Tuesday, June 30, 2020

Nyumba isiyokalika katika 'Bwawa la Damu' kwa Mangi Horombo

Baadhi ya wasomi wamezigawanya ndoto katika katika makundi makuu matatu, kundi la kwanza wanasema ni zile ndoto zinazotokana na Mungu, kundi la pili ni zile zinazotokana na shetani na kundi la tatu ni ndoto zinazotokana na mtu mwenyewe.

Kundi hili la tatu linatafsiriwa kuwa ndizo zinazochukua sehemu kubwa ya ndoto tunazoziota karibu kila siku kwenye maisha yetu. Wanachambua kwa kina kuwa aina hii ya tatu huwa inakuja kutokana na shughuli zetu tunazozifanya kila siku au mazingira yanayotuzunguka kila siku.

Wakati mwingine unaweza ukaota umefiwa na mzazi, au kaka au dada, au mtu wako wa karibu. Na ndoto hizi huwa zinakuja kwa uzito sana, kiasi kwamba unaposhtuka huamini kama kweli ilikuwa ni ndoto, kwasababu unaona kama tukio hilo lilikuwa ni halisi kabisa, unabaki kuishia kumshukuru Mungu na kusema asante  kwa kuwa ilikuwa ni ndoto tu huku ukihema kwa nguvu.

Kuna wakati unaota ukiwa utupu, halafu unakatiza barabara hususani maeneo ya mjini. Ukiwa ndani ya ndoto  unajiona na kuanza kutafuta namna ya kujificha, unajibanza katika vichochoro kisha unavizia watu wapungue ili ukimbilie upande mwingine. Wakati ukiyafanya hayo unakimbia na kurudi nyumbani ukidhani kwamba hujaonekana na wengi.

Muda kidogo wanakuja marafiki zako wa kike na kukuuliza mbona kuna picha zako zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii zikikuonyesha ukikatiza barabara ukiwa utupu na wakati wewe ni wa kiume, sasa linageuka songombingo ndani ya ndoto unaishiwa nguvu, unajiona ukipata fedheha ya milele isiyoweza kufutika unatamani kama ardhi ipasuke ikufukie.

Pia wakati mwingine unaota unapaa na watu usiowajua na wanakupeleka usipojua, au unaenda sehemu za kutisha, na unapoamka unakuwa huna amani umejawa na hofu na wasiwasi mwingi. Ndoto kama hizi huwa zinawapata watu wengi. Hata hivyo inakuwa ni vigumu kutoa jibu la moja kwa moja kuhusu ndoto hizo na vyanzo vyake ama Mungu au Shetani au mtu mwenyewe.

Sasa basi hitimisho kubwa hubaki katika kipengele kinaitwa mitholojia. Inavyoaminika ndoto huja kuelezea jambo moja kwa moja kama lilivyo au kinyume chake au huelezea kwa njia ya mifano na wakati mwingine huja kama fumbo.

Katika makala haya tutaangazia namna ambavyo nyumba iliyojengwa katika milki ya zamani ya Mangi Horombo huko Rombo mkoani Kilimanjaro ilivyozua tafrani na kusababisha watu kuiacha ukiwa, kutokana na ndoto na mauzauza kibao kwa waliokuwa wakiikaa hapo.

Mtunzaji wa eneo hilo Melania Peter Urio (65) anasema hakubahatika kumwona Mangi Horombo isipokuwa alikutana na taarifa mbalimbali zinazomhusu mangi huyo, miongoni mwa hizo ni eneo hilo linalofahamika kama ‘Bwawa la Damu’.

SABABU ZA KUITWA BWAWA LA DAMU

Sababu kuu za kuitwa Bwawa la Damu ilikuwa ni mauaji yaliyokuwa yakifanyika katika eneo hilo la Milki ya Mangi Horombo wakati wa vita vya koo zilikuwa zikipingana na kujiunga na utawala wa Mangi huyo.

Bi Melania anasema kuwa eneo hilo lilikuwa la maoteoni wakati wa vita inapokuwa kali walikuwa wakijificha na mara maadui walipokuwa wakiingia hapo walivamiwa na kuuawa.

