Monday, June 22, 2020

Wanaosambaza vipeperushi vya Freemason waonywa

Watu wanaojihusisha na masuala ya Freemason na kusambaza vipeperushi vya watu kujiunga na kundi hilo kwa ajili ya kupata mafanikio na utajiri wametakiwa kuacha kutupa vipeperushi hivyo katika mji wa Manispaa ya Moshi la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hayo yanajiri baada ya kuzagaa kwa vipeperushi vilivyoandikwa maneno ya kumtaka mtu kujiunga na Ufreemason yakiwa na nembo ya 666 huku namba za simu na picha za utajiri zikiwekwa katika vipeperushi hivyo.

Akizungumza ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Michael Mwandezi alisema kumekuwa na operesheni ya mara kwa mara ya kuwakamata wanaosambaza vipeperushi hivyo na kuwatoza faini kutokana na makosa hayo.

“Tumekuwa tukiendesha operesheni ya mara kwa mara kuwakamata wanaosambaza vipeperushi hivyo kwani wanatuharibia mji wetu wa Moshi, tunahamasisha mafanikio yanayopatikana kwa kufanya kazi za haki badala ya kusubiri bahati na tumekuwa tukiwakamata na kuwatoza faini,” alisema Mwandezi.

Mwandezi aliongeza kuwa vipeperushi hivyo vimekuwa vikichafua mazingira ya mji wa Moshi ambao umekuwa kinara wa usafi nchini na kwamba kufanya hivyo ni kuwarudisha nyuma.

“Moshi tunaendelea kuiweka safi siku zote, hawa wanaotupa vipeperushi tena vya freemason ni hatari kwa mazingira kwani mji unakuwa mchafu na tunasisitiza hilo halikubaliki katika Manispaa yetu,” aliongeza Mwandezi.

Kwa upande wake Afisa Afya wa Manispaa ya Moshi Sebastian Mgeta alisema wamekuwa wakifuatilia na kutoa angalizo kwa watu wanaofanya hivyo lakini changamoto kubwa ni kwamba watu wanaosambaza vipeperushi hivyo huwa sio wakazi wa Moshi na huingia mjini hapo na kuvisambaza kisha kuondoka.

“Wengi wao sio wa hapa Moshi, huwa wanaingia na kusambaza nyakati za usiku, halafu hawakai, kikubwa ni kwamba kuna sheria ndogo ndogo na zile za mazingira ambazo huwa tunazitumia kuwabana watu wa jinsi hiyo. Huo ni uchafuzi wa mazingira na hatari kwa afya ya jamii,” alisema Mgeta.

Mgeta aliwataka wakazi wa Manispaa ya Moshi kuendelea kutoa ushirikiano pindi wanapoona watu wa jinsi hiyo wakisambaza na wakati mwingine wakivitupa huku akisisitiza uelewa jinsi ya kuufanya mji wa Moshi kuendelea kuwa safi utasaidia kupiga vita usambazaji wa vipeperushi hivyo vya Freemason.


0 Comments:

Post a Comment