Nianze na kutoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa
Jamhuri Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli huwa napendelea kumwita JPM,
kwa kile ambacho umekifanya kuruhusu kwa awamu suala la wanafunzi kurudi kwenye
masomo yao, hilo ni jambo jema.
JPM umekuwa kitovu cha habari zote ulimwenguni kuhusu
msimamo wako pale ulipopeleka mapapai na sungura kwenye ile mashine yetu na
vikabaini kuwa na vyenyewe vina ugonjwa wa Covid-19 isipokuwa haukutupa taarifa
kama na vyenyewe viliwekwa karantini. Kilichofuata ukaikarabati ile maabara tu.
Leo nisingependa kujikita katika mtazamo huo wa watu
wa nje ambao kila wakati wanataka tutazame masuala kama ambavyo wao wamekuwa
wakitazama (Eurocentric view).
Hapo ndipo ninapomkumbuka Li Peng aliyekuwa
akifahamika kwa jina la ‘Bucha la Beijing’ wakati wa maandamano ya kushinikiza
masuala kadhaa yaliyofanywa na wanafunzi pale Tiananmen Square mnamo mwaka
1989. Walitulia pale kwa miezi mitatu hatimaye Juni 4 ya mwaka huo walijua
kwanini aliitwa ‘Bucha la Beijing’. Lakini msimamo wake ulisaidia kuifanya
China iwe hivi kwa kiasi tunavyoiona hivi leo kwa maana yeye alitazama kwa
mtazamo wa Kichina kuhusu wapi China anataka ifike.
Nijikite katika hili janga la Corona hapa nchini
kwetu, nafurahi kusikia umerudisha wanafunzi vyuoni na utaendelea kwa kadiri
utakavyoona hali inavyokwenda.
Binafsi nirudi katika suala la misibani, tunafahamu
kuwa binadamu tukishazaliwa lazima tufe lakini tunaobaki huwa tuna taratibu za
kuwahifadhi marehemu wetu.
Sasa tangu janga la corona ambalo pia limeikumba nchi
yetu taratibu zimebadilika kidogo ikiwamo ya idadi ndogo ya washiriki wa tukio
hilo ambayo imekuwa ikizingatiwa.
Ningependa kujua kama ulitukaza hata tusinywe maji ya
msibani na pia kwa idadi yetu wachache wakati wa kuzika hata pilau tusile eti
kisa corona.
Sijasikia popote ukitoa maelekezo kwa viongozi wa
vitongoji, vijiji na kata au hata wakurugenzi au wakuu wa wilaya na mikoa
kuhusu hili la kula na kunywa msibani.
Chonde chonde JPM tuweke sawa na hili nalo tunahitaji
majibu maana sasa hivi ujue watanzania wanakusikiliza wewe tu kuhusu
utakalosema. Hata Makonda mwenyewe hasikilizwi kama unavyosikilizwa wewe.
Litolee maelezo maana misiba huku kwetu ni kila siku.
Viongozi wanafika asubuhi kuhakiki kama tumepika pilau letu kwa ajili ya msiba
na maji na wanatoa maelekezo hakuna kunywa maji msibani.
Nakumbuka uliwahi kusema tuzaliane tuijaze Tanzania
yetu kweli wengi wanaendelea kulitendea kazi, sasa kwetu tupo kumi bado
shangazi na kina mjomba hawajafika na wakwe kama kumi na tano hivi.
Kabla ya msiba tulikuwa tukipika pilau lakini wakawa
hawaji kukagua kama maambukizi yanaweza
kutokea. Hivi sasa tu kwenye msiba tupo kumi wakati wa kuzika tayari vikwazo
kama vyote. Litolee majibu maana nionavyo wamekuwa waoga na wanafiki
kupitiliza.
Halafu JPM huku kwetu pia mahindi yameanza kutoa
mbelewele najua unafahamu siku nyingi, kipindi kama hiki kwa baadhi yetu lazima
tukohoe kutokana na unga unga ule wa mbelewele sasa sijui na lenyewe hili
tusaidie japo kidogo kutupa maelekezo tusije tukashikwa vikohozi kisha viongozi
wako ambao wamekuwa wakifuata maagizo yako na wakati mwingine wamekuwa
wakipitiliza wakapitiliza kwelikweli.
Kwa mfano kama chuo kipo karibu na shamba la mahindi
na upepo ukawa unavuma kuelekea darasani au mabwenini au walikopanga wanafunzi
hao na ungaunga wa mbelewele ukaenda huko.
Itakuwa tafrani darasani humo JPM nakueleza na penyewe
wametoka kurudi baada ya vyuo kufungwa. Hapatatosha.
Pia nimesikia hata hospitalini ukipelekwa wauguzi
wanasema, “…tubu kabisa, muombe Mungu akusamehe dhambi zako zote…,” sasa hapo
mgonjwa atapona kweli maana kila ukiumwa basi ni corona.
Kama utaona inafaa basi funga tu mjadala huu wa corona
kwa kuruhusu kila kitu kifanye kazi kama mwanzo tubaki kumtumainia huyu Mungu
na akili zetu za mbayuwayu, maana kama imefikia hatua naambiwa nitubu dhambi
zangu zote ninapofikishwa hospitalini hii ni hatari.
0 Comments:
Post a Comment