Mahakama ya Mwanzo ya Moshi
Mjini mkoani Kilimanjaro imemhukumu mkulima na mkazi wa Bomambuzi katika
Manispaa ya Moshi kwenda jela miezi mitatu na baada ya kumaliza kifungo kutoa
shilingi 50,000 kila mwezi baada ya kupatikana na hatia ya kutelekeza familia
yake kwa miaka saba.
Hayo yamejiri baada ya mlalamikaji
aliyefahamika kwa jina la Akwilina Boniface Mwase (38), Mama Lishe na Mkazi wa
Bonite kuithibitishia mahakama pasipo shaka yoyote namna mshtakiwa
aliyefahamika kwa jina la Exaud Martin Urassa (55), kuitelekeza familia yake
tangu mwaka 2012.
Hakimu Mkazi wa mahakama
hiyo Adnan Kingazi alisema mlalamikaji alimshtaki mshtakiwa kwa shtaka moja la
kutelekeza familia kwa mujibu wa kifungu cha sheria Na. 166 na 167 ya kanuni ya
adhabu.
Awali mahakama baada ya
kupokea ushahidi ilijiuliza hoja za msingi kwamba je, viini halisi vinavyounda
shtaka la wizi vimetimia? Pia kwamba je, kuna ushahidi kuwa mshtakiwa
ametelekeza familia kama alivyoshtakiwa? Na kwamba je, upande wa mashtaka
umeweza kuthibitisha shtaka la wizi dhidi ya mshtakiwa katika kiwango
kinachostahili cha kutokuacha chembe ya shaka?
Hakimu Kingazi alisema
katika kujibu hoja hizo mahakama ilijikita zaidi katika ushahidi uliotolewa na
pande zote mbili ili kuthibitisha shtaka
lolote la jina kisheria ni lazima pawepo na nia ovu na tendo ovu la mshtakiwa.
Aidha Kingazi alisema ushahidi
uliotolewa na mashahidi wote watatu wa upande wa mashtaka ulionyesha kufanana
kwa kiasi kikubwa na waliloliona ni kwamba mstakiwa mwenyewe alikiri kushindwa
kutoa matunzo kwa familia yake toka aondoke nyumbani kwa mke wake.
Pia Mshtakiwa aliiambia
mahakama namna alivyoondoka na kumuacha mke wake akiwa na mtoto.
Mshtakiwa aliiambia
mahakama kuwa matunzo alitoa mara moja tu kiasi cha Tshs. 35,000/= mwezi
januari mwaka 2019 na hadi sasa hajawahi kutoa tena kutokana na kukosa kipato.
Ilidaiwa mahakama hapo kuwa
kati ya mwezi June 2018 hadi 2019 nyakati tofauti tofauti huko katika maeneo ya
Bonite, Manispaa ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro mshtakiwa kwa makusudi na bila
halali huku akifahamu kuwa ni kosa alimtelekeza mtoto wake mwenye umri wa miaka
13 mhitimu wa darasa la saba bila kumpatia matunzo na huduma nyingine muhimu
kwa mtoto kitendo ambacho ni kosa na kinyume cha sheria.
Mshtakiwa alikana shtaka
lake aliposomewa ndipo upande wa mashtaka walipotakiwa kuthibitisha shtaka
hilo.
Mlalamikaji aliambia
mahakama kwa uchungu namna ambavyo mshtakiwa kama mume wake alivyomtelekeza na
mtoto toka mwaka 2012 hadi kufikia uamuzi wa kwenda Ustawi wa Jamii ambapo
walimuamuru mshtakiwa atoe Tshs. 75,000/= kwa mwezi.
Mshtakiwa aligoma kutoa
kiasi hicho na alipobanwa sana alitoa Tshs. 35,000/= shtaka hilo linafikishwa
mahakamani hapo alikuwa hajawahi kutoa chochote.
Ilidaiwa mahakamani hapo Ofisi
ya Ustawi wa Jamii waliwapa barua ili waende Ofisi ya Dawati la Jinsia Polisi
ambako walihojiwa na mshtakiwa aliamriwa atoe matunzo akaendela kukataa ambapo
Mlalamikaji aliomba apewe kila mwezi Tshs. 50,000/= pamoja na gharama nyingine
za shule na matibabu.
Kwa upande mtoto huyo
mwenye umri wa miaka 13, aliiambia mahakama kuwa hajawahi kuona mshtakiwa
(yaani baba yake) akitoa matunzo ya kitu chochote na kuongeza hata vifaa vya
shule mama yake ndiye aliyekuwa akimnunulia. Pia mtoto huyo alisisitiza kuwa
mshtakiwa hakuwahi kumuuliza chochote kuhusu maendeleo yake shuleni.
