Mkurugenzi wa Miembeni Action and Passion For People with Disability Hussein Msacky |
Taasisi isiyo kuwa ya
kiserikali ya Miembeni Action and Passion For People with Disability,
imewashauri wazazi na walezi kutowaficha majumbani watoto wenye ulemavuna
badala yake imewataka wawapeleke shule wapate elimu, kwani elimu ni haki yao
kama watoto wengine wasiokuwa na ulemavu.
Wito huo umetolewa na
Mkurugenzi wa taasisi Hussein Msacky, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake juu ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwenda kupiga
kura kuchagua viongozi wa Seriakali Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24
mwaka huu.
Alisema mila na desturi
potofu bado zinatajwa kuwa tatizo kubwa linalokwamisha ustawi wa jamii ya kundi
la watu wenye ulemavu ambao endapo watapatiwa elimu kama watoto wengine wana
nafasi kubwa katika kuleta maendeleo hapa nchini.
Alisema katika tafiti za hivi
karibuni ambazo imezifanya taasisi hiyo imebaini kuwa asilimia 95 ya wanaume
katika Manispaa ya Moshi huzitelekeza familia zao pindi wanapozaa mtoto mwenye
ulemavu na hivyo kubaki wakilelewa na upande mmoja wa mama pekee.
Aidha Msacky aliwataka
watunga sheria (BUNGE), kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuweza
kuwadhibiti wanaume ambao wamekuwa wakizikimbia familia zao na kubakia
zikilelewa na mama pekee.
“Mila potofu na vitendo
vya wanaume wengi kuzitelekeza familia zao zenye watoto walemavu, katika
Manispaa ya Moshi imekuwa ni changamoto kubwa, katika tafiti zetu
tumebaini kuwa mama anapojifungua mtoto mwenye ulemavu mwanaume huikimbia
familia hiyo, na wengine huwapa majukumu ya kuwalea watoto wenye ulemavu
wanawake wenye umri mkubwa, hali ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa
kulifanya zoezi la kuwatambua watoto hao kuwa gumu,”alisema Msacky.
Hata hivyo
Msacky aliishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC),
kuzitambua changamoto za watu wenye ulemavu kabla ya kampeni kuanza ili na wao
waweze kushiriki kikamilifu katika kampeni hizo.
“Tunaelekea kwenye
uchaguzi wa Seriakli za Mitaa, wapo watu wenye ulemavu wa kutoona, kusikia,
lakini kutokana na hali zao walizonazo wanahitaji kuwepo na misaada
mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakalimani,”alisema.
Alisema watu wenye
ulemavu mara kwa mara katika maisha ya kila siku wamekuwa wakikabiliwa na
vitendo vya kubaguliwa, wakitengwa na kukataliwa kutokana na ulemavu wao hivyo
tunaiomba serikali za Kata kuwatambua watu wenye ulemavu na kuisimamia
sheria ya uchaguzi kwani kila mtu anahaki sawa ya kuchagua na
kuchaguliwa.
Kwa upande wake Salimu
Rashid Salimu, alisema idadi kubwa ya watu wenye ulemavu, wameendelea kukumbana
na vizuizi vingi katika jamii, wapo ambao wamekuwa wanatengwa katika maisha ya
kijamii, kiuchumi na kiutamaduni na mara kwa mara wamekuwa wakinyimwa haki za
kushiriki katika siasa na kuwa huru kutoa fikra zao.
“Watu wenye ulemavu wengi
wamekuwa wakitamani na wao waweze kufika kwenye mikutano ya kampeni, lakini
wanashindwa kufika kutokana na hali zao, unaweza kuangalia tu hata kwenye
mikutano watu wenye ulemavu ni wachache sana wanaojitokeza kuja kushiriki,”alisema
Salimu.
Aliongeza kusema
kuwa”Tunaiomba tume ya taifa ya Uchaguzi kutenga maeneo maalumu ya watu wenye
ulemavu pindi wanapofika kwenye mikutanio ya kampeni wawe na eneo lao maalumu
pamoja na ulinzi ili hata kama kutatookea vurugu waweze kusaidiwa,”alisema.
Mwezi Novemba mwaka huu,
Watanzania watapiga kura kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa zenye jukumu la
kikatiba la kupeleka madaraka kwa wananchi na kuwahusisha katika shughuli
mbalimbali za kimaendeleo, ambapo mwaka mmoja baadaye, 2020 utafanyika
uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge na Madiwani.
STORY & PHOTO BY: Kija Elias
DATE: Novemba 5, 2019
0 Comments:
Post a Comment