Tuesday, November 12, 2019

Namna ofisi ya kata Soweto Moshi ilivyochomwa moto


Novemba  10, mwaka huu wamechoma moto ofisi ya Mtendaji Kata ya Soweto Manispaa ya Moshi  mkoani Kilimanjaro na kusababisha hasara  mbalimbali zikiwemo nyaraka za serikali na thamani za ofisi kuungua moto.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira amesema  kuwa kati ya saa 7:30 hadi saa 8 usiku wa kuamkia  Novemba 10 mwaka huu, katika mtaa wa Wailes Kata ya Soweto Manispaa ya Moshi watu hao wasiojulikana walivamia ofisi hiyo na kuichoma moto kwa kutumia mafuta ya petrol.

“Watu wasiofahamika waliichoma ofisi ya mtendaji kata ya Soweto, kwa kutumia mafuta ya petrol na kusababisha baadhi ya nyaraka za serikali na thamani za ofisi kuungua moto, baada ya moto huo kuwaka mtu mmoja ambaye yupo jirani na ofisi hiyo aliweza kusikia harufu ya mafuta na kuchungulia kwa nje ya dirisha la nyumba yake na kuona moto ukiwa unawake kwenye ofisi hiyo,  alitoa taarifa kwa askari wa doria ambao walifika na kuanza kuuzima moto huo kwa kushirikiana na wananchi,”alisema Dkt Mghwira.

Alisema katika uchunguzi wa awali moto huo uliwashwa kupitia madirisha ya mbele ya jengo hilo ambapo kuta za madirisha zinaonekana  zilimwagiwa mafuta ya petrol na kuwashwa kwa kutumia kiberiti.

Dkt. Mghwira ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, alisema watekelezaji wa uchomaji moto huo waliacha kiberiti  ambacho kilionekana kikiwa na msokoto wa bangi, ambapo moto huo uliunguza sehemu ndogo ya jengo na nyaraka zilizokuwa karibu na madirisha ziliweza kuungua zote.

“Sio nyaraka zote zimeungua moto, kama ambavyo taarifa zinatolewa kwenye mitandao ya kijamii, nyaraka zilizoungua ni zile ambazo zilikuwa karibu na moto ulipoanzia,  na nyaraka nyingi ambazo zimeungua ni taarifa mbalimbali za chanjo, machapisho na makablasha mbalimbali yaliyokuwa na taarifa za afya,”alisema.

Aidha alisema serikali imepoteza kumbukumbu zote za taarifa za afya katika kata ya Soweto, huku akiwataka vijana na makundi mengine kujiepusha na vitendo vya kihalifu, viashiria vyovyote  wakati wote kwani sheria itawachukulia hatua dhidi yao.

“Naviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwa macho na vitendo vyovyote vya uhalifu vyenye kuvuruga amani na usalama wa  nchi, ambapo pia ameliagiza jeshi la polisi kuhakikisha wanafuatilia na kuwabaini wale wote waliohusika na uchomaji moto wanapatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro Salum Hamduni, amesema amepokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na kwamba atahakikisha wanawafuatilia wahusika wote, wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria

“Tutafanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha wale wote waliohusika wanatendewa haki kwa mujibu wa sheria,”alisema.  

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Michael Mwandezi, alikiri kutokea kwa tukio hilo la uchomaji moto ofisi ya mtendaji kata na kuwataka wananchi hususan wa kata hiyo kuwa watulivu  katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

“Napenda kuwahakikisha wananchi  kwamba uchaguzi utafanyika kwa amani na uhuru,  na kwamba kuchomwa moto kwa ofisi hii hautaathiri shughuli za uchaguzi , uchaguzi utafanyika kama kawaida,  na shughuli zingine za serikali ndani ya kata hiyo vitaendelea kama kawaida,”alisema Mwandezi.

0 Comments:

Post a Comment