Desemba 23, 1933 alizaliwa
mtawala wa kimila wa Japan Akihito ambaye nashika rekodi ya kuwa Mtawala wa 125
wa Japan.
Akihito alichukua madaraka hayo ya kimila Januari 7, 1989 hadi
yalipokoma Aprili 30, 2019 na mtoto wake Prince Naruhito akishika madaraka hayo.
Jina lake ni Tsugu Akihito wa utawala wa Heisei.
Akihito alizaliwa Tokyo nchini
Japan. Ukoo huo wa Heisei unakuwa miongoni mwa koo za kifalme zilizotawala kwa
muda mrefu. Akihito ni mtoto wa tano na mtoto wa kwanza wa kiume wa Mtawala wa
Japan Hirohito (Emperor Showa) na mama yake ambaye ni Malkia Nagako.
Tangu
akiwa mtoto alianza kuishi katika namna ya kijadi ya Japan kama mtoto wa
kifalme ambapo mwaka 1940 alianza kusoma elimu yake katika shule ya Peers.
Mwishoni
mwa vita vya pili vya dunia Akihito alikuwa akiishi nje ya Tokyo lakini alirudi
kuendelea na shule mnamo kwa 1949 baada ya vita kumalizika.
Vita hivyo
vilipomalizika viliondoa nguvu ya Mfalme kutawala katika kila sekta isipokuwa
katika baadhi ya matukio na kusalia kuwa na nguvu katika sherehe tu.
Akiwa shuleni Akihito alijitahidi kujifunza
lugha ya kiingereza na utamaduni wa Magharibi. Mwalimu wake alikuwa Elizabeth Gray
Vining ambaye alikuwa raia wa Marekani.
Kama ilivyokuwa kwa baba yake Akihito
alisomea masuala ya Baiolojia ya Majini. Mnamo mwaka 1952 alipokuwa na umri wa
miaka 19 aliingia kama mrithi wa kiti cha Ufalme wa Japan.
Miaka saba baadaye
alivunja rekodi iliyokaa kwa miaka 1,500 alipomuoa mwanamke Shōda Michiko ambaye
ni binti mfanyabiashara tajiri katika ardhi hiyo.
Michiko alikuwa amemaliza
elimu yake katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Wanawake jijini Tokyo.
Akihito
ana watoto Prince Naruhito aliyezaliwa Februari 23, 1960, Prince Akishino
(Novemba 30, 1965) na Princess Nori (Aprili 18, 1969).
Akihito alikuwa mtawala wa Japan Januari 7,
1989 baada ya kifo cha baba yake. Rasmi alitawazwa kukalia kiti hicho Novemba
12, 1990. Utawala wake umepewa jina la Heisei ikiwa na maana Kuipata Amani.
Akihito na Michiko wamezuru maeneo mbalimbali hapa ulimwenguni wakiwa ni mabalozi wenye nia njema wa Japan.
Akihito alionekana kwa mara ya kwanza katika runinga mnamo mwaka 2011 baada ya
tetemeko la ardhi na
Tsunami lililoathiri zaidi upande wa Kaskazini Mashariki mwa Honshu.
Tetemeko hilo liliondoa maisha ya
watu akali ya 20,000 na kuwa la pili kwa uharibifu baada ya ajali ya kinu cha
nyukilia cha Fukushima Daiichi.
Agosti 8, 2016 alionekana tena katika runinga
akiweka bayana nia yake ya kuachia kiti hicho. Wakati huo akiwa na umri wa
miaka 82 Akihito alisema hali yake ya kiafya sio nzuri na kwamba ilikuwa ngumu
kwake kubeba majukumu ya kiutawala.
0 Comments:
Post a Comment