Wednesday, December 25, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Muhammad Jinnah ni nani?


Desemba 25, 1876 alizaliwa mwanasheria, mwanasiasa na mwasisi wa taifa la Pakistan Muhammad Ali Jinnah maarufu Qaid-i-Azam ikiwa na maana Kiongozi Mkubwa. 

Ali Jinnah alizaliwa Karachi, wakati huo ikiwa India kwa sasa ni Pakistan na Kufariki dunia Septemba 11, 1948. 

Alikuwa mwanasiasa wa Kiislamu, mwasisi na gavana –jenerali wa kwanza wa Pakistan. 

Jinnah alikuwa mtoto wa kwanza kati ya saba wa mzee Jinnahbhai Poonja ambaye alikuwa mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na mkewe Mithibai. 

Familia hiyo ilikuwa miongoni mwa wanachama wa ngome ya Khoja ambao ni Wahindu walioachana na imani hiyo na kujiunga na Uislam kwa karne nyingi zilizopita na pia Familia hiyo ilikuwa ni wafuasi wa Aga Khan. 

Tarehe rasmi ya kuzaliwa kwake inachanganya kwani rekodi za shule zinaonyesha alizaliwa Oktoba 25, 1875 lakini  Jinnah mwenyewe aliwahi kusema kuwa alizaliwa Desemba 25, 1876. 

Baada ya kupata mafunzo ya shule akiwa nyumbani mnamo mwaka 1887 Jinnah alipelekwa katika shule moja maarufu mjini Karachi ya Sind Madrasat al-Islam ambayo kwa sasa ni Chuo Kikuu kinachofahamika kwa jina la Sindh Madressatul Islam.  

Baada ya hapo Jinnah alikwenda kwenye shule ya Kikristo ya CMS. Akiwa hapo alifanikiwa kufanya mtihani uliompa kwenda Chuo Kikuu cha Bombay ambacho kwa sasa ni Mumbai nchini India. 

Kutokana na ushauri aliopewa na rafiki yake ambaye alikuwa Mwingereza, Baba yake mzee Poonja aliamua kumpeleka mtoto wake nchini England ili kupata uzoefu wa kibiashara. 

Lakini kabla hajaondoka wazazi wake walifanya mipango ya haraka ili aweze kuoa. 

Alitua London na kujiunga na Lincoln Inn ikiwa ni miongoni mwa taasisi ya kisheria ambayo ilikuwa ikiwaandaa wanafunzi kuwa wanasheria. Mnamo mwaka 1895 akiwa na umri wa miaka 19 alikuwa rasmi miongoni mwa waliokuwa vizuri katika taasisi hiyo. 

Akiwa bado jijini London Jinnah alipatwa na mfadhaiko baada ya kufiwa na mke wake na mama yake. 

Hata hivyo alifanikiwa kumaliza masomo yake ambayo alikuwa akisomea muundo wa Kisiasa wa Uingereza na mara kadhaa alikuwa akizuru katika baraza la wawakilishi au bunge dogo la Uingereza. 

Alivutiwa zaidi na falsafa ya Uliberali ya William E. Gladstone ambaye alikuja kuwa waziri mkuu wa nne wa Uingereza mnamo mwaka 1892 mwaka ambao Jinnah alikuwa akiwasili London. 

Hata hivyo Jinnah aliendelea kufuatilia kwa karibu maisha na masuala kadhaa ya Wahindi na wanafunzi wa Kihindi. 

Wakati kiongozi na mwanamapinduzi wa India Dadabhai Naoroji alipokuwa katika Bunge la Uingereza; Jinnah na wanafunzi wenzake wa Kihindi walikuwa wakifanya kazi usiku na mchana kwa ajili yake na matokeo yake alifanikiwa. 

Naoroji aliweka rekodi ya kuwa mhindi wa kwanza kukalia kiti katika bunge dogo la Uingereza. 

