Wednesday, December 18, 2019

Milioni 500 noti bandia zakamatwa Dar


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limekamata noti bandia kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 500 na kuwatia nguvuni watu watatu wanaosadikiwa kuwa na kiwanda chenye mitambo ya kufyatua noti bandia maeneo ya Chanika Mkoani humo.

Noti bandia zilizokamatwa ni za shilingi elfu kumi kumi ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 103, noti za shilingi elfu tano tano zaidi ya shilingi Milioni106, noti za shilingi elfu mbili zaidi ya Milioni 45, Dola za Marekani zaidi ya shilingi Milioni 300, fedha za Msumbiji zaidi ya shilingi Milioni 3 na fedha za DRC zaidi ya shilingi Milioni 7.

"Tutaendelea na Kampeni hii ya kuwabaini na kuwakamata wote wanaohusika na mtandao huu kisha kuwapeleka Mahakamani" amesema SACP Lazaro Mambosasa Kamishina wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam.

Akizungumzia tukio hilo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga amesema adhabu inayotolewa kwa mujibu wa sheria kwa sasa ni ndogo sana ambapo amependekeza kuwa kuna haja ya kufanya mabadiliko ya sheria ili wanaohusika na vitendo hivyo vya uhujumu uchumi kupata adhabu kali ikiwemo kutengwa katika jamii huku akitolea mfano baadhi ya nchi kunyonga wahusika wa makosa ya Uhujumu uchumi.

Hii imetokea zikiwa siku chache zimepita tangu Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Ole Sabaya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na maofisa wa BOT kukamata noti Bandia zaidi ya shilingi milioni 11 wilayani humo.

0 Comments:

Post a Comment