Juni 9, 68 alifariki dunia mtawala wa Rumi
aliyefahamika kwa jina la Nero. Mtawala huyu aliitawala Rumi yote kutoka mwaka
54 hadi kifo chake.
Nero alikuwa mtawala wa mwisho kutoka ukoo wa Julio-Claudia.
Nero aliasiliwa na mjomba wake mkubwa na baadaye akawa mrithi na aliyekalia
kiti cha kuliongoza dola hilo.
Nero aliingia madaraka na kukubaliana ulinzi wa
bodigadi kutoka Jeshi la Kifalme ambao walikuwa na kazi ya kuwalinda watawala
wa Kirumi. Walinzi hao walikuwa katika kikosi cha kijeshi chenye mafunzo ya
hali ya juu kilichofahamika kama Praetorian.
Mama yake Nero aliyefahamika kwa jina la Julia
Agrippina maarufu Agrippina the Younger alishikilia maisha na hatima ya Nero
kwa miaka ya mwanzoni ya maisha yake. Miaka ya mwanzoni ya utawala wake Nero,
maelekezo mengi alikuwa akiyapokea kutoka kwa watu watatu ambao walimfanya awe
imara. Mama yake, mwalimu wake aliyefahamika kwa jina la Lucius Annaeus Seneca
na bodigadi mkuu kutoka Praetorian aliyefahamika kwa jina la Sextus Afranius
Burrus.
Kadri miaka ilivyozidi kwenda Nero alianza kusimama na
kujitegemea katika serikali na sera zake za kigeni. Aidha wakati wa utawala
wake Nero alikuwa na wasiwasi na Jenerali Corbulo ambaye alifanya vizuri katika
vita na kuingia mikataba ya amani na Dola la Parthian katika umiliki wa
Armenia.
Jenerali Corbulo aliogopeka hasa hatua iliyomfanya
Nero amuaru ajiue. Lakini kabla hajafanya hivyo Jenerali Corbulo alisema maneno
haya, “Nina thamani” kisha akauangukia upanga na kufa.
Pia alikuwa na Jenerali mwingine mahiri aliyefahamika
kwa jina la Suetonius Paulinus ambaye aliongoza mapambano ya kumwangusha Malkia
Boudica huko nchini Uingereza.
Licha ya falme nyingine kutaka kuonyesha uwezo wao
mbele yake Nero aliendelea na mipango ya ndani ya kuijenga Rumi ikiwamo
kutafuta diplomasia na dola nyingine, kufanya biashara na kuiweka Rumi
kiutamaduni zaidi akiamuru ujenzi wa kumbi za starehe na muziki pia kukuza
michezo. Hata hivyo bado utawala wa Nero unachukuliwa kuwa ulikuwa wa kikatili.
Mnamo mwaka 68 Gavana wa Gaulish (Gallia Lugdunensis)
aliyefahamika kwa jina la Vindex aliamua kumpindua Nero. Katika jaribio hilo
lililoshindwa Vindex alisaidiwa na Galba ambaye alikuwa Gavana wa Tarraconensis
upande wa Hispania.
Hata hivyo Nero alikimbia Rome wakati ambao mamlaka za
kiraia na kijeshi zilipomchagua Galba kuwa mtawala wa Rumi. Nero aliamua kujiua
Juni 9, 68 baada ya kuona kuwa anahukumiwa pasipo mlalamikaji (trial in
absentia) na kwamba aliona akihukumiwa mbele ya hadhira kama adui wa umma.
Kitendo cha kujiua kilimweka Nero kuwa mtawala wa kwanza
wa Rumi kujiua. Kifo chake kilianzisha kipindi kingine kigumu kwa Dola la Rumi ambapo
vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza ambapo watawala wanne waliwania nafasi ya
uongozi.
0 Comments:
Post a Comment