Tuesday, December 3, 2019

Burkina Faso ni taifa la namna gani?


Burkina Faso ni taifa lililopo Afrika Magharibi ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 274,200.

Taifa hili limezungukwa na nchi sita Mali kwa upande wa Kaskazini, Niger kwa upande wa Mashariki, Benin kwa upande wa Kusini Mashariki, Togo na Ghana kwa upande wa Kusini na Ivory Coast kwa upande wa Kusini Magharibi.

Julai 2019 Umoja wa Mataifa ulikadiria idadi ya watu wa taifa hilo kuwa ni milioni 20.3

Burkina Faso ni taifa lililopo katika ukanda wa nchi zinazotumia lugha ya Kifaransa (Francophone) katika shughuli za kila siku. Asilimia 40 ya watu waliopo katika taifa hilo huzungumza lugha ya Mossi.

Awali taifa hilo lilikuwa likifahamika kama Upper Volta kutoka mwaka 1958 hadi 1984 lakini Agosti 4, 1984 Rais wa wakati huo Thomas Sankara alibadilisha jina hilo na kuwa Burkina Faso.

Watu wa taifa hilo wamekuwa wakifahamika kwa jina la Burkinabe. Mji mkuu wa Burkina Faso ni Ouagadougou (Wagadugu).

Taifa hilo lilijipatia uhuru wake mnamo Agosti 5, 1960 chini ya Rais Maurice Yameogo.

Mnamo mwaka 1966 Yameogo aliondolewa madarakani  kwa mtutu wa bunduki katika jaribio lililofanikiwa.

Kuondolewa huko kulitokana na hali ya njaa na ukame katika taifa hilo na mapinduzi hayo ya kijeshi yalifanywa na Sangoule Lamizana amabye alikuja kuwa Rais baadaye wa taifa hilo.

Hata hivyo mnamo mwaka 1980 aliondolewa madarakani kwa nguvu za kijeshi katika jaribio lililongozwa na Save Zerbo kutokana na hali ngumu katika vyama vya ushirika.

Serikali ya Zerbo ilipinduliwa mwaka 1982 na Jean-Baptiste Ouedraogo. Huyu alikuwa wa mrengo wa kushoto na waziri mkuu wake akawa Thomas Sankara.

Sankara akatupwa jela na wakati juhudi za kumtoa zikifanyika mapinduzi ya kijeshi yalifanyika mnamo mwaka 1983 na Sankara kuwa Rais wa taifa hilo.

Akiwa madarakani Sankara alibadilisha kabisa maisha ya watu wa taifa hilo ndani ya muda mfupi aliokaa madarakani akiweka sera ya elimu mbele katika taifa hilo.

Usawa katika ugawa wa ardhi hususani kwa wakulima, kuwatetea wanawake na watoto dhidi ya ndoa za utotoni na ukeketaji.

Aliondolewa madarakani na kuuawa mwaka 1987 na rafiki yake wa karibu Blaise Compaore.

Akiwa madarakani Compaore alinusurika kuondolewa madarakani kwa mtutu wa bunduki mnamo mwaka 1989 na hivyo akaitisha uchaguzi wa mwaka 1991 na 1998 aliopita.

Mwaka 2005 pia alirudi madarakani kibishi katika miongoni mwa chaguzi zilizolalamikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa haukuwa huru na wa haki.

Mnamo mwaka 2014 kulifanya maandamano makubwa nchini humo yaliyomfanya atoroke nchini humo na kwenda zake uhamishoni na nafasi yake kuchukuliwa na Rais wa mpito Michel Kafando.

Novemba 29, 2015 Roch Marc Christian Kabore alichaguliwa kuwa Rais wa taifa hilo kwa asilimia 53.5 ya kura na aliapishwa Desemba 29, 2015.

Uchaguzi huo ulitokana na jaribio la mapinduzi ya kijeshi na kikosi cha ulinzi na usalama cha zamani cha Rais Compaore cha RPS.

Compaore hadi sasa yupo nchini Ivory Coast alikokimbilia baada ya kujiuzulu nafasi hiyo.

Imetayarishwa na Jabir Johnson ………………………….Desemba 3, 2019

0 Comments:

Post a Comment