Tuesday, June 16, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: George Stinney Jr. ni nani?

Juni 16, 1944 alifariki dunia kijana mdogo mwenye asili ya Kiafrika nchini Marekani George Stinney Jr. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 14. Alizaliwa Oktoba 21, 1929.

Stinney Jr. alihukumiwa kifo kwa kupigwa shoti ya umeme kwa kosa la kuwaua watoto wawili wa kizungu wenye umri wa miaka 7 na mwingine 11.

Miaka 70 baadaye ilibainika kwamba Stinney Jr alihukumiwa kimakosa kwa kosa ambalo hakulifanya. Saa 1:30 asubuhi ya Juni 16, 1944 Stinney Jr. mfungwa mwenye Na. 260 akiwa amevalia mavazi ya wafungwa  wa jela la Columbia huko South Carolina, alisindikizwa na askari jela hadi kwenye jengo dogo la matofali maalum kwa ajili ya kutekeleza hukumu ya kifo.

Wakati hayo yote yakitokea Stinney Jr. alikuwa ameshikilia Biblia yake kwani hapo kabla alikuwa mshirika wa Kanisa la Greenhill Missionary Baptist.

Mbele ya hadhira ya watu takribani 50 wakiwamo wazazi wa watoto waliouawa aliulizwa Stinney Jr. kuwa ana neno lolote la mwisho, mtoto yule ambaye alikuwa na uzito wa kilo 43 alisikika akisema, “No, Sir.” Akaulizwa tena kuna lolote unalotaka kusema kuhusu mauaji haya, akajibu “No, Sir.”

Kofia ya umeme yenye Volti 2,400 ilivikwa kichwani mwake, macho yake yalikuwa yakishuhudia hatua zote hizo huku mate yakimtoka mtoto Stinney Jr. Ikafuatiwa na shoti ya umeme wa volti 1,400 kisha volti nyingine 500 katika sehemu aliyokalia.Hapo ndipo habari ya Stinney Jr. ilipoishia.

Dakika 3 na sekunde 45 wahudumu walifika na kuuondoa mwili wa George Stinney Jr. Mashuhuda kutoka Alcolu na Manning walirudi nyuma kusimulia walichokishuhudia.

Hata hivyo mnamo mwaka 2004, uchunguzi ulianza tena kuhusu Kesi ya Stinney. Baadhi ya watu na Chuo Kikuu cha Sheria cha Northeastern walianza upya kuitazama kesi hiyo.

Hatimaye mwaka 2014 ikiwa ni miaka 70 baadaye mahakama ilisema namna mashtaka yake yalivyoendeshwa hayakufuata misingi ya haki ya uendeshaji wa shtaka hilo. Uchunguzi uligundua kuwa wale watoto waliuliwa kwa kupigwa na kitu chenye uzito mkubwa, ambao mtu mwenye miaka ya Stinney Jr asingeweza kukinyanyua.

Tukio lenyewe lilikuwa hivi, baada ya kutoka shule Machi 24, 1944 wasichana wadogo wawili wenye asili ya kizungu huko Alcolu, South Carolina walikuwa wakicheza nje ya kiwanda cha mbao ambako wazazi wao walikuwa wakifanya kazi. Watoto hao walikuwa wakichezea baiskeli na mipango yao ya kutafuta matunda na maua mazuri.

Watoto hao Betty June Binnicker aliyekuwa na umri wa miaka 11 alikuwa akiifuata reli akiwana rafiki yake mwenye umri wa miaka 7 Mary Emma Thames. Baada ya kupita kiwanda cha mbao walikutana na watoto wawili wenye asili ya Kiafrika, George Stinney Jr aliyekuwa darasa la saba na mdogo wake Amie ambao walikuwa wakichunga ng’ombe.

Kiufupi ni kwamba walikuwa majirani na walikuwa na mazoea ya kucheza pamoja. Hukumu ya Stinney Jr. inasalia kuwa hukumu ya binadamu mdogo zaidi duniani katika karne ya 20 kuwahi kuhukumiwa kifo akiwa na umri wa miaka 14.

Inadaiwa wakati huo mahakama na jeshi la polisi wote walikuwa ni wazungu kutokana na ubaguzi dhidi ya watu weusi. Miili ya watoto hao ilipatikana pori moja lililokuwa likimilikiwa na Mmarekani mweupe sio mbali sana na George Stinney Jr. alishtumiwa kwa mauaji hayo.

Kesi yake ilidumu kwa saa mbili baada ya kutiwa mikononi mwa polisi, na kupelekwa mahakamani kwa kushtakiwa muda huo huo, na kuhukumiwa kifo.

George alipelekwa Gereza la mbali ,yapata km 80, toka mji aliokuwa akiishi wa Alcolu huko South Carolina. Wakati akisubiri siku ya kifo chake hakuwaona wazazi wake wala mwanasheria,na muda wote alionekana akiwa ameshika Bibilia. 

0 Comments:

Post a Comment