Ushahidi wa upande wa
mlalamikaji uliendelea kutolewa mahakamani hapo ambako Omari Saidi Kubingwa
(80), Balozi wa nyumba 10 eneo walilokuwa wakiishi mshtakiwa na mlalamikaji
kama mke na mume aliiambia mahakama namna alivyoitwa na mlalamikaji mwaka 2012
na kumshuhudia mshtakiwa alifungasha virago na kuondoka nyumbani.
Alipomuuliza kwanini anatoa
vyombo na kuondoka alidai kuwa amechoshwa na tabia za mke wake za kurudi usiku
kila siku.
Shahidi huo aliongeza kuwa
alimuuliza mlalamikaji kuhusu tabia hiyo alikana na kusema kuwa mume wake ndiye
aliyekuwa akiondoka usiku na kurudi asubuhi. Aliendelea kumsihi sana mshtakiwa
asiondoke bila mafanikio.
Katika utetezi wake
mshtakiwa alikana kabisa kuitelekeza familia. Mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa
walianza kuishi na mlalamikaji toka mwaka 2005 na 2006 walimzaa mtoto huyo.
Mshtakiwa aliongeza kuwa waliendelea
kuishi pamoja hadi mwaka 2008 ambapo mlalamikaji alianza kwenda Semina za
maombi na kurudi usiku sana.
Alidai mahakama hapo kuna
wakati alikuwa akimuuliza na mlalamikaji alimwambia nabii amekuwa akiwaamuru
kuishi hivyo. Mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa mnamo mwaka 2012 maumivu
yalimshinda na aliamua kuondoka nyumbani na kwenda kuishi katika nyumba za
wageni yaani gesti ambapo mwaka 2014 alifanikiwa kupangisha maeneo ya
Uswahilini.
Hata hivyo katika shtaka
hilo ilidaiwa mahakama hapo mtoto huyo mwenye umri wa miaka 13 mhitimu wa
darasa la saba aliwahi kufanyiwa vitendo vya ukatili wakati alipokuwa akiishi
kwa baba yake huyo ambaye alioa mke mwingine.
Mtoto huyo alifukuzwa na
mlalamikaji kwa madai kuwa baba yake ameondoka nyumbani na amfuate huko aliko ambapo
mtoto huyo alikwenda kwa mshtakiwa na mshtakiwa alimpokea mtoto.
Mwaka 2017 mtoto huyo alibakwa
na alitoa taarifa polisi. Mtoto alifikishwa hospitali na baada ya kupimwa
alionekana kubakwa, kuumizwa na kusababishiwa maumivu makali sehemu zake za
siri.
Mtuhumiwa wa ubakaji alikamatwa
na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ambako mwaka jana 2018 alihukumiwa
kutumikia kifungo cha maisha jela.
Hakimu Kingazi alisema
mshtakiwa alishindwa kumlinda mtoto Princes wakati akiishi naye hadi
kusababisha kubakwa na kusababishiwa maumivu makali mwilini mwake.
Kibaya zaidi ni kwamba
badala ya kumfariji mtoto huyo mke mdogo wa mshtakiwa aliendelea kumfanyia
mtoto vitendo vya kikatili ikiwamo kumchapa vibaya hadi kumsababishia majeraha
mwilini mwake hadi walimu walimshangaa mtoto.
Kitendo hicho kilisababisha
walimu kutoa taarifa Ofisi ya Dawati la Jinsia Polisi ambapo waliwaita wazazi
wote wa mshtakiwa na kuwahoji kuhusu tukio hilo.
Ilielezwa mahakama hapo
kuwa mbakaji mbakaji tayari ameshahukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha
gerezani mwaka jana (2018) baada ya kupatikana na hatia na kwamba kilichobaki
ni ukatili aliotendewa na mama ndogo wake.
Hakimu Kingazi alitoa
maelekezo kuwa uchunguzi ufanyike upya na ikibainika mama mdogo huyo alimfanyia
mtoto kitendo cha ukatili basi apelekwe mahakamani kujibu shtaka na hatimaye
sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Aidha Hakimu Kingazi
alisema mshtakiwa amepunguziwa adhabu yake kutokana na sababu za maombolezo
alizozitoa kuwa anategemewa na familia nyingine ambapo anaye mtoto mchanga na
wazazi wake wote ni wazee na wanamtegemea yeye.
STORY BY: Jabir Johnson..........................Novemba
30, 2019.
0 Comments:
Post a Comment