Friday, December 20, 2019

TCRA yasisitiza umuhimu wa usajili laini za simu


Mhandisi Imelda Salum; Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwasababu unawalinda watumiaji dhidi ya wahalifu wanaotumia mitandao sambamba na kuisaidia serikali kuwa na takwimu sahihi ya watumiaji wa huduma za simu za mkononi, zitakazosaidia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Hayo yamejiri Ijumaa ya Desemba 20 mwaka huu wakati wa zoezi la usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama za vidole ikiwa ni mwendelezo wa mpango wa Mamlaka hiyo kutoa elimu ya usajili wa laini za simu kwa wafanyabiashara wa soko la Memorial  lililopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Imelda Salum.

“Lengo la kuendesha zoezi la usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole ni kudhibiti vitendo vya uhalifu unaofanyika kwa njia ya mitandao ukiwepo utapeli  hivyo anasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kusajili laini zenu  za simu kabla ya Desemba 31 mwaka huu ambapo zoezi hilo litafungwa,” alisema Mhandisi Imelda.

“Zoezi hili la usajili wa laini za simu lilianza tangu mwezi Mei mwaka 2019 ambapo serikali ilianza rasmi kusajili laini za simu  kupitia Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA),kupitia mfumo huu wa laini za vidole serikali itaweza kudhibiti vitendo vinavyofanywa kwenye mitandao ya simu ambavyo ni vitendo vya kihalifu kwa sababu tunaamini kabisa wananchi wakisajili laini zao kwa mfumo huu wa alama za vidole tutaweza kuwatambua kwa urahisi watumiaji wote wa huduma za mawasiliano waliopo kwenye nchi yetu,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Moshi Kippi Warioba, Afisa Tawala ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Moshi Natanael Mshana, amewataka wenye kapuni za simu kuhakikisha  wanakwenda zaidi maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna changamoto ya wananchi kusajiliwa laini zao za simu.

“Asilimia 75 ya wananchi walio wengi wapo maeneo ya vijijini, wananchi hawa  wanahitaji sana huduma hii, niwaombe wenye makampuni kutoka zaidi mjini na kwenda vijijini wazazi wetu walioko vijijini wakipata hii huduma ni rahisi kwao hata watoto wanaoishi mjini kuwatumia fedha,” alisema.

Aliongeza kusema kuwa  jumla ya laini milioni 19.68, zimeshasajiliwa kwa alama za vidole ambazo sawa na asilimia 72 ya laini zote  zinazotumika  ambazo ni idadi ya laini milioni  47.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Moshi wameiomba Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuharakisha zoezi la utoaji wa vitambulisho ili wananchi waweze kutumia katika zoezi hilo la usajili wa laini za simu.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EDITED BY: Jabir Johnson
DATE: Desemba 20, 2019

Afisa Tawala wa Wilaya ya Moshi Natael Mshana akipokea zawadi ya simu kutoka kampuni ya mawasiliano nchini ya Halotel wakati wa usajili wa laini za simu za mkononi. 


0 Comments:

Post a Comment