Friday, November 1, 2019

Somalia ni taifa la namna gani?


Somalia ni taifa lililopo kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki katika Pembe ya Afrika. Kijiografia, imezungukwa upande wa kaskazini-mashariki na Ethiopia na Jibuti, na upande wa magharibi ya kati na Kenya; Ghuba ya Aden nayo iko mashariki. 

Mji mkuu na mji mkubwa zaidi ni Mogadishu ambao una wakazi milioni 2.1 Mogadishu ipo katika mkoa wa Banaadir ambao ni miongoni mwa mikoa 18. Nchi iliunganika mwaka 1960, kutokana na makoloni mawiliː la Waitalia (kusini) na la Waingereza (kaskazini). 

Baada ya mwaka 1991 nchi ya Somalia ilibaki haina serikali wala umoja wa taifa, iligawiwa na wakereketwa na wanamgambo wa ukoo na eneo, hasa Somaliland, Puntland na Galmudug upande wa kaskazini. Katika miaka 2008-2013 ilihesabika kama nchi filisika. 

Kwa sasa ni nchi dhaifu lakini inaanza kujengwa upya kama shirikisho na ndio kwa sasa inaitwa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia. Kisomali ndiyo lugha ya kawaida ya wakazi wengi na lugha rasmi pamoja na Kiarabu. 

Kati ya lugha nyingine zinazotumika nchini, mojawapo ni Kiswahili. Upande wa dini, 99.8% ni Waislamu, hasa Wasuni.

Jamhuri ya Somalia ilikaribia kuangamia kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini kwa sasa kampuni za binafsi za mawasiliano ya mitambo, zimetwaa karibu miji yote Somalia, na hata kutoa huduma njema kuliko nchi zilizo jirani. 

Somalia ni nchi mojawapo Afrika ambayo ina mawasiliano ya bei rahisi zaidi, pengine kwa kuwa Somalia haikuwa na serikali iliyotoza ushuru. 

Katiba wanayoitumia sasa ni ile ya mwaka 2012 baada ya kuifanyia marekebisho. Rais wa sasa wa Somalia ni waziri mkuu wa zamani wa taifa hilo Mohamed Abdullahi Mohamed (Farmajo). 

Tukio kubwa la kukumbukwa baada ya kuundwa kwa serikali ya Shirikisho ni kulipuka kwa bomu Oktoba 2017 katika mji mkuu lililosababisha zaidi ya watu 500 kupoteza maisha.

Imetayarishwa na Jabir Johnson………………………………………….Novemba 1, 2019

0 Comments:

Post a Comment