Historia ni somo kuhusu maisha ya binadamu na
utamaduni wao wakati uliopita. Mara nyingi neno historia pia lina maana ya
maarifa yoyote kuhusu wakati uliopita, yawe au yasiwe maarifa ya watu (kwa
mfano "historia ya ulimwengu").
Wanahistoria wanapata maarifa yao kutoka maandishi ya
zamani (hasa kwa Historia andishi), kutoka fasihi simulizi na kutoka akiolojia
(hasa kwa Historia ya awali).
Kwa mfano historia ya neno Kilimanjaro; Umaarufu wa
jina hili umetokana na mlima mrefu uliosimama pekee unaoitwa Mlima Kilimanjaro,
upatikanao kaskazini mwa Tanzania.
Asili ya neno hili ni makosa ya kisarufi yaliyofanywa
na wageni kutoka ng'ambo ambao waliwasili eneo hilo karne ya 18 na kuwakuta
wazawa wakiishi maeneo hayo kuuzunguka
mlima huo.
Inasemekana kuwa wazawa wa eneo hilo yaani wachaga
waliuita mlima huo 'kilimakyarooo', wakimaanisha kilima kirefu.
Lakini kutokana na kushindwa kutamka hilo neno
'wazungu' walitamka kwa namna yao na kuuita huo mlima Kilimanjaro, ambalo ndilo
neno litumikalo hadi hivi sasa kutokana na kwamba wao waliweza kuhifadhi hilo
jina kwa njia ya maandishi na kulitangaza kote duniani.
Neno ‘Kilimanjaro limetumika pia kuutaja mkoa wa
Kilimanjaro ambao una wilaya zipatazo saba za Same, Mwanga, Rombo, Moshi
Vijijini, Moshi Mjini, Hai na Siha
Katika makala haya tutaangazia mji wa Moshi, sababu ya
kuitwa jina hilo.
Mji wa Moshi ulianzia katika eneo la Old Moshi,
Tsudunyi upande wa milimani ambako sehemu hiyo ilikuwa ikiitwa Moshi hapo
kabla.
Wakati wa ujio wa wageni mbalimbali kutoka nje ya bara
la Afrika katika ardhi ya Uchagani miaka
ya katikati ya karne 19 kwa ajili ya kufanya biashara na upelelezi wa
upatikanaji wa mali ghafi walikutana na jamii zenye nguvu.
Wakitokea maeneo Ya Pwani, Ulaya, Asia na Uarabuni
waliikuta Old Moshi ukiwa ndio mji mkubwa zaidi kibiashara katika ardhi ya
uchagani ikiwa mikononi mwa kiongozi shupavu Mangi Mkuu Rindi Makindara.
Mangi Mkuu aliingia mikataba mbalimbali ya kibiashara
na mahusiano ya kidiplomasia na serikali za Waingereza, Wajerumani na hata
Zanzibar.
Baada ya Mangi Rindi Mandara Kufariki, Wajerumani
ambao walikuwa wameshajipanga walibadilika na kuanza kuwa wababe wakati huo
Gavana wa Wajerumani Kilimanjaro akiwa Dkt. Karl Peters na walijenga kituo cha
kijeshi Old Moshi, hiyo ikiwa ni mwishoni mwa mwaka 1891.
Huo ndio ukawa mwanzo wa utawala wao Kilimanjaro. Hata
hivyo Umangi wa Old Moshi ulikuwa umerithiwa na Mangi Meli Mandara mtoto wa
Mangi Rindi Mandara ambaye alikuwa jeuri na mwenye kujiamini sana na hakutaka
kuwa chini ya utawala wa Wajerumani.
Mangi Meli hivyo hakukuwa na maelewano mazuri kati
yake na Wajerumani na hata watu wa Old Moshi kwa ujumla walikuwa wajeuri sana
dhidi ya ubabe wa wajerumani.
Wakati huo huo Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu
aliimarisha mahusiano yake na Dr. Karl Peters kiasi cha kumzawadia binti mrembo
aliyeitwa Ndekocha.
Kitendo hicho kilimfanya Dkt. Karl Peters ahamishe Ofisi za Utawala za
Wajerumani Kilimanjaro Kutoka Old Moshi, Tsudunyi hadi Marangu, Lyamrakana
mnamo mwaka 1892.
