Jengo la chuo cha maendeleo ya jamii, likiwa katika hatua za mwisho kukamilika. |
Serikali imetoa fedha zaidi ya Sh milioni 600 kwa
ajili ya kukarabati Chuo Cha Maendeleo ya Jamii, huku ikiwaonya watu
watakaobainika kuzitumia vibaya fedha hizo serikali haitasita kuwachukulia
hatua za kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa na
Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Senyamule, wakati alipokuwa akikabidhi fedha
hizo kwa mkuu wa chuo cha FDC ambapo
alisema kuwa mtu yeyote atakayebainika kuzitumia fedha hizo kinyume na malengo
yaliyokusudiwa atazitapika fedha hizo.
DC Senyamule alisema fedha
za serikali zinapokuja zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na
kwamba serikali haitasita kumchukulia
hatua kali za kisheria.
“Serikali Kuu imetoa
Sh milioni 647 kwa chuo cha FDC Same,
ili ziweze kutumika kwa ajili ya kukarabati majengo yote, kujenga bweni,
madarasa mawili, jengo la utawala, karakana ya magari pamoja na darasa la
wanafunzi wa shule ya awali.”alisema.
Aidha DC Senyamule, alimtaka mkuu wa chuo cha
Maendeleo ya Jamii FDC Same, kuhakikisha anasimamia kikamilifu shughuli za
ujenzi huo huku akimtaka mkandarasi huyo kumaliza kazi kwa muda uliowekwa na serikali.
"Rais Dkt. John
Magufuli anayafanya haya yote ili
wanafunzi ambazo hawakufanikiwa kuendelea na masomo ya juu waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri
ama kuajiriwa kutokana na fani ambazo mmezipata kutoka katika chuo
hiki.”alisema.
Alisema mradi wa kukuza
ujuzi na stadi za ajira ulianzishwa kwa lengo la kutekeleza vipaumbele vya
serikali vilivyoainishwa katika mkakati wa serikali wa kufikia Tanzania ya
Viwanda ifikapo 2025, lakini pia kuwezesha vijana kupata ujuzi kwa vitendo
kuliko nadharia pamoja na kujengea uwezo vyuo vya kati.
“Namshukuru sana Rais Dkt.
Magufuli kwa kuweza kutupatia wilaya ya Same fedha kwa ajili ya kukarabati chuo
hiki, kwani chuo hiki kilikuwa kimesahaulika kwa miaka mingi mno na miundombinu
ya majengo haya yalikuwa machakavu, lakini kutokana na fedha hizi sasa
matumaini mazingira ya chuo yataboreka," DC Same.
Itakumbukwa kwamba serikali
ilianzisha vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (VMW) kwa madhumuni ya kuimarisha
maarifa na stadi kwa wananchi ili waondokane na ujinga, umaskini na maradhi na
hatimaye kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
“Vyuo hivi vilianzishwa kwa
lengo la kumtayarisha mtanzania ambaye ni mtu mzima aweze kukuza utu wake na
kumfanya awe kamili katika jumuiya ya Watu wake, aweze kutumia akili zake
vizuri na kuweza kuamua mambo yake au ya
umma kwa njia iliyo sahihi, ikiwa ni pamoja na kufikia kiwango cha juu zaidi
katika ufundi wa kazi anazozifanya,”alifafanua.
Naye Mwenyekiti wa Bodi John Mwasi, ameitaka jamii
kuona umuhimu wa kuwasomesha watoto viziwi
huku pia akitoa rai kwa wale wenye uwezo kutoa fursa za ajira kwa vijana hao.
Nao baadhi ya wahitimu wa
chuo hicho katika risala yao iliyosomwa kwa niaba yao na Salim Elia, walisema wanakabiliwa na uhaba
wa walimu wa ufundi, vifaa vya ufundi
hasa useremala zikiwemo mbao za kufanyia mazoezi ya vitendo na vitambaa
kwa ushonaji.
“Tunaishukuru serikali kwa
kutuletea umeme chuoni hapa, lakini changamoto iliyopo ni kwamba tangu umeme huo uletwe haujaweza kusambazwa
kwenye mabweni na kwenye karakana ya kujifunzia hali ambayo inakuwa ngumu kwetu
kujifunza kutokana na changamoto hiyo ya umeme,”alisema.
Mwajuma Hemedi, ameomba
kuwepo kwa fursa za mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana tunaohitimu mafunzo
ya ufundi stadi kwani wanahitaji kujiajiri wenyewe kama walivyofanya baadhi ya
wenzao.
0 Comments:
Post a Comment