Monday, December 2, 2019

Ufahamu mwezi Desemba



Huu ni mwezi wa 12 na wa mwisho katika mwaka kwenye mtiririko wa kalenda ya Julian na Gregori.

Ni mwezi wa saba na wa mwisho katika miezi saba yenye siku 31. Neno Desemba limetokana na neno la Kilatini ‘Decem’ ikiwa na maana ya 10. Kwa asili ni mwezi wa 10 katika kalenda ya Romulus ya mwaka 750 K.K ambayo ilikuwa ikianzia mwezi Machi.

Siku za baridi hazikujumuishwa katika mwezi. Lakini ilipoongezwa miezi ya Januari na Februari  ndipo Desemba ikabidi isalie kuendelea kutumia jina lake na kuwa katika mtiririko wa miezi 12.

Katika Rumi ya zamani sikukuu kubwa nne zilikuwa zikiadhimisha mwezi Desemba.

Baada ya kuanza kutumika kwa kalenda ya kisasa ya Gregori sikukuu hizo hazikuingizwa katika mtiririko huo.

Kwa upande wa Wafaransa waliwahi kutengeneza kalenda yao ambayo waliitumia kwa miaka 12 kutoka kwama 1793 hadi 1805 ambayo ilijulikana kwa jina la Kalenda ya Mapinduzi ya Ufaransa.

Katika kalenda hiyo mwezi Desemba ulijumuishwa katika miezi ya Frimaire (mwezi wa tatu) na Nivose (mwezi wanne); miezi hiyo ilikuwa ya barafu kuganda na baridi hivyo Desemba katika maeneo hayo huwa ni kipindi cha baridi na barafu.

Katika Elimu ya Nyota mwezi Desemba una nyota mbili; Mshale na Mbuzi.

Nyota ya Mshale ni nyota ya tisa katika mlolongo wa nyota 12. Nyota hii ni kwa watu waliozaliwa kati ya Tarehe 23 Novemba na 20 Disemba. Asili yao ni Moto.

Siku yao ya Bahati ni Alhamisi.  Namba yao ya Bahati ni 3. Sayari yao ni Jupiter (Mushtara).

Ubora unaohitajika kusawazisha mambo ni kuwa wenye uwezo wa Kuongoza, Kuratibu, Kuandaa, Kupanga na Kusikiliza kwa makini. Nyota za watu ambao anaelewana nao ni nyota za Punda na Simba. Nyota za watu ambao haelewani nao ni nyota za Mapacha, Mashuke na Samaki.

Wenye nyota ya Mshale ni waaminifu wanaopenda sana mafanikio, wako tayari wakati wowote katika kazi.

Kutokana na hili wana bahati ya kuwa katika sehemu muafaka na katika muda unaotakiwa.

Pia wenye Nyota ya Mbuzi huangukia katika mwezi huu pia kwani huanzia Disemba 21 na  Januari 19.

Sifa ya Nyota hii ni Uongozi. Ubora unaohitajika kusawazisha mambo ni kuwa wenye Uchangamfu na Furaha. Nyota za watu ambao anaelewana nao ni nyota za Ng’ombe na Mashuke.

Nyota za watu ambao haelewani nao ni nyota za Punda, Kaa na Mizani. Mbuzi wana kipaji cha kuchambua mambo kidogo kidogo au kufuatilia kitu bila watu kujua na kupata ufumbuzi wa uhakika mwishoni.

Mbuzi wanapenda kuwajibika, ni wenye bidii ya kazi, katika kazi yeyote watakayofanya hata kama ikiwa ni ya kipuuzi.

Ni viumbe waaminifu sana, watu wastahamilivu na wenye kuweza kuvumilia matatizo yeyote.

Imetayarishwa na Jabir Johnson...........................Desemba 2, 2019




1 comment: