Wahitimu wa Chuo cha ufundi
Ghona kilichopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameaswa kuanzisha viwanda
vidogo vidogo ili ziwasaidie katika
kuanzisha miradi yao ya kiuchumi .
Wito huo ulitolewa na
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Childreach Tanzania Martha
Lyimo, wakati alipokuwa akikabidhi jana vyerehani na vifaa
vya useremala kwa wahitimu hao ambao ni viziwi katika mahafali yao nane chuoni
hapo.
Akizungumza kwa niaba ya
mkurugenzi Meneja miradi wa Childreach Tanzania Bi. Winfrida Kway, alisema watu
wenye ulemavu mara kwa mara katika maisha yao ya kila siku wamekuwa wakikabiliwa na vitendo
vya kubaguliwa, kutengwa na kukataliwa kutokana na ulemavu wao hivyo Childreach
Tanzania imeona ni vema wahitimu hao
ikawapatia vitendea kazi hivyo ambavyo vitaweza kuwasaidia kwenda kuanzisha
viwanda vidogo vidogo.
Bi. Winfridah Kway |
“Mwaka 2017 hadi mwaka 2019
shirika la childreach Tanzania kupitia mradi wake wa mafunzo kwa vitendo
limeweza kuwafikia jumla ya wanafunzi 23 kwa kuwawezesha vifaa mbalimbali kama vile
vyerehani, vitambaa vya kushonea nguo na vifaa vya useremala, ikiwa ni pamoja
na mahitaji mengine yote
muhimu,”alisema.
Aliongeza kusema kuwa
“Wanafunzi wa fani ya useremala hupewa
nyenzo zote muhimu za kuweza kujiajiri pindi wanapo rudi majumbani huku wanafunzi wa fani za ushonaji nao pia
huwezeshwa vifaa kama vile vyerehani na vitambaa,”alisema.
Aidha alisema Childreach
Tanzania pia imeweza kujenga miradi mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa darasa
kwa ajili ya kusomea na kufanyia mafunzo ya vitendo, uboreshaji wa vyoo ili
kuwawezesha wanafunzi kuwa na miundombinu mizuri ya kiafya ili kuweza kunguza
magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake mgeni rasmi
katika mahafali hayo Afisa Elimu Ufundi Halmashauri ya Moshi Ladislaus Tilya, alisema endapo wahitimu hao
wataitumia vyema taaluma waliyoipata wataweza kujitengenezea ajira na hata
kuajiri watu wengine.
Awali akitoa taarifa ya
maendeleo ya chuo, Mkuu wa Chuo hicho Aminiel Mwanga alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho
mwaka 2010 na umoja wa wazazi wenye watoto walemavu Kanda ya Kaskazini (UWAVIKA),
wanafunzi hao wamefaidika na mafunzo mbalimbali, ambayo yamekuwa yakitolewa
chuoni hapo.
“Lengo la kuanzishwa kwa
kituo hiki ni kuwasaidia watoto viziwi ambao wanamaliza elimu ya msingi na
hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari na waliohitimu elimu ya
sekondari na hawakupata mahali pa
kujifunza stadi mbalimbali za kiufundi zitakazowasaidia kujitegemea wao wenyewe,”alisema.
"Mbele yako kuna
vijana 10 viziwi wakiwemo wasichana 5 na
wavulana 5 ambao wamehitimu leo mafunzo yao ya ufundi yaliyodumu kwa muda wa
miaka mitatu, wahitimu hao walijifunza masomo ya taaluma kama vile Hisabati ,
kiingereza , Kiswahili, uraia, ujasiriamali na stadi za maisha pia wamejifunza
masomo ya ushonaji kwa wasichana na wavulana walijifunza useremala, uchomeleaji
kama masomo ya misingi ya ufundi,"alisema Mwalimu Mwanga.
STORY BY: Kija Elias, Moshi
DATE: Novemba 27, 2019
0 Comments:
Post a Comment