Monday, December 16, 2019

Wagonjwa wenye VVU/Ukimwi Moshi Vijijini wakimbia matibabu

Wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, wamedaiwa kukimbia kiliniki za dawa katika hospital na vituo vya afya, mara baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo,  jambo ambalo limepelekea kusuasua kwa utoaji wa huduma ya ufuatiliaji hasa kwa wagonjwa wanaoishi maeneo ya vijijini.

Aidha wagonjwa hao wengine wamedaiwa kwamba wamebadili hata majina yao halisi huku wengine wakihama kwenye  maeneo wanayoishi na kwenda kuishi katika  mikoa mingine ili wasijulikane hali inayodaiwa kutishia kuwepo kwa ongezeko kubwa la maambukizi ya VVU katika jamii.

Hayo yameelezwa jana na Muuguzi na mshauri nasaha Judith Shayo, ambaye pia ni Mratibu wa kikundi cha Ndekira kilichopo Kibosho  wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kituo kinacho hudumia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Alisema changamoto zinazowakabili wauguzi kwa sasa katika majukumu yao  ni kuwepo kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa VVU ambao wamekimbia huduma hiyo  hali hiyo inachangia kufifisha juhudi zao katika kupunguza maambukizi .

“Hapa Kibosho kuna wagonjwa walioanza kiliniki vizuri, halafu wamepotea  ghafla wamekuwa hawaji tena kuchukua dawa, tumekuwa tukiwatumia wale walioelimishwa kuwatembelea wagonjwa vijijini, wanapokwenda kuwatafuta wale wagonjwa wanapofika kwa ndugu zao wanaambiwa kwamba huyu mtu alishafariki, au alihama na kwenda kuishi zake mkoani Singida hayupo tena hapa,"

aliongeza kuwa "Inabidi kuwafuatilia huko Singida unakuta hapatikani tena kwenye namba yake ya simu aliyoitoa, hivyo imekuwa changamoto kwetu kwani pia tumegundua wagonjwa wengine wanadanganya majina yao halisi,”alisema.

Alisema kuwa changamoto nyingine ni kuwa kikundi hicho kimelemewa na watoto wenye mahitaji na hivyo kushindwa kuwahudumia kutokana na mashirika yaliyokuwa yakitoa misaada hiyo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum kujiondoa.

“Changamoto hii ni kubwa mashirika ambayo tulikuwa tukiyategemea yamejitoa hivyo hatuna tena uwezo wa kuwahudumia hawa watoto hii imetuathiri sana kwani fedha ambazo walikuwa wakitusaidia zilikuwa zikitumika kuwaibua watoto ambao wanamahitaji maalum,”asema.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo yalifanyika hivi karibuni, Prof. Patrick Ndakidemi, alisema serikali imeanza kuboresha mazingira katika sekta ya afya  ili kupunguza changamoto zilizopo kwa wauuguzi. “Tuendelee kuwapongeza watoa huduma wetu wa afya  waendelee kutoa elimu ya afya kwenye jamii kuhusiana na maambukizi ya virusi vya ukimwi, kwani takwimu kwa wilaya ya Moshi Vijijini ni asilimia 1.3 haya ni maambukizi makubwa sana  hivyo ni vyema walioko kwenye ndoa na wale ambao bado ni vyema wakawa waaminifu kwenye ndoa zao,”alisema

Vilevile Prof. Ndakidemi ameitaka jamii hususani waliko kwenye ndoa kuwa waaminifu na wenza wao huku wanaokaribia kuoa kuhakikisha kwamba wanachukua jukumu la kupima afya zao kwanza.

Akielezea namna alivyoupata ugonjwa huo mmoja wa waathirika wa ugonjwa huo (jina tunalo), alisema kutokana na Mama yake mazazi kutokuhuduria kiliniki kwa wakati, “Mimi hapa mama yangu alipokuwa na ujauzito wangu, alikuwa hahudhurii kiliniki  mara kwa mara  alikuwa hajuia kama ana maambukizi ya VVU, nilikuja kujitambua nikiwa darasa la nne,”alielezea kijana huyo.

Katika harambee hiyo zaidi ya Sh milioni 8 zilipatikana pamoja na vyakula , nguo kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi na VVU.

2 comments: