Monday, June 22, 2020

Anthony Komu amhofia mgombea CCM

Mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyetangaza kuhamia NCCR-Mageuzi Machi mwaka huu baada ya Bunge kumalizika Anthony Komu ameonyesha wasiwasi mkubwa dhidi ya mgombea anayeonekana kutajwa kuwania jimbo hilo wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) Deogratius Mushi.

Komu alitangaza kuhamia NCCR-Mageuzi baada ya bunge ambalo limevunjwa Juni 16 mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli mnamo Machi 29, mwaka huu kutokana na kauli za kejeli, kashfa na kukiuka maagizo ya Chadema.

Akizungumza na Tanzania Daima Komu alisema kinachomtisha ni kwamba endapo Mushi wataamua kumpitisha itampa kazi kubwa kumshinda kutokana na kwamba aliwahi kuwapo upinzani kabla ya kurudi CCM.

Komu alisema katika uchaguzi kuna masuala muhimu ya kuangazia ikiwamo aina ya mgombea unayekutana naye na ili kupata uungwaji mkono ni lazima umjue kwa kina zaidi na uwezo  wake na wako.

“ Jambo la msingi katika siasa ni rasilimali na aina ya mgombea unayekutana naye, kila mgombea ana namna yake ya kupambana hivyo lazima umwangalie bila hivyo ndio sababu unaona mgombea huyu anaungwa mkono zaidi kuliko huyu,pia ajenda za chama huwa zinaonyesha dira,” alisema Komu.

Aidha Komu alisema mustakabali wake ndani ya NCCR-Mageuzi sio mbaya kwani yeye alikuwapo tangu hapo awali kabla hajahamia Chadema na kwamba kinachosubiriwa ni kukabidhiwa  kadi ya uanachama ambayo watampa ile ile ya kwanza.

Mbali na hilo Komu alisema kumekuwa na utamaduni ambao sio mzuri kwa wachapakazi wa taifa hilo kuwekwa pembeni wakiwamo wenyeviti wa vitongoji, vijiji na madiwani hali ambayo imekuwa ikiongeza wimbi la watu kutoa na kupokea rushwa.

Mushi aliyekuwa diwani wa kata ya Kibosho Magharibi katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini kwa tiketi ya Chadema, alijiuzuru nafasi hiyo na vyeo vyote alivyowahi kuwa navyo ndani ya chama hicho mnamo Aprili 27, 2019 na kuhamia CCM na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuchaguliwa ndani ya chama kupeperusha bendera katika jimbo la Moshi Vijijini.


0 Comments:

Post a Comment