Mwinjilisti Genoveva Mikomanga, akionyesha kiapo. |
Makamu Mkuu wa Askofu wa
Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT), Dayosisi ya Mwanza Mchg
Henry Kanyumi, amewataka Watumishi wa Mungu kuendelea kuimarisha amani ya nchi
na siyo kuleta migogoro ndani ya makanisa.
Mchg Kanyumi
aliyasema hayo Jumapili Novemba 11, 2019 wakati wa Ibada maalum ya
kumweka wakfu na kusimikwa kazini, Mwinjilisti Genoveva Mikomanga, kuwa
mtumishi katika Kanisa jipya la AICT Mlima wa Mizeituni katika ibada maalumu ambayo ilifanyika Makao Mkao Makuu ya (AICT) Makongoro
Jijini Mwanza wengine waliowekwa wakfu na kusimikwa kazini ni Wazee sita wa
kanisa hilo hafla ambayo iliyoongozwa na Makamu Askofu Mkuu wa kanisa hilo
nchini.
Mchg Kanyumi
alisema katika ulimwengu tuliopo sasa, migogoro imejaa na sasa inaonekana kama
kitu chema na cha kawaida na migogoro hiyo inayoanzia katika familia,
jumuia, vijiji, wilaya, mikoa na hata katika taifa letu kwa jumla.
“Ipo migogoro mingine
baina ya ndugu na ndugu, jirani na jirani na hata pengine ya kabila na kabila,
licha ya ile ya kimataifa, ipo pia migogoro ya kidini yaani kutokuelewana
kati ya Mchungaji na Wazee wa kanisa, Mwinjilisti na wazee unakuta
hawaelewani, madhehebu ya kidini na miongoni mwa waamini wenyewe kwa wenyewe na
migogoro hiyo husababishwa na tamaa ya mali na madaraka, ubinafsi na
chuki,”alisema Makamu Askofu Kanyumi.
Alisema hivi leo kuna
familia ambazo haziwezi kukaa pamoja na kumaliza matatizo yao na badala yake
huchukua njia za vita, ugomvi na hata pengine mauaji kama suluhisho la migogoro
yao, na hiyo yote inatokana na familia hizo kutokuwa na nafasi ya kukaa
pamoja na kuzungumza, watu wanaishi katika ulimwengu wa kuoneana mashaka na
hivyo baadaye kuishia katika fujo.
Mwinjilisti Genoveva Mikomanga (kushoto) akisaini kiapo mara baada ya kusimikwa na Makamu Askofu Mchg Henry Kanyumi (kulia) |
“Mafuta mliyopakwa leo
hapa yanakuwa leseni ya utumishi wenu wa kiroho, inayokupa haki ya kufanya
huduma ya Uinjilisti, Uchungaji ualimu uzee wa kanisa, mmepakwa mafuta haya na
kuweka katika wakfu ili kwenda kuiweka vizuri roho ya utumishi ndani yetu
kutoka kwa Mungu aliye hai hatutegemei kuona mafarakano ndani ya
kanisa,”alisema.
Mchg Kanyumi
aliwataka Watumishi wa Mungu kuacha kuyafanya makanisa wanayoyachunga
kuwa ya kisiasa ili kutunza amani na utulivu katika nchi ya Tanzania , huku
akiwataka Wakristo na wasio Wakristo, ni wajibu kutumia njia ya
mazungumzo ya amani na imani za kimungu ili kufikia makubaliano yoyote na
kusuluhisha migogoro.
Alisema ikiwa kuna
migogoro ya kidini, basi wahusika wakae pamoja na kumaliza migogoro hiyo kwa
amani na utulivu , kwani kila binadamu ana karama zake, lakini pia ana
mapungufu yake, hivyo kukosa ni jambo la kawaida, na pale ambapo tunakoseana
sharti tukiri makosa na kuwa tayari kujisahihisha, tusiwe na kiburi wakati
tunapokosolewa au kusahihishwa.
Katika mahubiri yake
Makamu Askofu Kanyumi, alimzungumzia mtumishi wa Mungu Elisha ambapo majira
yalipowadia Mungu mwenyewe alienda na kumtia mafuta na kuwa mflme hivyo
majira yanapofika na kuwadia hakuna anayeweza kuzuia maana huduma haitoki kwa
mwanadamu bali inatoka kwa Mungu, ambapo alimpongeza Mwinjilisi Genoveva
Mikomangwa kwa hatua aliyofikia na kusimama kama mtumishi Deborah.
Akizungumza mara baada ya
kuwekwa wakfu Mwinjilisti Genoveva Mikomangwa, alisema anamshukuru Mungu
hapa alipofika maana nilianza na kanisa lenye watu 55 hadi sasa ndani ya miezi
mine ana zaidi ya waumini 400.
“Matarajio yangu ni kuona
kanisa la Mungu linaongezeka, linakuwa na kukomaa, hata Bwana Yesu aliwahubiri
watu 3,000 na waliweza kuokoka, hivyo natamani kuliona kanisa la
Mungu, si tu ongozeko la wingi wa watu bali kuona kanisa la Mungu
linakomaa, natamani sana kuendelea kuwafungua wengine waliofungwa katika
utumishi wa Mungu alionipa natamani kusimama kama mtumishi Deborah, liko kusudi
kwani dunia bado ipo gizani,”alisema Mwinjilisti Mikomangwa.
STORY BY: Kija Elias
DATE: Novemba 12, 2019
0 Comments:
Post a Comment