Saturday, June 6, 2020

Martin Palermo na rekodi ya kustaajabisha ya kukosa penati nyingi katika mchezo mmoja


Mwananadharia wa Ujerumani Albert Einstein (1879-1955) ambaye anachukuliwa kuwa ni miongoni mwa watu wenye akili waliowahi kuwapo katika karne ya 20 aliwahi kusema, ugonjwa wa akili (kichaa) ni pale ambapo unarudia makosa yale yale kwa kitendo kile ukitarajia kupata matokeo tofauti.

Nukuu hiyo ilikuja kutumiwa na Jimmy Kinnon (1911-1985) mwandishi maarufu wa masuala ya dawa za kulevya na mwanzilishi wa Jamii ya Watu walioathirika kwa dawa za kulevya ya Narcotics Annonymous (NA) mnamo mwaka 1981 miaka minne kabla ya kufariki kwake.

Kiuhalisi Kinnon alikuwa akiwafafanulia wanachama wenzake kuwa kuendelea kutumia dawa za kulevya kisha kuwa na matarajio ya siku moja itatokea ukaacha huko ni kujidanganya na hapo ndipo tafsiri ya ugonjwa wa akili inapokuja kwa mujibu wa msomi na mwananadharia Einstein.  

Katika kuchukua nukuu hizo Einstein alimwelewa sana mwanzilishi wa majimbo katika taifa la Marekani Benjamin Franklin (1706-1790) ambaye alisisitiza katika nukuu zake kuhusu ukichaa, “Ukichaa ni kufanya jambo hilo, tena na tena zaidi, lakini ukitarajia matokeo tofauti.”

Nimeyasema hayo kwa kuanza ili kukupeleka katika tukio moja ambalo nafikiri itachukua miaka 300 kwa rekodi hiyo kuvunjwa. Tumekuwa na msemo unaovutia kwelikweli kwamba “rekodi zimewekwa ili zivunjwe” lakini kwa hii ya Martin Palermo hakika itakuwa gumzo siku ambayo mchezaji atavunja.

ILIKUWAJE KWA MARTIN PALERMO? 


Katika muda wa majeruhi, nyota wa soka wa Argentina wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, Martin Palermo aliweka mpira wake katika alama ya kupigia mkwaju wa penati kisha akajiandaa na kurudi nyuma mita kadhaa akiwa na hakika ya kuipatia timu yake ya taifa, mpira uligonga mtambaa panya na kutoka nje.

Dakika tano baadaye Argentina iliendelea kupeleka mashambulizi dhidi ya Colombia, mpira ukamiminwa kama unataka kutoka nje, Palermo aliruka juu akijiandaa kuukung’uta mkwaju, mlinzi wa Colombia Alexander Viveros alipaniki na kuuokoa mpira ule kwa mkono Argentina wakapata mkwaju wa penati.

Palermo kama kawaida akaenda kuuweka kwenye alama ya kupigia mkwaju wa penati. Kwa mguu wa kushoto kisha alijivuta nyuma hatua kadhaa na kuufumua mkwaju ule hatimaye uliishia kugonga mtambaa wa panya au besela kwa wale wenzangu na kisha kutoka nje ya uwanja ambako ulikwenda kugonga puto au pulizo lililokuwa nyuma ya lango.

Wakati huo Kocha wa Argentina alikuwa Marco Bielsa ambaye hakuvutiwa na kitendo cha Palermo ambaye alikuwa akikimbia kiunyonge.

Katika akili yake Bielsa alikuwa akifikiri kijana wake atajirekebisha akipata fursa nyingine ya kufunga.

Dakika 10 baadaye mchezaji wa Colombia Arley Bentancourt aliisukuma safu ya ulinzi ya Argentina ndani ya eneo la hatari na Bentancourt akaanguka na Colombia wakapata mkwaju wa penati ambao Ivan Cordoba aling’ang’ania kupiga licha ya kwamba Hamilton Ricard naye alikuwa anataka.

Mlinda mlango wa Argentina siku hiyo alikuwa German Burgos ambaye alishindwa kuzuia mkwaju huo na kutinga wavuni.

Colombia nzima ilishangilia na Cordoba alivua jezi yake Na. 2 mgongoni na kuipeperusha hewani juu. Mwamuzi Ubaldo Aquino akapuliza kipenga cha mapumziko, Argentina 0-1 Colombia.

