Thursday, November 7, 2019

Kilimanjaro yatakiwa kufanya kilimo biashara


Wakulima mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuanza kulima kilimo hai cha kibiashara ambacho kinatumia mbolea za asili ili kukifanya kilimo hicho kuwa chenye tija na kuweza kumwongeza mkulima mnyororo wa thamani katika mazao yanayozalishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi mtaalamu wa kilimo kutoka shirika lisilo la kiserikali la Solidaridad  Jumanne Magese, alisema baadhi ya wakulima wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya matumizi bora ya kilimo Hai hali ambayo wanahitaji kuwa taarifa sahihi ili waweze kuzifanyia kazi.

“Wakulima wengi wanaolima kilimo ambacho wanatumia madawa ya viwandani  ni kutokana na elimu kutowafikia kwa wakati, hivyo kwa sasa tunahitaji kuwa na wakulima ambao wanapata taarifa kwa wakati na kuzifanyia kazi,”alisema Magese.


Magese alisema, malighafi ambazo zimezalishwa kwa kutumia madawa ya viwandani zinakuwa na athari kubwa kwa mlaji, lakini kwenye kilimo Hai kunakuwa hakuna zile changamoto za mabaki ya kemikali za madawa yaliyoweza kutumika hali ambayo inamsaidia mkulima kuwa na umiliki wa mnyororo wa thamani  kutokana na mbolea za asili ambazo amezitumia katika shamba lake. 

“Ninawashauri wakulima kuanza kulima kilimo Hai kwa kutuamia mbolea za asili ikiwemo mkojo wa sungura, mbolea ya samadi, mkojo wa popo  na mkojo wa ng’ombe,"alisema.

Naye Mshauri wa Mawasiliano  kwenye Sekta ya  Kilimo Hai Tanzania Costantine Akitanda, aliwataka wakulima kupunguza matumizi ya kilimo cha mbolea zenye kemikali na badala yake watumie kilimo Hai ambacho kina tija kwa afya za watanzania.

Akitanda aliyasema jana wakati wa zaira ya waandishi wa habari ambao wapo kwenye mafunzo ya siku tatu, ambayo yanatolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) walipotembelea shamba la mkulima wa Kahawa Remy Temba, lililopo Uru- Shimbwa wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema zipo faida nyingi katika kilimo Hai kisichotumia kemikali ambapo mazao yake yanasoko kubwa duniani ikilinganishwa na mazao ambayo yanalimwa kwa kutumia mbolea za viwandani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mtendaji wa Shirika la Floresta Tanzania Richard Mhina alisema magonjwa mengi yanayotokana na vyakula ambavyo vimezalishwa na kemikali ambayo yanaingia kwenye mfumo wa mwili wa binadamu hupunguza uwezo wa mwili kupambana na magonjwa.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
DATE: 7/11/2019


0 Comments:

Post a Comment