Tuesday, November 26, 2019

Uzinduzi wa Kitabu "My Life, My Purpose" cha Mkapa


Novemba 12, 2019 Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamini William Mkapa alizindua kitabu cha yake binafsi chenye jina la “My Life, My Purpose”

Sherehe za Uzinduzi huo zilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere ( JNICC) Jijini Dar-es-Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli (JPM).

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa kitabu hicho Rais Magufuli alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kumpa afya njema na umri mrefu na baraka nyingi Rais Mkapa ambaye ni aliweza kumuunga mkono sana katika uongozi wake tokea akigombea nafasi ya Ubunge ya Jimbo Biharamulo Mashariki ambalo hivi sasa ni Jimbo la Chato wakati Mzee Mkapa akigombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Magufuli alieleza historia fupi ya nafasi aliyomteua mara tu baada ya uchaguzi huo wa mwaka 1995 ambapo Rais Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi chini ya Mama Anna Abdalla.

Magufuli alieleza jinsi alivyojifunza mambo mbali mbali kutoka kwa Rais Mkapa kwa kueleza kuwa viongozi wote mbele ya Rais Mkapa wakati wa uonmgozi wake walikuwa na haki sawa sambamba na kuwaunga mkono katika kazi zao, zikiwemo kazi alizozifanya pamoja na uwamuzi wa Rais Mkapa katika shughuli zake za kazi hasa katika ujenzi wa barabara pamoja na madaraja hapa nchini.alifanya jitihada kubwa za kuondoa Umasikini,

Alieleza mafanikio ya Rais mstaafu Mkapa ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mkakati wa Kuondoa Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Mali na Biashara Tanzania (MKURABITA), Mradi wa (TASAF), Kuimarisha huduma za jamii zikiwemo elimu na kuongoza idadi ya wanafunzi wa skuli za msingi sambamba na kuendelea kutunza amani na umoja wa Watanzania.

Alieleza kuwa Watanzania wengi na watu mbali mbali duniani kupitia kitabu hicho watamfahamu Mzee Mkapa pamoja na kuifahamu vyema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Magufuli alieleza jinsi Mzee Mkapa alivyogusia suala zima la imani katika kitabu chake hicho jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Mzee Mkapa ni kiongozi MchaMungu.

Alieleza kuwa kutokana na nidhamu na uwajibikaji wake Rais mstaafu Mkapa aliweza kupata nafasi mbali mbali za uongozi ndani na nje ya Tanzania na hatimae kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa hata baada ya kustaafu nafasi yake ya Urais, Rais mstaafu Mkapa ameendelea kuisaidia Tanzania na nchi nyengine nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kujenga utawala bora katika bara la Afrika pamoja na kusimamia amani na kuwa msuluhishi.
Marais wa Tanzania kutoka kushoto Benjamin William Mkapa, John Pombe Magufuli, Jakaya Kikwete, Ali Hassan Mwinyi na Mohammed Shein wa SMZ

Kitabu hicho kinaeleza historia ya Rais mstaafu Mkapa kuanzia alipozaliwa, safari yake ya masomo, safari ya kisiasa ikiwemo uongozi wa nchi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005 na pia, mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa na Kimataifa katika masuala ya uongozi.
Aliitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya Uongozi na kutoa wito wa kukifanyia tafsiri ya lugha ya Kiswahili kitabu hicho.

Aliwahimiza viongozi wastaafu wengine kuiga hatua za Mzee Mkapa kwa kuandika vitabu vya maisha yao na kupiongeza hatua zinazoendelea za kuandika kitabu cha Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu Mzee Jakaya Mrisho Kikwete.

Alihamasisha Taasisi hiyo ya uongozi kwa kuendeleza historia za viongozi na kuwasisitiza Watanzania kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu huku akitoa wito kwa Watanzania kuendeleza umoja na mshikamamo wao na wasikubali kuyumbishwa na badala yake washirikiane katika kuijenga Tanzania ili izidi kuleta maendeleo .

Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa alizundua kitabu hicho katika siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake Novemba 12 na pia siku ambayo alikuwa akitimiza umri wa miaka 81 alitoa shukurani kwa wale wote waliomuunga mkono katika kutayarisha kitabu hicho huku akimuelezea Rais Julius Kambarage Nyerere kwa jinsi alivyojifunza mambo mengi kutoka kwake.

Alieleza kuwa katika kitabu chake hicho amemuelezea Mwalimu Nyerere kwa mtazamo wake kama anavyomjua jambo ambalo limempa faraja kubwa sana. Na kueleza kuwa kitabu hicho kitawasaidia wanafunzi na viongozi pamoja na vizazi vijavyo.

Mapema Profesa Joseph Semboja Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi alitoa maelezo mafupi ya Mradi wa Tawasifu na kueleza kuwa taasisi yake iliyoanzishwa mwaka 2010 ndio iliyokuwa na jukumu la kutayarisha kitabu hicho na kumuunga mkono.

Alieleza kuwa hivi karibuni Taasisi hiyo itatoa kitabu cha Maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na kuongeza kuwa viongozi wengi wakiwemo wa nchi za Magharibi wamekuwa na utamaduni wa kuandika vitabu vya historia ya maisha yao na kutoa shukurani kwa viongozi hao ambao hufanya hivyo na watu kupata kuvisoma na kuwasaidia

Kwa bahati mbaya Profesa Semboja alieleza kuwa viongozi wengi wa Bara la Afrika hawapati nafasi ya kuandika vitabu vyao kutokana na mazingira yao na badala yake hujifunza maandishi kutoka kwa nchi nyengine wanazoandika vitabu kama hivyo.

Alieleza kuwa historia ya kiongozi katika bara la Afrika si historia yake binafsi bali ni historia ya nchi nzima na kueleza kuwa Mzee Mkapa ameandika historia ya nchi na sio historia yake binafsi na ndio maana uzinduzi wake umejumuisha makundi mbali mbali na tukio hilo si la kifamilia bali ni la Kitaifa.

Aliongeza kuwa mwaka 2016 mchakato wa kuandika kitabu hicho ulianza na kutoa shukurani kwa watu walioshiriki kwa namna moja ama nyengine kufanikisha kitabu hicho.

Jumla ya TZS Milioni 230 sawa na Dola za Kimarekani laki Moja zimetumika ambapo gharama hizo sio kubwa ikilinganishwa na gharama za vitabu vinavyochapishwa na viongozi wengine katika nchi nyingi duniani wakiwemo viongozi wastaafu wa Marekani.

Nae Profesa Rwekaza Mukandala Mgoda wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitoa uchambuzi wa Kitabu hicho cha Rais Mkapa ambacho kina Sura 16 na kurasa 320 pamoja na utangulizi uliotayarishwa na Rais mstaafu wa Msumbiji Rais Chisano.


0 Comments:

Post a Comment