Friday, November 29, 2019

Wanne wafariki kwa homa ya Ini wilayani Hai, Kilimanjaro

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai Helga Mchomvu akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo Novemba 28,2019.

Halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imesema , inaendelea na mapambano dhidi ya uwepo wa ugonjwa wa homa ya ini, baada ya watu wanne kugundulika kufariki kutokana na ugonjwa huo.

Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Hai Freddy Kaduma, aliyasema hayo kwenye kikao cha baraza la madiwani wakati akijibu swali la Diwani wa kata ya Machame Uroki Robson Kimaro,  katika swali lake Kimaro alitaka kujua ni mikakati gani ambayo seriakali ya wilaya hiyo, imeichukua ili kuhakikisha inadhibiti ugonjwa wa homa ya ini ambao umekuwa tishio katika wilaya hiyo.

Kaduma alisema ugonjwa wa huo kwa sasa hivi umeanza kuwa tishio katika wilaya Hai, na kwamba halmashauri ya wilaya ya hiyo, tayari imekwishaanza kuchukua mikakati  ya kukabiliana na ugonjwa huo kwa  kuwaelimisha jamii jinsi  ya kukabiliana nao.

“Ni kweli ugonjwa huu upo katika wilaya yetu ya Hai, tayari kuwa watu kadhaa wamefariki kutokana na ugonjwa huo ambao  unaenezwa kwa njia ya ngono isiyo salama, kugusana, kujamiana  na ugonjwa huu unafafana kabisa na ugonjwa wa UKIMWI, endapo mgonjwa atabainika kuambukizwa na ugonjwa wa homa ya ini chanjo hiyo haitafanya kazi,”alisema.

Alisema serikali ya wilaya imeanza kuweka nguvu  kubwa kwa ajili ya kutoa elimu  katika jamii ili kuwaelimisha wananchi kutokana na ugonjwa huo ambao unaenea kwa kasi ili waweze  kwenda kupata chanjo mapema.
“Tayari  jambo hili tumeshaliwasisha katika ngazi ya Mkoa  ili waweze kutuletea dawa za chanjo, ili tuweze kuwachanja wananchi wote, lakini chanjo hizi zitakuwa zalipiwa na sio bure,’alisema.

Katika swali lake la msingi diwani Robson Kimaro, alisema ndani ya kata yake watu wanne wametajwa kufariki kutokana na ugonjwa huo, halmashauri imeweka nguvu gani ili kuhakikisha ugonjwa huo hauendelei kuenezwa katika maeneo mengine.

“Homa ya ini ni ugonjwa ambao umeanza kuenea kwa kasi kubwa ndani ya halmashauri ya wilaya ya Hai, na katika kata yangu watu wanne wamefariki kutokana na ugonjwa huo, serikali imechukua hatua gani katika kukabiliana na tatizo hilo?,”alihoji Kimaro.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Masama Kusini Elingaya Massawe, aliitaka halmashauri hiyo kuhakikisha kwamba idara ya afya inakwenda kufanya mikutano kwa wananchi ili kuwapata elimu ya kutosha jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias, Moshi
DATE: Novemba 28, 2019







0 Comments:

Post a Comment