Kifupi ni kwamba mechi hiyo ilikuwa inachezwa ikiwa ni karibu kumbukizi ya tano ya kuuawa kwa Andres Escobar.

Zikiwa zimebaki dakika 20 kumalizika kwa mchezo huo Colombia wakiwa mbele dhidi ya Argentina, Javier Zanetti alimtandika kiwiko Rubiel Quintana na kuonyeshwa kadi nyekundu, Zanetti kwa huzuni alitoka nje ya uwanja.

Dakika 15 zikiwa zimesalia wakati huo Juan Roman Riquelme alimiminina mpira upande wa pili ambao alikuwapo Palermo.

Naye bila hiyana akaruka kichwa, kwa mara nyingine tena Viveros akaingia mzima mzima ndani ya eneo la hatari, Argentina wakapata mkwaju wa penati.

Palermo akachukua tena mpira ule kwa ajili ya mkwaju wa penati. Mtangazaji wa kwenye runinga wa Argentina aliyefahamika kwa jina la Marcelo Araujo alisikika akimhamasisha Palermo kwa nguvu kubwa, “Vamos Martin, vamos….” Yaani kwa taarifa yako, mpira ule ulipita juu ya mtambaa wa panya ingekuwa Tanzania tungesema “mpira ule umeonekana huko Mtoni kwa Azizi Ali, Dar es Salaam.”

Palermo alivuta bukta yake katika muundo wa V hadi kifuani mwake, huku akitoa sauti. Mtangazaji wangu wa TV Mr. Araujo alikaririwa akiwaambia watazamaji wake, “Hapana, ni Mungu tafadhali, inawezekanaje kuwa hivyo?”

Kocha Bielsa hakuelewa nini kimetokea alishtukia yupo kwenye vyumba vya kubadilisha baada ya mwamuzi kumtoa kwenye benchi la ufundi kutokana na utovu wa nidhamu. Huo ulikuwa mkwaju wa pili.

Kabla ya kupata mkwaju wa tatu wa penati Los Cafeteros alipata mabao mawili kupitia kwa Edwin Congo na nyota aliyetokea benchi Johnnier Montano.

Wakati muda ukikaribia kumalizika katika mchezo huo Palermo aliangushwa katika eneo la hatari na mkwaju wa tatu Argentina wakampa tena Palermo apige, kwa taarifa yako mkwaju wake uliokolewa na mlinda mlango wa Colombia tungesema alimpelekea mikononi. Ooooooops! Argentina 0-3 Colombia.

Ulikuwa na mchezo wa hatua ya makundi ya Copa America 1999 uliochezwa katika Uwanja wa Feliciano Cáceres mjini Luque. Mchezo huo ulichezwa Julai 1, 1999.

Katika mchezo wa ufunguzi wa kundi C Argentina iliizabua Ecuador mabao 3-1 Diego Simeone alifunga katika dakika ya 12 na Palermo alitupia mawili katika dakika ya 55, 61. 

Baada ya kukosa penati tatu dhidi ya Colombia Palermo alicheza tena katika mchezo uliofuata wa makundi dhidi ya Uruguay na kuifungia bao Argentina katika ushindi wa mabao 2-0.

Argentina iliishia robo fainali ya michuano hiyo baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 na Brazil walioibuka mabingwa wa Copa America 1999. Palermo ana rekodi nyingine ya kuhudumu na mataifa mawili Hispania na Argentina akifunga mabao 249 katika mechi 592.

Argentina alihudumu mechi 15 tu na kuifungia mabao 9 kutoka mwaka 1999 hadi 2010. Klabu mbalimbali aliwahi kuzitumikia ikiwamo Villareal, Real Betis, Boca Juniors. Alizaliwa Novemba 7, 1973 huko La Plata, Argentina ambapo kipaji chake cha soka kilionekana Estudiantes de La Plata na baadaye akapelekwa Boca Juniors.

Palermo anasalia kuwamo katika rekodi ambazo ni vigumu kuvunjika kirahisi, hoja ni nyepesi tu nani atakuachia ukose penati mbili mfululizo kwa mpira wa kisasa kama huu wa kizazi chetu na ndio sababu nasisitiza kuwa rekodi ya Palermo kukosa mikwaju mitatu ya penati itachukua miaka 300 mchezaji kuivunja.

0 Comments:

Post a Comment