Serikali ya Sudan imezindua satelaiti yake ya
kwanza kwa ajili ya kufanya utafiti wa masuala ya kijeshi, kiuchumi na
teknolojia ya anga la mbali.
Uzinduzi huo umefanyika nchini China, na
kutangazwa juzi jumanne na kiongozi wa baraza huru nchini Sudan Abdel Fattah
al-Burhan katika makao makuu ya taifa hilo Khartoum.
Al-Burhan amekaririwa akisema satelaiti hiyo
imejielekeza katika kufanya utafiti katika anga za mbali na kupata data ambazo
zitasaidia mahitaji ya kijeshi nchini humo.
Shirika la Habari la China Xinhua limeripoti kuwa
satelaiti hiyo SRSS-1 ilizinduliwa Jumapili ya Novemba 3 mwaka huu katika jimbo
la Kaskazini mwa China la Shanxi.
Msemaji wa serikali ya Sudan Mohamed al-Faki
Suleiman ameliambia shirika la habari la AFP kuwa miezi michache ijayo
satelaiti hiyo inatakuwa ikiangaliwa kutokea Sudan.
Al-Faki ameongeza kuwa uzinduzi huo umefanywa na
China ikiwa ni sehemu ya makubaliano katika mradi huo. Taifa la Sudan ambalo
hadi sasa linaendelea na mapambano yake dhidi ya uchumi ambao unaonekana ni
mbovu limekuwa likijitahidi kwa miongo kadhaa kufanya utafiti wa anga za mbali.
Mnamo mwaka 2013 enzi za utawala wa mbabe Rais
Omar al-Bashir alianzisha Chuo cha Utafiti wa Anga (ISRA).
CHANZO: SPACE WATCH AFRICA
0 Comments:
Post a Comment