Mnamo mwaka 1896 Jinnah alirudi zake Karachi na kukuta biashara za baba yake zikiwa katika hali mbaya na hivyo kuanza kujitegemea. Jinnah aliamua kwenda zake Mumbai kwa ajili ya shughuli za kisheria ambako ilimchukua miaka mingi kuweka misingi ya kuwa mwanasheria imara. 

Takribani kwa miaka 10 baadaye Jinnah alikuwa amejiingiza vizuri katika masuala ya siasa. 

Hakuwa nah obi yoyote, hakuegemea sana katika dini aliweza kujigawa vizuri katika sheria na siasa. 

Pia Jinnah hakuwa mtu wa kupenda wanawake kwani alijinidhamisha kwa mwanadada Rattenbai (Rutti) binti wa Sir Dinshaw Petit ambaye alikuwa milionea wa Mumbai. 

Alimuoa mwanadada huyo mnamo mwaka 1918 licha ya upinzani mkali kutoka kwa wazazi wake na watu wengine wa karibu. Baadaye alifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike waliyempa jina la Dina. 

Kutokana na shinikizo kutoka kila upande hawakuweza kuwa na furaha hatimaye walitengana. 

Alikuwa ni dada yake aliyefahamika kwa jina la Fatima aliyeamua kumsaidia kwa kumpa msaada wa kisheria na kampuni. 

Katika masuala ya kisiasa kwa mara ya kwanza Jinnah alionekana mwaka 1906 akiwa na Chama cha Congress kwenye mkutano mkuu uliofanyika Kolkata na kuanzia hapo chama hicho kilianza kupigania uhuru wa taifa la India. 

Miaka minne baadaye alichaguliwa kuwamo katika baraza la kiheria  na ndio ukawa mwanzo wake katika kujiwekea mizizi ya kisiasa hadi kuwa kiongozi mkubwa. 

Jinnah alikuwa amedhamiria kuweka umoja na mshikamano baina ya Wahindu na Waislamu akiwa katika harakati hizo alipewa cheo cha kuwa balozi bora wa Muungano wa Wahindu na Waislamu ambacho alipewa na Gokhale. 

Wakati akiendelea ushawishi wa Mahtma Gandhi katika siasa za India ulianza kuwa juu hivyo aliamua kuachana na Chama cha Congress mnamo mwaka 1920. 

Alipojiondoa alitumia muda wake mwingi katika Muungano wa Kiislamu maarufu Muslim League. 

Katika siasa za Pakistan anachukuliwa kuwa ni baba kutokana na kufuatilia kwa karibu maandiko na mashairi ya Mwanafalsafa Sir Muhammad Iqbal. 

Mvutano wa upande ambao ulikuwa na waamini wengi wa Kiislamu ndio ulifanya kupatikana kwa taifa la Pakistan kwani Waingereza ilibidi waingilie kati ambapo Machi 22-23, 1940 mjini Lahore Muslim League ilifikia mwafaka wa kuanzisha taifa la Kiislamu la Pakistan hivyo ukawa mwanzo wa kujitenga kwake na India ambayo ilikuwa na wanaharakati wengine Mahtma Gandhi na Jawaharlal Nehru ambao walikuwa Wahindu. 

Waingereza walikubali kuwapo kwa taifa la Pakistan mnamo mwaka 1947 na Jinnah akawa kiongozi wa kwanza wa ardhi hiyo huru. 

Alikutana na changamoto nyingi kutokana na uchanga wa taifa hilo; watu wa ardhi hiyo hawakumchukulia Jinnah kama Gavana-Jenerali kama Waingereza walivyotaka wao walimwita Baba wa Taifa. 

Alifanya kazi kwa nguvu na kujituma hadi alipofariki dunia mnamo mwaka 1948 kutokana na umri na ugonjwa. Alizikwa jijini Karachi ambao ni mji mkuu wa Pakistan katika eneo alilozaliwa.



0 Comments:

Post a Comment