Wednesday, December 11, 2019

LATRA: Usafiri wa treni Moshi utamaliza changamoto ya usafiri


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) Gilliard Ngewe, amesema kuwepo kwa usafiri wa gari Moshi kutaondoa changamoto ya usafiri kwa wakazi wa mikoa ya kanda ya Kaskazini ambao wengi wao walikuwa wakijikuta wakipata adha kubwa ya usafiri hasa inapofika msimu wa siku za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Ngewe aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanahabari muda  mfupi mara baada ya kuwasili kwa treni ya abiria ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika kituo cha Moshi, mkoani Kilimanjaro ikitokea Jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa miaka mingi abiria waliokuwa wakisafiri kwa kutumia usafiri wa sekta binafsi walikuwa wakilangulia nauli kutoka Sh 20,000 hadi Sh 100,000 hususani katika kipindi cha sikuu ya Krismasi na mwaka mpya.

Katika hatua nyingine  Mkurugenzi huyo alitoa maelekezo kwa TRC  kuhakikisha kwamba maeneo ambayo bado ni korofi kuhakikisha yanarekebishwa ili watumiaji wa usafiri huo waweze kufika kwa muda uliopangwa ili kuondoa usumbufu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TRL Prof. John Kondoro, alisema majaribio ya treni hiyo yanalenga kupima hali ya uhitaji wa usafiri wa treni kwa nyakati mbalimbali.

Prof. Kandoro alisema treni hiyo iliwasili mjini  Moshi  saa tano na nusu  ikitokea Jijini Dar es Salaam ikiwa na mabehewa tisa, saba yakiwa ni ya abiria wa madaraja mbalimbali, moja la mizigo na moja la chakula na kwamba liliwasili mjini Moshi, likiwa na abiria zaidi ya 260.
“Changamoto tuliyokumbana nayo wakati tunakuja na ndiyo imetufanya tuchelewe kuingia ni ile ya baadhi ya miundo mbinu ya reli kuwa ya mashaka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha”, alisema.

Aidha  Prof. Kondoro alisema ilibidi maeneo mengine treni hiyo iendeshwe kwa umakini kutokana na ukweli kuwa usalama wa abiria ni lazima upewe kipaumbele.

“Miundo mbinu hii ndiyo inaanza kutumika sasa baada ya kutokutumiwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, hivyo ni lazima kuwe na tahadhari”, alisema.

Naye  katibu wa Bodi ya (TRC) Hawa Mwenda, alisema tiketi zote za daraja la pili kulala na lile la daraja la pili kukaa, zilikwisha muda mfupi hata kabla baadhi ya abiria waliofika kituo cha Moshi wakitokea Dar es Salaam, hawajaondoka kituoni hapo.

“Taarifa zilizoko eneo la kukatia tiketi ni kwamba tiketi zote 48 za daraja la pili (kulala) na 60 za daraja la pili (kukaa) zimejaa”, alisema na kuongeza, tayari zile za daraja la tatu zilimalizika mapema huku  abiria wanaohitaji bado walikuwa ni wengi.

Bi Mwenda alisema mwitikio wa abiria umekuwa mkubwa kuliko matarajio ya shirika hilo na ilibidi maofisa wa shirika hilo walioko ofisi ya Moshi kuwasiliana na wenzao walioko katika vituo vya njiani kama vile Kisangiro, wilayani Mwanga na kwingeneko, ili kuangalia uwezekano wa kuuza tiketi ambazo hazijapata wateja katika maeneo hayo ili wauziwe wale walioko katika kituo cha Moshi.

Alisema tayari wateja wengi haswa wafanyabiashara wameonyesha nia ya kutumia usafiri huo kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao yakiwemo mazao ya kilimo kwa kile alichosema wameeleza ni kuepuka changamoto wanazokumbana nazo wanapotumia usafiri wa barabara kusafirishia mizigo yao.

Treni hiyo ya abiria, iliwasili Desemba 7 mwaka huu mjini Moshi majira ya saa tano za asubuhi na kupokewa na mamia ya wananchi, ambapo mbali na wale waliokwenda kuwapokea wageni wao, wengi wao walikuwa ni wananchi waliokwenda kushuhudia kuanza tena kwa huduma hiyo ya treni kati ya Moshi na Dar es Salaam, baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miaka 25.

STORY BY: Kija Elias
DATE: Desemba 11, 2019

0 Comments:

Post a Comment