Tuesday, November 19, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Abdel Fattah El Sisi ni nani?


Novemba 19, 1954 alizaliwa  mwanasiasa na mwanajeshi wa zamani wa kitengo cha Usalama wa Misri  ambaye kwa sasa ni Rais wa sita wa taifa hilo. 

Jina lake halisi ni Abdel-Fattah Said Hussein Khalil el Sisi. Mwanasiasa huyo amewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jenerali wa zamani wa Jeshi nchini Misri. Tangu Februari 10, 2019 El Sisi alishika nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika nafasi ambayo ataishika kwa mwaka mmoja. 

El Sisi alizaliwa Cairo na baada ya kujiunga na jeshi alikwenda Saudi Arabia kabla ya kujiunga na jeshi la Misri. Mnamo mwaka 1992 El Sisi alikwenda mafunzo ya kijeshi huko Watchfield, Oxfordshire nchini Uingereza. 

Mwaka 2006 alijiunga na chuo cha Kijeshi cha Marekani cha Carlisle, Pennsylvania. Baada ya kurudi alishika nyadhifa mbalimbali katika jeshi la Misri ikiwamo Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. 

Baada ya mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyomweka madaraka Mohamed Morsi, El Sisi aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali ya Morsi. Hiyo ilikuwa Agosti 12, 2012 akichukua nafasi ya Hussein Tantawi alishika nafasi hiyo enzi za utawala wa Hosni Mubarak. 

Akiwa Waziri wa Ulinzi El Sisi alihusika kwa kiasi kikubwa katika kumwondoa madarakani Morsi kwa nguvu ya kijeshi tukio ambalo lilifanyika Julai 3, 2013 baada ya maandamano makubwa ya raia wa Misri Juni 2013. 

El Sisi aliikataa katiba ya Misri mwaka 2012 na kuanzisha mfumo mwingine anaoutumia kwa sasa kuliongoza taifa hilo. Wakati wa mapinduzi hayo ya kijeshi El Sisi hakuingia mara moja aliteuliwa kiongozi wa mpito Adly Mansour ambaye aliteua baraza jipya la mawaziri. 

Baada ya uteuzi huo baraza hilo halikukaa sana kwani Udugu wa Kiislamu ulilikataa hivyo Agosti 14, 2013 polisi walizua maandamano makubwa nchini humo yaliyosababisha mamia ya watu kuuawa na maelfu kujeruhiwa hali iliyokosolewa vikali na jumuiya za kimataifa. 

Machi 26, 2014 baada ya kilio kikubwa kutoka kwa wananchi El Sisi aliamua kustaafu shughuli za kijeshi na kuingia katika mbio za kuwania urais mwaka 2014 uliofanyika Mei 26 hadi 28. 

Katika kinyang’anyiro hicho mshindani mkubwa wa El Sisi alikuwa Hamdeen Sabahi lakini hata hivyo El Sisi alipita kwa kishindo kwa asilimia 97 ya kura. 

Mnamo Juni 8, 2014 alitawazwa kuwa rais wa sita wa Misri. Baadhi ya vyombo vya habari ulimwenguni vinamtaja El Sisi kuwa dikteta na mtu mwenye nguvu wakimlinganisha na watawala wengine waliopita katika taifa hilo. 

Katika uchaguzi wa mwaka 2018 El Sisi alipata upinzani mkali baada ya kushikiliwa kijeshi kwa Luteni Jenerali Sami Anan na baadaye kutangazwa kupotea kwake, pia mwanasiasa na mwanajeshi wa zamani wa taifa hilo Ahmed Shafik kukutwa na makosa ya rushwa na video za ngono. 

Kuondolewa kwa mwanasheria na mwanaharakati Khaled Ali na Mohamed Anwar El-Sadat kulionyesha dhahiri kuwa El Sisi ni mbabe na dikteta nchini Misri.

0 Comments:

Post a Comment