Tuesday, November 19, 2019

Mwanasiasa wa upinzani Niger atupwa jela baada ya kutoka Uhamishoni


Mwanasiasa wa upinzani nchini Niger Hama Amadou amekamatwa na kutupwa jela baada ya kurudi kutoka uhamishoni juma lililopita. 

Taarifa kutoka nchini humo jana Jumatatu zimesema mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 69 alirudi nchini humo kutoka uhamishoni kwa ajili ya kumzika mama yake aliyefariki dunia hivi karibuni. 

Amadou maarufu Phoenix alijisalimisha katika mahakama moja katika mji mkuu Niamey baada ya mazishi ya mama yake aliyezikwa mjini Filingue kilometa 180 kaskazini mwa mji mkuu wa taifa hilo. 

Alipojisalimisha katika mahakama hiyo, imeelezwa kuwa ilimpeleka jela moja kwa moja kwa kosa la biashara ya watoto. 

Mnamo Novemba mwaka 2015 alikamatwa kwa makosa kama hayo aliporudi toka nje ya nchi huku waungaji mkono wake wakisema ni mashtaka ya kupikwa. 

Katika uchaguzi wa Machi 2016 akiwa jela alipigiwa kura na kupata asilimia 17.7 nyuma ya Rais Issoufou anayeliongoza taifa hilo aliyeshinda kwa asilimia 48.4 ya kura. 

Katika kinyang’anyiro hicho aliachiwa kutoka jela kutokana na hali yake ya kiafya ambapo alikimbilia nchini Ufaransa hadi aliporudi juma lililopita. 

Machi 2017 Amadou na wengine 20 walishtakiwa kwa kujihusisha na biashara ya watoto kutoka Nigeria kupitia Benin kuingia nchini humo. 

Mnamo Agosti mwaka huu Amadou alitangazwa na chama chake cha Moden kuwa atawania nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu ujao wa Desemba 2020.

CHANZO: News24

0 Comments:

Post a Comment