Saturday, November 23, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Japhet Hasunga ni nani?


Novemba 23, 1965 alizaliwa mwanasiasa wa Tanzania ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga. Huyu ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), anafahamika kwa jina la Japhet Ngailonga Hasunga.

Alichaguliwa kuwa mbunge wa Vwawa kwa uchaguzi uliofanyika mwaka 2015. Ameoa na ana familia yake na miongoni mwa vitu anavyoviamini tangu utoto wake ni kuishi maisha ya kawaida.

Hasunga alizaliwa katika kijiji cha Iyula Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Mbeya ambapo wazazi wake waliishi hapo, alilelewa hapo hapo kijijini na kukulia hapo mpaka ilipofika wakati wa kupelekwa shule

Mwanzoni mwa mwaka 1976 mpaka 1982 ndio mwaka ambao pengine ulitengeneza njia ya kusaka elimu, kwani mwaka huo ndio alipata nafasi ya kusonga mbele kwa kuwa na alama za juu zilizo mpekea kujiunga na Shule ya Sekondari ya Sangu iliyopo Mbozi, Mbeya kwa wakati huo sasa ni Songwe na huo ulikuwa ni mwaka 1982 hadi 1986 alipofanikiwa kupata cheti cha Elimu ya Sekondari (CSEE). Kuanzia mwaka 1987 mpaka 1989 ambapo alijiunga na Shule ya Sekondari ya Mzumbe na kuhitimu Kidato cha sita.

Kati ya mwaka 1992 mpaka 1995 alijiunga na chuo cha Maendeleo ya menejimenti Mzumbe (IDM) na kupata Stashahada ya Juu ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu.

Mwaka 1998 alihitimu Shahada ya juu ya Uhasibu na Ukaguzi wa Mahesabu (CPA) kutoka NBAA na kusajiliwa kama Mhasibu kamili Mwaka 2001.

Mnamo mwaka 2006 hadi 2007 Hasunga alikwenda  katika chuo cha Manejimenti cha Maastrichs nchini Uholanzi na kutunukiwa Shahada ya udhamili katika masuala ya Biashara, sera za Uchumi na mikakati.

Katika harakati za siasa Hasunga alianza akiwa katika Chama cha NCCR–Mageuzi na kuajiriwa kama mtendaji wa shughuli za chama, wakati huo chama kilikuwa katika hatua za kujiimarisha na hivyo kubahatika kuwa miongoni mwa wanachama waanzilishi wa NCCR–Mageuzi, hiyo ikiwa ni mwaka 1992 hapo bado chama kilikuwa hakijasajiliwa na hakika unapotaja mafanikio ya NCCR–Mageuzi ni lazima pia umtaje Hasunga kuwa miongoni mwa waliochangia.

Katika kipindi hicho yeye alikuwa ni Afisa Utawala wa chama, mwaka huohuo (1992) akawa miongoni mwa wanachama waanzilishi.

Wakati NCCR–Mageuzi ikipata usajili wake Machi 21, 1993 yeye alikuwa ni mtu muhimu katka ukuzi wa chama.

Mwaka 1994 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu, Mwaka 1995 alichaguwa kuwa Naibu Mkurugenzi idara ya sera na nyaraka, pia katika mwaka huohuo wa 1995 alibahatika kuwa Kaimu Naibu Katibu wa chama.

Mnamo mwaka 2001 alijiunga na Chama cha Mapinduzi. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa nafasi ya ubunge aliwakilisha Jimbo la Uchaguzi la Vwawa katika Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Mbeya kwa sasa ni mkoa wa Songwe.

Hasunga katika uchaguzi huo aliibuka kidedea kwa kumshinda mpinzani wake kwa zaidi ya kura 36,705 dhidi ya kura 35,400 za mpinzani wake kwa hiyo ilikuwa ni tofauti ya kura 1305.

0 Comments:

Post a Comment