Friday, June 5, 2020

Unaijua sababu ya Binadamu kuishi miaka mingi?

Mbwa aliambiwa: Utalinda nyumba za watu, utakuwa rafiki bora wa mwanadamu, utakula makombo atakayokuachia, na utapewa umri wa miaka 30.

Mbwa akasema: Miaka 30 ni mingi, nataka miaka 15 tu. Akapewa.

Kima aliambiwa: Utarukaruka kutoka tawi hili kwenda lingine. Utakuwa na kazi ya kuwahadaa na kuwachekesha watu. Utaishi miaka 20.

Kima akasema: Miaka 20 ni mingi nataka miaka 10 tu. Akapewa.

Punda aliambiwa: Utafanya kazi kuanzia mawio mpaka machweo na kubeba mizigo mizito mgongoni mwako. Utakula shayri, hutokuwa na akili, na utapewa umri wa miaka 50.

Punda akasema: Nimekubali kuwa punda, lakini miaka 50 ni mingi sana, nataka miaka 20 tu. Akapewa.

Mwanadamu aliambiwa: Wewe utakuwa kiumbe mwenye akili zaidi duniani, utaitumia akili yako kuwaongoza viumbe wengine, utaishi maisha mazuri ili kuiendeleza dunia, na utapewa umri wa miaka 20. Mwanadamu uwa hatosheki kabisa. Hivyo basi….!

Mwanadamu akasema: Niwe mtu wa kuishi miaka ishirini tu? Hiyo ni michache mno. Nataka ile miaka 30 aliyoikataa punda, ile 15 aliyoikataa mbwa, ile 10 aliyoikataa kima. Akapewa.

Tangu wakati huo mwanadamu huishi miaka 20 kama mtu, kisha huoa au kuolewa. Baada ya hapo anaishi miaka 30 kama punda, akifanya kazi kuanzia mawio mpaka machweo na kubeba mizigo mizito mgongoni mwake.

Watoto wake wanapokuwa wakubwa anaishi miaka 15 kama mbwa akilinda nyumba, kufunga milango na kuzima umeme na kula chakula kidogo au makombo anayoachiwa na watoto wake.

Anapozeeka na kustaafu anaishi miaka 10 kama kima. Anahama kutoka nyumba hii kwenda nyingine, na kutoka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mwingine. Anatengeneza uongo na visa ili kuwachekesha wajukuu zake.

Hivyo kila hatua anayopiga mwanadamu inampa majukumu na sifa fulani. Usifanye mambo ya vijana kama umeshazeeka na usifanye mambo ya wazee ungali kijana.


0 Comments:

Post a Comment