Monday, November 11, 2019

Askofu Hotay awaasa kidato cha nne kuhusu Utandawazi


Askofu  wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Hotay, amewataka wazazi na walezi kuwa na jicho la pekee kwa vijana wao ambao wanaishi katika kizazi chenye kasi ya maendeleo ya utandawazi.

Askofu Hotay, aliyasema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 20 ya shule ya sekondari Bishop Alfa Memorial, iliyopo Pasua Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, shule hiyo inamilikiwa na kanisa hilo.

Askofu aliwataka wazazi na walezi kuwasimamia vijana wao vema katika suala la maadili , kwani ulimwengu wa sasa umegubikwa na utandawazi mkubwa wa kiteknolojia, ambao kwao wakiutumia vizuri, utawasaidia na wakiutumia vibaya, utawapoteza.

Aidha, Askofu Hotay aliwataka wanafunzi wanaohitimu elimu ya sekondari kuweka bidii zao katika kusoma, maana bila kuwa na elimu , dunia itawasubiri na mambo mabaya yaliyopo ndani yake yatawangoja kwa hamu, kama matumizi ya mitandao ya kijamii yasiyo sahihi kwao.

“Ninawasihi sana vijana wangu mitandao ya kijamii ina faida zake na hasara zake, kama mtaitumia vizuri inaweza kuwasaidia katika kujiendeleza kielimu, lakini kama mtaitumia vibaya, bila kuchuja mitindo ya maisha iliyo kinyume na maadili yetu mtapotea ,”alisisitiza Askofu Hotay.

Alisema ugunduzi wa teknolojia upo katika hali ya juu kwa sasa na teknolojia kila siku inabadilika , akawaomba waende wakaitumia vizuri  teknolojia  ili iweze kuleta mapinduzi ya kisayansi katika taifa.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
DATE: Novemba 11, 2019

0 Comments:

Post a Comment