Lakini Karl Peters alifanya ukatili mwingi sana pamoja
na mauaji katika ardhi ya Uchagani hususan Marangu kiasi cha kuimarisha sana
ulinzi wake binafsi na hakuchukua muda mrefu aliondoka Kilimanjaro.
Gavana mpya Aliyekuja Kilimanjaro Von Bulow hakuwa na
maelewano hata na Mangi Ndegoruo Marealle mwenyewe licha ya kuishi Marangu na
alitumia mabavu kujaribu kulazimisha kila kitu.
Ubabe wake ulipelekea Von Bulow kuingia katika mzozo
na Mangi Meli, wakati huo ofisi za utawala wa Wajerumani zikiwa Marangu
alikozihamishia Karl Peters.
Von Bulow aliamua kuivamia tena Old Moshi kupambana na
Mangi Meli ambaye alionekana ni jeuri sana na asiyetishika.
Von Bulow alikusanya majeshi yake pamoja na askari
mamluki wa Kinubi kutoka Sudan na wengine wa Kizulu kutoka Afrika Kusini.
Mashushushu wa Mangi Meli Walikuwa Makini Kufuatilia
nyendo zao na mnamo Juni mwaka 1892, waliivamia old moshi.
Jeshi imara la Mangi meli lililojumuisha askari kutoka
Old Moshi, Uru na Kilema walijibu mapigo kwa ustadi mkubwa na askari wa Von
Bulow waliuawa kwa wingi sana na kuzidiwa.
Von Bulow alikimbia lakini alitafutwa na askari wa
Mangi Meli akapatikana akiwa amejificha huko Kahe naye akauawa huko huko.
Baada ya Von Bulow kuuawa Wajerumani wote Kilimanjaro
walikimbia na hawakuthubutu kurudi Kilimanjaro kwa karibu mwaka na nusu, mpaka
waliposhawishiwa sana kurudi na taasisi za kidini.
Baada ya kushawishiwa sana, Wajerumani walirudi
Kilimanjaro mwaka 1893 mwishoni wakiwa na silaha nzuri za kisasa kwa wakati huo
za kivita na jeshi imara sana kupambana na majeshi ya Wachaga.
Waliingia Old Moshi usiku na kufanya mashambulizi ya
kushtukiza kwenye ngome ya Mangi meli.
Vita ilipiganwa siku mbili usiku na mchana na Mangi
Meli na majeshi yake walizidiwa na kuamua kujisalimisha ili kuepusha mauaji
zaidi.
Mangi Meli alipewa masharti ya kutoa malighafi na
nguvu kazi ya kutosha kujenga kituo kipya cha kijeshi cha Wajerumani Old Moshi
na Ofisi za utawala wa Wajerumani.
Baada ya vita ya pili kati ya Wachaga na Wajerumani
gavana mpya wa wajerumani kilimanjaro kapteni Johannes aliamua kurudisha Old
Moshi ofisi za utawala wa wajerumani kilimanjaro ambazo Karl Peters alikuwa
amezihamishia Marangu.
Kapteni Johannes alizirudisha lli aweze kuidhibiti Old
Moshi. Hapo ndipo mji wa Moshi ukarudi upya eneo hilo la Tsudunyi na Ofisi za
Utawala Kilimanjaro kuanzia Mwaka 1893 - 1919.
Mwaka 1912 reli lliyokuwa inajengwa ikitokea Tanga
Kuelekea Kilimanjaro ilifika katika tambarare za Moshi na taratibu ukaanza mji
mpya ambao uliitwa "The New Moshi" Yaani Mji Mpya wa Moshi kwasababu
mji wa Moshi wenyewe ulikuwa kule mlimani.
Mwaka 1919 Ofisi za Utawala Kilimanjaro pamoja na
taasisi zake kama Hospitali Ya Mawenzi, Mahakama n.k. vilivyokuwa Old Moshi,
zilihamishiwa huku chini kwenye tambarare ambapo palikuwa bado ni mapori na
hakuna hali nzuri sana ya hewa.
Baadaye ule mji kule juu mlimani ukapewa jina jipya
"The Old Moshi" na Mpaka Leo panaitwa Old Moshi. Majengo yaliyokuwa
ofisi za utawala kule Old Moshi sasa hivi ndio Majengo ya Halmashauri ya Wilaya
Ya Moshi Vijijini.
0 Comments:
Post a Comment