Tuesday, November 5, 2019

Mifuko Mbadala kutoka Kenya yazua tafrani Kilimanjaro

Mwandishi wa gazeti la Jamhuri Charles Ndagula (kulia) akiwa ameshika mfuko mbadala unaozalishwa na Harsho kushoto ni Meneja wa Fedha Beatrice Muro na katikati ni Meneja wa kiwanda cha utengenezaji wa vyakula vya mifugo Harsho milling Co. Ltd, Joseph Njeru.
Wazalishaji wa Mifuko Mbadala wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kuwepo kwa shehena kubwa ya mifuko hiyo iliyo chini ya viwango ambayo imeingizwa nchini ikitokea nchi jirani ya Kenya.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Meneja wa  fedha katika Kiwanda cha kutengeneza vyakula vya mifugo Harsho milling Co. Ltd Beatrice Muro, alisema wamebaini kuwepo kwa mifuko hiyo kwenye masoko ya Kwasada, Mbuyuni, Soko la Kati, na meneo mengine.

Muro alisema “TBS wamependekeza  tuzalishe mifuko ambayo ina uzito wa GSM 70,lakini hadi sasa ukienda sokoni kuna mifuko mingi ambayo iko chini ya viwango, mifuko hiyo ipo kuanzia GSM 54 hadi 34.”alisema.

“Sisi wazalishaji wa ndani tumeitikia wito wa serikali  wa kuzalisha mifuko mbadala ya GSM 70, lakini  kwa wingi wa mifuko hii inatuumiza sana sisi wazalishaji wa ndani  ambao tunakidhi viwango ambavyo vimewekwa na serikali,”alisema Muro.

Naye Meneja wa kiwanda cha utengenezaji wa vyakula vya mifugo Harsho milling Co. Ltd, Joseph Njeru  alisema “Kama kweli serikali itasimamia uzalishaji wa mifuko ya GSM 70  hapa nchini, itakuwa ni ngumu sana wale wanaoleta kutoka Kenya  kuleta na kuiuza kwa bei ambayo tunazalisha, kwani kuna gharama za usafirishaji, mpakani watakapofika lazima watalipa kodi  ya serikali na hivyo hawataweza kuuza kwa bei hiyo ya chini,”alisema Njeri.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa soko la Mbuyuni ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema wapo baadhi ya watumishi wa serikali wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi na kuingiza mifuko mbadala iliyo chini ya viwango.

“Mimi ni mfanyabiashara wa mpakani pale Holili, huwa nakwenda kuchukua mizigo yangu na kuleta hapa sokoni Mbuyuni, lakini nataka nikuambie mwandishi, wapo baadhi ya watumishi wa serikali  kweli sio waaminifu kabisa tumekuwa tukiwashuhudia pale mpakani wanashirikiana na wafanyabiashara kutoka Kenya ambao wanazalisha mifuko hii mbadala, wanapoileta huwa wanasaidiwa  na hawa watumishi wa umma kuipitisha kwa njia za panya,”alisema.

Alisema mifuko hiyo inapofikishwa mpakani  watumishi hao hupigiwa simu, kisha huwapa maelekezo na  inapofika jioni kuna Haice za kutoka Holili hupakiza mifuko hiyo na kuipeleka Moshi mjini, na inapofikishwa Moshi inashushwa na kuwekwa kwenye matoroli na kupelekwa usiku kwenye  masoko.

Alipotafutwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira kuzungumzia hali hiyo  mkuu huyo alikiri kuingizwa kwa mifuko hiyo iliyo chini ya viwango huku akiitupia lawama TBS kwa kushindwa kudhibiti bidhaa hizo.

“Ni kweli kuna mifuko mingi sana ambayo inaingizwa, na watu hawa wanatumia njia za panya katika wilaya ya Rombo, Holili na Mwanga na mifuko hii ipo  chini ya viwango na hivi karibuni nilifanya oparesheni  kwa kushirikiana na TRA na tulifanikiwa kukamata mifuko mingi sana,”alisema Dkt. Mghwira.

Aidha Dkt Mghwira alisema katika oparesheni hiyo pia walifanikiwa kukamata bidhaa zilizoingizwa nchini kwa njia za panya ikiwemo sukari, chumvi, mafuta ya kupikia aina ya Kimbo na Korie.

Akitolea ufafanuzi  kuhusu uwepo wa mifuko mbadala isiyokuwa na ubora  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt.  Athuman Ngenya  alisema  kuwa  Juni 21, mwaka huu,  shirika hilo lilitoa muongozo kwa wazalishaji na wasambazaji wa mifuko ya kubebea bidhaa aina ya (non woven) baada ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki lililotolewa na Serikali.

“Muongozo huu ulitolewa  ili kutoathiri upatikanaji wa mifuko mbadala wakati taratibu za kuandaa kiwango cha mifuko mbadala  ambapo  wazalishaji wa mifuko hiyo mbadala (non-woven) wanapaswa kuzalisha mifuko hiyo kwa kuzingatia  uzito usiopungua GSM 70.

Alifafanua kuwa “Mifuko hiyo iwe yenye kuweza kurejeleshwa (Recyclable) iwe na anuani ya mzalishaji au nembo ya biashara (Trademark) pia iwe imethibitishwa ubora wake na Shirika la Viwango Tanzania (TBS),”alisema Dkt Ngenya.

Hata hivyo Dkt. Ngenya  alikiri kuwa “Ni kweli kwamba kumekuwa na malalamiko ya uingizwaji wa mifuko isiyokidhi viwango ambayo imekuwa ikiingia nchini kupitia njia zisizo halali  hivyo shirika  la TBS kwa kushirikiana na taasisi nyingine  za Serikali  ikiwemo Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Jeshi la Polisi zinafanya ukaguzi  wa sokoni na mipakani ili kubaini kama kuna mifuko hiyo isiyoruhusiwa,” alifafanua Dkt Ngenya.

Aliongeza kusema kuwa “Zoezi hili ni endelevu na kwa wale wanaobainika wakiingiza bidhaa hafifu sokoni hatua kali za kisheria huchukuliwa dhidi yao,”alisema.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias, Moshi

Date: Novemba 5, 2019

0 Comments:

Post a Comment