kuwapa haki za kiraia
kwa sababu waliogopa wageni wengi. Tatizo hilo lilisababisha vita vya Makaburu
dhidi ya Uingereza na Jamhuri za Makaburu zilitwaliwa na jeshi la Kiingereza
hadi mwaka 1902 zikawa makoloni.
Jitihada za kupatanisha Wazungu wa Afrika Kusini
(yaani Waingereza na Makaburu) zilisababisha kuundwa kwa Muungano wa Afrika
Kusini kama nchi ya kujitawala ndani ya Milki ya Uingereza. Waafrika kwa jumla
hawakuwa na haki za kiraia katika nchi hiyo isipokuwa katika Jimbo la Rasi kama
walikuwa na elimu na mapato ya kulipa kodi za kutosha.
Baada ya vita kuu ya pili ya dunia Chama cha National
kilichofuata itikadi kali kilipata kura nyingi na kuchukua serikali ya Afrika
Kusini. Hapo kilianzisha mfumo wa ubaguzi wa rangi kwa jina la apartheid.
Haki za wasio Wazungu zilipunguzwa zaidi. Maeneo ya
Kiafrika yalitangazwa kuwa nchi za pekee chini ya usimamizi wa serikali ya
Kizungu ya Afrika Kusini; kwa hiyo wananchi kutoka maeneo hayo hawakuwa tena na
haki za kukata rufaa mbele ya mahakama; walipewa vibali vya muda tu kukaa
kwenye miji. Waafrika walipaswa kutembea muda wote na pasipoti na vibali; ndoa
na mapenzi kati ya watu wa rangi tofauti zilipigwa marufuku. Shule na makazi
zilitenganishwa.
Siasa hiyo ilisababisha mafarakano kati ya nchi nyingi
za dunia na Afrika Kusini. Upinzani kutoka Uingereza na Jumuiya ya Madola
ulisababisha kuondoka kwa Afrika Kusini katika jumuiya hiyo na kutangazwa kwa
Jamhuri ya Afrika Kusini.
Wenyeji wa taifa hilo ambao hawakupewa haki zao
walianzisha ghasia ikiwa ni sehemu ya kupaza sauti ya kutaka haki zao. Lakini
ziliwagharimu wengi wao walipoteza maisha kwani mamlaka za serikali
hazikuwaacha kirahisi. Wengine walitupwa jela na kutumikia vifungo mbalimbali.
Mauaji ya Sharpville ya Machi 21, 1960 ni miongoni mwa
vuguvugu za kupinga sera hizo za kibauguzi nchini Afrika. Tukio hilo lilionyesha
mwanzo wa upinzani wa silaha nchini Afrika Kusini, na kushawishi ulimwengu kupinga
sera za ubaguzi wa Afrika Kusini.
Waafrika wapatao 180 walijeruhiwa (kuna madai kuwa
walikuwa zaidi ya 180) na 69 waliuawa wakati polisi wa Afrika Kusini walitumia
silaha kuwazuia waandamanaji wapatao 300, ambao walipinga sheria hizo, katika
mji wa Sharpeville, karibu na Vereeniging huko Transvaal.
Katika maandamano kwenye kituo cha polisi huko
Vanderbijlpark, mtu mwingine alipigwa risasi. Baadaye siku hiyo hiyo huko
Langa, nje ya Cape Town, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kwa
waandamanaji waliokusanyika, wakipiga risasi tatu na kujeruhi wengine kadhaa.
Mauaji ya Soweto ya Juni 16, 1976 ni miongoni kati ya
harakati za kupinga sera za kibaguzi nchini Afrika kusini zilizopitishwa Juni
24, 1950.
0 Comments:
Post a Comment