Thursday, November 14, 2019

SBL yaunga mkono mapambano dhidi ya ajali za barabarani Kilimanjaro


Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), imetoa vifaa mbalimbali vya usalama barabarani pamoja na elimu kwa madereva wa mabasi na waendashaji wa bodaboda na bajaji mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, ukiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kupambana na ajali za barabarani.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa kampeni kwa nchi nzima kwa SBL kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara  hususani madereva inayojulikana kama ‘Usitumie Kilevi na Kuendesha  Chombo cha Moto’ inayohamasisha madereva kuepuka kuendesha vyombo vya moto wanapokuwa wametumia kilevi.

Akizungumza na Kipindi cha Kili Breakfast cha Redio Kili FM mkoani Kilimanjaro Novemba 14, 2019 Mkurugenzi wa Mahusiano wa SBL John Wanyancha alisema utoaji wa vifaa vya usalama barabarani kama stika, vipeperushi vyenye ujumbe wa usalama barabarani na program za elimu kupitia vyombo vya habari umekuja mwishoni mwa mwaka ili kuhakikisha sikukuu zilizopo zinamalizika kwa Amani kwani ajali zilizo nyingi zimekuwa zikitokana na madereva kushindwa kujizuia kunywa pombe.

“Tunapoelekea msimu wa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, kampuni ya SBL inapenda kuwakumbusha wateja wake na umma kwa ujumala kusherekea sikukuu zinazokuja kistaarabu kwa kuhakikisha wanapoendesha wasiwe wametumia vileo hivyo,” alisema Wanyancha.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Kilimanjaro Zauda Mohamed aliwaonya madereva na watumiaji wengine wa barabara kuacha tabia ya kutumia vileo hivyo pasipo kufikiri  kwani wao wapo katika kusimamia sheria, atakutwa amezidisha kiwango cha unywaji wa pombe atawajibishwa.

“Kifungu cha 49 sura ya 168 ya sheria za usalama barabarani kinaweka wazi kuwa unywaji wa pombe unatakiwa usizidi kuliko kiwango cha 0.80BAC/100mls (Blooc Alcohol Concentration), kwa wenye vyombo vya abiria hawaruhusiwi kabisa kutumia kilevi chochote,” alisema RTO Zauda.

Hata hivyo RTO Zauda alisisitiza usalama na kwamba jeshi la polisi halitamani kuona uharibifu wa mali, majeruhi au watu kupoteza kutokana na ajali zinazotokana na utumiaji wa pombe usio wa kistaarabu.

Aidha Madereva wa vyombo vya usafiri kwa nyakati tofauti wamesema elimu juu ya usalama barabarani unapotolewa kila wati unasaidia kupunguza tatizo ukilinganisha na matumizi ya nguvu ambazo hatimaye huwa zinasababisha uhasama baina ya jeshi la Polisi na madereva.

STORY BY: Jabir Johnson
PHOTO BY: Burton Graphics
DATE: Novemba 14, 2019

0 Comments:

Post a Comment