“Mangi Horombo alilitengeneza kwa ajili ya ulinzi, maadui walipokuwa wakija waliwapitisha kwenye upenyo uliokuwa wazi huku wenyewe wakiangalia kutoka juu wakiingia hapo wanawaulia na kuwachoma moto,” anasema Bi. Melania.

Bi Melania anasisitiza kuwa askari wa Mangi Horombo walikuwa wakitumia mbinu ya kushtukiza kuzivamia koo fulani fulani na kujifanya kama wamezidiwa hivyo kuanza kukimbia, pindi wanapokimbia hukimbilia katika uelekeo ulipo upenyo ambao lazima maadui watawafuata kwenye mtego huo.

“Mara zote mtego huu uliwanasa maadui wengi na waliuawa wa kutosha, kwasababu maaskari wengine walikuwa wamejificha juu, …” anasema Bi. Melania.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni  wa wilaya ya Rombo Florentine Henrico Langu, anasema kuwapo kwa Bwawa la Damu ni miongoni mwa vivutio vya utalii wa utamaduni katika wilaya hiyo ambao unaweza kukuza utalii wa ndani kutokana na wilaya hiyo kuwa na vivutio vingi vya asili.

UWEPO WA NYUMBA YENYE MAUZAUZA

Baada ya miaka mingi kupita, na eneo hilo kuanza kupotea palionekana kama tambarare nzuri ambayo inafaa kujengwa, ndipo baadhi ya wana ukoo wa Mangi Horombo waliamua kujenga nyumba hapo kwa ajili ya kuishi.

Nyumba hiyo ilikamilika na wahusika hawakukaa sana wakaondoka lakini inaelezwa kuwa hakuna mtu yeyote anayetaka kukaa humo kutokana na hofu inayojitokeza wakati wa usiku kwani ndoto ndoto za ajabu haziishi.

Bi Melania anasema wenye nyumba baada ya kumaliza ujenzi huo walienda zao Dar es Salaam, lakini waliamua kuwaacha watu wa kuilinda lakini baadaye watu hao waliondoka kutokana na mauzauza hayo.

“Mwenyewe unaiona nyumba, ilivyo nzuri lakini hakuna anayetaka kukaa, hata wa kupanga hawataki kila mmoja anahofia usalama wake ndoto za ajabu zinawajia,nyumba inaota nyasi tu,” anasema Bi. Melania.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu sababu za mauzauza hayo ni kwamba huenda kutokana na damu iliyomwagika hapo hasa kutokana na Mangi Horombo ambaye alikuwa mbabe na mwenye nguvu zote za kimwili na kiroho.

“Huyu Mangi Horombo alikuwa kama wachifu wengi ambao walikuwa wakimiliki maeneo na kuzishinda koo nyingine hata kwa uchawi, inawezekana hata kuwateketeza kwenye eneo hili kulitokana na kuwapumbaza kichawi,” anaongeza Bi. Melania.

Mangi Horombo alifariki dunia akiwa na miaka 82 mnamo mwaka 1802. Katika mkoa wa Kilimanjaro Mangi Horombo ndiye pekee aliyeenziwa kwa jina lake kusalia katika ukumbusho wa vizazi hata vizazi.

Kwasababu mkoa wa Kilimanjaro una wilaya za Hai, Same, Mwanga, Moshi na Rombo. Wilaya ya Rombo pekee katika kupewa jina hilo ilichaguliwa kutokana na Mangi Horombo.

Pia wakati unapopanda mlima Kilimanjaro kwa njia ya Marangu kuna kituo kinafahamika kwa jina la Horombo hiyo ni kwasababu ya umarufu wa Mangi Horombo aliyekuwa mtawala wa eneo ambalo kwa sasa ni Rombo.

Historia yake ni ndefu lakini sifa yake ya ubabe kwa wakorofi na mpatanishi kwa waliogombana vilimfanya ajichotee umaarufu katika kuteka koo mbalimbali.

Alifariki dunia wakati vita na koo moja upande wa Kenya. Inaelezwa alipigwa mshale wenye sumu kali na kupoteza maisha. Jina lake halisi alilopewa wakati anazaliwa ni Maingudu.

0 Comments:

Post a Comment