Thursday, December 5, 2019

Ivory Coast ni taifa la namna gani?


Ivory Coast ni taifa ambalo lipo Kusini ya Pwani ya Afrika Magharibi. Mji Mkuu wa taifa hilo ni Yamoussoukro uliopo katikati ya taifa hilo. 

Hata hivyo mji mkuu wa kibiashara na kitovu cha uchumi wa taifa hilo ni Abidjan. 

Taifa hilo limepakana na Guinea  na Liberia kwa upande wa Magharibi, Burkina Faso na Mali kwa upande wa Kaskazini, Ghana kwa upande wa Mashariki, na Ghuba ya Guinea iliyopo katika bahari ya Atlantiki kwa upande wa Kusini. 

Taifa hilo kabla halijatawaliwa na mataifa kutoka barani Ulaya lilikuwa na dola mbalimbali kama Gyaaman (Kong) na Wabaule. Mnamo mwaka 1843 Ufaransa ilishika mamlaka ya eneo hilo na ilipofika mwaka 1893 ikalifanya kuwa koloni lake. 

Taifa la Ivory Coast lilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1960 na Rais wake wa kwanza akiwa ni Félix Houphouët-Boigny aliyetawala taifa hilo hadi mwaka 1993. 

Mnamo mwaka 1999 taifa hilo liliangukia katika mapinduzi ya kijeshi na mwaka 2002 lilijiingiza katika vita vya kidini likirudia tena mnamo mwaka 2007 pia 2010 hadi 2011. 

Mnamo mwaka 2000 taifa hilo lilijipatia katiba mpya. Taifa hilo linasifika kwa kuwa na madaraka makubwa kwa Rais. 

Uzalishaji wa kakao, kahawa umekuwa ndio mhimili wa taifa hilo la Afrika Magharibi. 

Katika kilimo hicho taifa hilo lilitisha sana miaka ya 1960 hadi 1970 na ilikwenda hadi miaka 1980. Katika karne ya 21 uchumi wa taifa hilo umejikita katika masoko hususani kilimo biashara. 

Lugha ya taifa hilo ni Kifaransa huku lugha za makabila zikiendelea kama Wabaule, Dioula, Dani, Anyin na Cebaara Senufo. 

Kwa ujumla lugha 78 kwenye taifa hilo zinazungumzwa. Idadi kubwa ya waumini ni wa Kiislamu na Wakristo wa Katoliki.

Imetayarishwa na Jabir Johnson.........................................Desemba 5, 2019

0 Comments:

Post a Comment