Kulikuwa na watoto wawili Shija na Mabula, walioishi na wazazi wao mjini Shinyanga. Shija alikuwa anasoma darasa la tatu na Mabula anasoma darasa la nne.
Shija akitoka shule husaidia kazi za nyumbani. Mabula yeye hakupenda kurudi nyumbani mapema. Alizurura mitaani na watoto wengine akiuza pipi na karanga.
Marafiki wa Mabula walimshawishi aache shule ili auze pipi na karanga. Akawa anatoroka shule ili azurure na wenzake. Mwalimu aliwaeleza wazazi wake tabia hii. Wakamuonya mtoto wao, lakini hakusikia.
Kila siku aliaga kuwa anakwenda shule, lakini alikuwa hafiki shuleni. Siku moja Mabula alitoroka tena na kujiunga na wenzake. Safari hii walikwenda kwenye kituo cha mabasi yaendayo Mwanza, Kahama na Nzega na kuendelea kuuza karanga. Hatimaye Mabula aliacha kabisa kwenda shule.
Baba yao aliwaita Shija na Mabula akamwambia Mabula, "Tumekuonya mara nyingi lakini hutaki kusikia. Wewe unataka kuwa kama punda wa dobi?."
Shija akauliza, "Baba, kwani punda wa dobi alifanya nini?" Baba akaanza kuwaeleza kisa cha dobi na punda wake.
Dobi alimtesa sana punda kwa kumpa chakula kidogo na kumfanyisha kazi nyingi sana. Siku moja punda akakimbilia porini akatafuta sehemu yenye majani mazuri, akaishi huko.
Akanenepa na kupendeza sana. Karibu na pale alipokuwa anaishi punda wa dobi, palikuwa na Simba mmoja mzee aliyedhoofu sana kwa ugonjwa. Sungura aliishi na Simba yule akimuuguza.
Siku moja Simba akamwambia Sungura Sungura, "Nataka kula nyama lakini sina nguvu za kwenda kuwinda. Tafadhali nenda kanitafutie nyama".
Sungura akakubali. Sungura alizunguka akakutana na punda wa dobi. Alimwona alivyonenepa na kupendeza, akamwambia, "Simba amenituma nije nikuite. Amesikia kuwa wewe ni mnyama mwenye sura nzuri sana. Anataka uende kwake akakuone"
Punda wa dobi akakubali wakaenda. Walipofika walimkuta Simba amekaa nje. Simba alipomwona punda wa dobi alivyonenepa, akataka amkamate.
Punda wa dobi aliogopa sana. Akarusha mateke kwa nguvu. Simba akaanguka chini na punda wa dobi akakimbia na kurudi kwake. Alijeruhiwa kidogo na makucha ya Simba. Sungura hakutaka rafiki yake afe kwa njaa.
Kesho yake, akaenda tena kwa punda wa dobi. alimdanganya kjuwa Simba alitaka kuona uzuri wake.
Akamweleza kuwa Simba hatamjeruhi tena kwa makucha yake. Sungura akasema," Jana alipokurukia ilikuwa ni furaha ya kukuona." Punda wa Dobi akamwambia Sungura , "Lakini leo Simba akinikwaruzwa kwa makucha yake, nitakupiga mateke ufe."
Sungura na Punda wa Dobi wakaondoka, wakaenda kwa Simba. Walipofika, Simba akamrukia Punda wa Dobi na kumtia makucha shingoni.
Punda wa Dobi akaanguka chini Simba akamwua, akapata nyama. Baba alipomaliza hadithi hii, Mabula alikuwa anatetemeka kwa hofu. Baba yake akamwambia, "Mwanangu usipobadili tabia yako, siku moja utafungwa jela.
Hao marafiki zako wanakudanganya kama Sungura alivyomdanganya Punda wa Dobi." Tangu siku hiyo Mabula alikwenda shule akaacha kuzurura na kuuza pipu na karanga.
0 Comments:
Post a Comment